Kiama waliotajwa na CAG

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akiwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma wakati akiwasili katika Ukumbi wa Malaika Jijini Mwanza kufungua mkutano wa majaji wa tathimini ya utendaji wa mahakama na kufanya mapitio ya mpango mkakati wa mahakama 2020/2021 - 2024/2025, jana. Picha na OMR

Mwanza. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameonya viongozi wa taasisi zilizotajwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa matumizi mabaya ya fedha akisema “watapata cha moto.”

Ripoti za CAG Charles Kichere kwa mwaka 2021/22 zilizowasilishwa bungeni jijini Dodoma zimeonyesha ubadhirifu katika taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali, hali ambayo imewaibua wadau mbalimbali, wakitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan amekwishaanza kuchukua hatua kwa kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) na kuivunja Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mbali na hilo, Rais Samia ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka kuhakikisha makatibu wakuu na watendaji wakuu wote wa taasisi za Serikali wanapitia kwa kina taarifa ya CAG, wajibu na kuzifanyia kazi kwa haraka hoja zote.

Pamoja na maagizo hayo, Dk Mpango akiwasalimia wananchi wa Wilaya ya Kwimba juzi wakati akienda shamba la mifugo la Mabuki na kituo cha kunenepesha ng’ombe wa nyama alisema japo Serikali imeanza kuwachukulia hatua, lakini waliohusika na ufujaji fedha za umma watakiona chamoto.

“Ni kweli Serikali ya Mama Samia imeleta fedha nyingi, si tu katika mkoa huu lakini nchi nzima. Hizi ni fedha zenu, ni fedha za kodi, hata hizo nyingine ambazo tunakopa huko bado ni za kwenu, ndiyo maana tunazirudisha kwa kujenga miundombinu ya miradi ya vituo vya afya, zahanati, maji na miundombinu mingine,” alisema.

Katika kusisitiza hilo, Dk Mpango akasema, “kwa hiyo, tumeanza kuwachukulia hatua viongozi wote watakaothibitika kwenye taarifa za GAG au waliokula fedha zenu watapata cha moto.”

Aliwataka viongozi kuhakikisha wanatumia fedha zinazopelekwa kwenye maeneo yao kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuwahudumia wananchi kama zilivyokusudiwa na si kufanyiwa ubadhirifu.

“Nataka niwaombe viongozi wa ngazi zote, fedha hizi zisimamiwe vizuri isipotee hata shilingi, hakikisheni fedha zinazokuja hapa Kwimba, zinazokuja Mkoa wa Mwanza, zinazokuja mikoa mingine ya nchi yetu zinasimamiwa ipasavyo na asiwepo mtu wa kuzidokoa,” alisema.

Dk Mpango aliwataka wananchi kutunza miundombinu inayojengwa na Serikali ili ije iwahudumie baadaye, huku akiwasihi kupanda miti kwa ajili ya kutunza mazingira yatakayoepusha nchi na majanga ya mabadiliko ya tabianchi.

Akiwa katika shamba la Mabuki, Dk Mpango aliiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inaweka utaratibu maalumu wa maofisa mifugo kuanzia ngazi ya kata kuwatambua wafugaji na idadi ya mifugo yao ili kuboresha huduma za ugani na kuongeza tija ya mifugo nchini.

Dk Mpango aliwaonya wananchi wanaovamia shamba hilo, huku akiwataka wazazi kutumia vizuri chuo cha ufugaji Mabuki kwa kuwapeleka vijana wao kujifunza njia bora za ufugaji ili kujiendeleza kiuchumi.

Alisema ni wakati wa kuhakikisha mifugo iliyopo nchini inapata thamani kwa kukuzwa katika ubora unaohitajika ili kupata masoko nje ya nchi.

Awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema Serikali imeweka ng’ombe 500 katika kituo cha Mabuki chini ya usimamizi wa vijana waliowezeshwa na Serikali kuinua zao hilo.

Alisema Serikali inakusudia kuimarisha sekta ya mifugo kwa kutumia vituo atamizi nane vilivyopo maeneo mbalimbali nchini.

Ulega alisema mashamba nane yaliyotengwa na Serikali yatasaidia kuwafundisha vijana na wafugaji kufuga kibiashara ili kusaidia upatikanaji wa mifugo bora itakayotoa nyama inayofaa kuuzwa masoko ya kimataifa.


Maagizo mahakamani

Katika hatua nyingine, Dk Mpango akifungua mkutano wa majaji jijini Mwanza, aliitaka Mahakama kujitathimini kwenye utendaji haki kwa kuwachunguza watumishi wake dhidi ya tuhuma za rushwa aliyosema inaondoa imani kwa wananchi na mhimili huo.

Dk Mpango pia aliutaka mhimili huo ufanye maboresho yatakayopunguza urasimu hasa katika kesi za madai kwa kuwapunguzia gharama za uendeshaji wake wananchi ili wapate haki zao.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alisema mahakama inatarajia kuweka mfumo wa kutoa tafsiri za hukumu kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha nyingine, ikiwemo lugha ya Kiswahili ili kuhakikisha kila mwananchi anaelewa hukumu hizo kupitia njia ya mtandao bila kujali uelewa wa lugha yake.

Kuhusu madai ya rushwa alisema tayari wameiomba Takukuru kuwasaidia kufanya tathmini ya mitazamo, hisia na dhania za wananchi kuhusu rushwa dhidi ya Mahakama.

“Nami napenda kuwageukia watumishi na viongozi wote wa Mahakama na kuwaomba katika Mkutano huu, tufanye tathmini ya uhalisia, mianya, vipenyo, viashiria na perception ya rushwa ambayo wananchi wengi bado wanayo dhidi ya Mahakama,”alisema

Alisema katika mkutano huo watatathmini hatua waliyofikia kukidhi matarajio ya wananchi kwa Mahakama pamoja na kutathmini namna mhimili huo ulivyotimiza matarajio ya Serikali na Benki ya Dunia kuhusu maboresho ya utoaji haki na kutoa Dola za Kimarekani milioni 91 zitumike katika maboresho hayo kuanzia Februari 2022 hadi Desemba 2025.

“Tunapozungumzia tathmini ya maboresho Mahakamani, hatuishii katika mahesabu ya idadi ya majengo bora na ya kisasa nchi nzima, kwa idadi ya vituo vya Mahakama vilivyounganishwa na mifumo ya Tehama au idadi ya Sheria na Kanuni zilizotungwa au kurekebishwa chini ya mpango wa maboresho. Tunapotathmini maboresho tunapima thamani halisi, sio fedha iliyowekezwa bali mabadiliko makubwa yatokanayo,” alisema