Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibano CAG, AG wakishtakiwa mahakamani

Muktasari:

  • Shauri hilo la madai namba 16 ya mwaka 2023 limefunguliwa Mahakama Kuu na wakili wawili wakihoji ubadhirifu wa fedha kwenye mfuko mkuu wa hazina wanaotakiwa kuudhibiti.

Dar es Salaam. Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) zimeburuzwa mahakamani kutokana na madai ya ubadhirifu wa fedha za umma zilizotolewa katika Mfuko wa Hazina kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 na Sheria ya Ukaguzi ya mwaka 2020.

Shauri hilo la madai namba 16 ya mwaka 2023 limefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dodoma na Wakili Alphonce Lusako, akiwakilishwa na Wakili John Seka, dhidi ya CAG na AG.

Hata hivyo, wadaiwa hao wameweka pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo, wakiiomba Mahakama iitupilie mbali bila kuisikiliza, wakibainisha hoja mbili za kuipinga kesi hiyo, suala ambalo limekwama.

Kwanza, wamesema shauri limefunguliwa mahakamani kwa kukiuka kifungu cha 14 cha Sheria ya ukaguzi wa fedha za umma (Public Audit Act, Cap 418 RE 2020), wakibainisha kuwa, kifungu hicho kimempa CAG kinga ya kutoshtakiwa.

Katika hoja ya pili walidai shauri hilo halina mashiko kisheria kwa kuwa linakiuka na kutofuata matakwa ya sheria, Sheria ya Maboresho ya Sheria (kuhusu ajali mbaya na masharti mengineyo) sura ya 310.

Kutokana na hoja hizo waliomba kesi hiyo ifutwe na mlalamikaji alipie gharama za kesi walizotumia.

Lakini Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Deo Nangela Machi 15, 2024 ilitupilia mbali pingamizi hilo baada ya kukataa hoja zote mbili za wadaiwa na kuamuru kuendelea kusikiliza shauri la msingi kwa njia ya maandishi.

Hivyo, wadaiwa, CAG na AG wanapaswa kuwasilisha utetezi Aprili 11, mwaka huu, kujibu hoja za mdai zilizowasilishwa na mlalamikaji, Seka, kabla ya mdai kuwasilisha majibu ya hoja za wadaiwa Aprili 18, 2024, kama ataona ni muhimu kufanya hivyo.

Katika madai yake, Wakili Lusako amerejea ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha wa Juni 30, 2021 kuwa ilionyesha katika mwaka wa fedha wa 2020/21, Serikali ilitoa zaidi ya Sh7.69 bilioni kwa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Ndege katika jengo lake la kusubiria abiria.

Hata hivyo, Lusako anadai kuwa ripoti hiyo ilibaini kuwa, fedha hizo hazikuwa sehemu ya bajeti iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano na ilikuwa kinyume na Sheria ya Bunge.

Anadai kuwa, kwa mujibu wa ripoti hiyo, CAG amerejea kifungu cha 47 (1a) cha Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 kinachosema, fedha hazitatolewa nje ya Mfuko Mkuu wa Hazina isipokuwa kama zimepata kibali cha Bunge.

Lusako anadai kuwa, CAG pia amerejea kifungu cha 4 cha sheria hiyo hiyo kinachosema kuwa, pale ambako matumizi ya fedha kwa ajili ya Serikali na mashirika ya umma yameidhinishwa, yatatumika tu kwa mujibu wa madhumuni yaliyoelezwa na ndani ya mipaka iliyowekwa.

“Katika mwaka wa fedha 2020/21, Sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza ilipokea jumla ya Sh8.33 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza, matumizi ambayo hayakujumuishwa katika Bajeti ya Sekretarieti ya Mwanza.

“Nilibaini kuwa, kati ya jumla ya fedha zilizopokewa, Sh7.69 bilioni zilikuwa mgawo wa fedha kutoka hazina wakati Sh640 milioni zilitoka katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

“Mgawanyo wa fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli ambazo hazijapangwa awali, unaathiri utekelezaji wa shughuli zilizopangwa, zaidi ya hayo unatengeneza mwanya wa matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

“Ninapendekeza Serikali na mamlaka zinazohusika kusimamia uzingatiaji wa Sheria ya Bajeti na kanuni zake kwa madhumuni ya kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana, zaidi ya hayo, taasisi zinahimizwa kuhakikisha utekelezwaji wa miradi ya maendeleo unatengewa bajeti kwanza kabla ya kuanza kufanyika,” imesema sehemu ya ripoti ya CAG.

Kutokana na maelezo hayo, Wakili Lusako amedai kuwa wadaiwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao, kwa kuwa wana majukumu ya kikatiba na kisheria ya kuhakikisha sheria zinakuwepo, zinasimamiwa na kuhakikisha majukumu ya Serikali yanatekelezwa kiasi cha kuhakikisha utajiri wa nchi unatetewa na kulindwa.

Pia, amesema wadaiwa wana wajibu wa kuhakikisha uchumi wa nchi unapangwa na unachochewa kwa njia shirikishi.