Jengo la abiria Uwanja wa Ndege Songwe laanza kutumika

Mwonekano wa nje wa jengo la abiria Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA) uliopo Wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya.
Mbeya. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA) umezindua jengo la kisasa la la abiria lenye uwezo wa kuchukua watu 800 wanaosafiri kwenda ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja lililoanza kujengwa Agosti 9, 2021.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumapili Desemba 24, 2023 ikiwa ni kutekeleza agizo la Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa alilolitoa Desemba 5 mwaka huu mara baada ya kufanya ziara na kubaini kuwepo kwa changamoto ya jengo la kupumzikia abiria ambapo lililokuwepo awali lilikuwa dogo.
Meneja Uwanja wa Ndege, Paschal Kalumbete ameiambia Mwananchi Digital leo Jumapili Desemba 24, 2023 utekelezaji wa mradi huo ni agizo la Waziri Mbarawa ambaye aliwataka kabla ya Desemba 25 jengo hilo lianze kutumika ili kupunguza msongamano wa abiria kwenye jengo dogo.
“Tulikuwa na jengo dogo ambalo lilikuwa likitumiwa na abiria wanaoingia na kutoka mataifa mbalimbali nchini, tunaishukuru Serikali kwani uwepo wa jingo hili jipya utapunguza msongamano wa abiria,”amesema.
Abiria Boaz Dunkey, mkazi wa jijini Mwanza amesema kukamilika kwa jengo hilo kutakuwa chachu kwani awali kulikuwa na msongamano mkubwa wa abiria uliokuwa ukitokana na ufinyu wa miundombinu ya jengo la kupumzikia .
“Unajua abiria unapotumia usafiri wa anga unahitaji kuwa katika utulivu wakati wa kusuburi ndege sasa ule msongamano ulikuwepo unatuathiri kwa kiasi fulani lakini jingo hili kuanza kutumika kutasaidia,”amesema.
Kaimu meneja wa uwanja, Nicholous Mwankunga amesema kikubwa ni kuishukuru Serikali kwa kupanua wigo wa kukamilisha jengo la kisasa la abiria lenye uwezo wa kuchukua watu 800 kwa wakati mmoja hali ambayo itawasaidia kukaa kwa utulivu na usalama zaidi wakati wa kusubiri Ndege na kuhifadhi mizigo.