Kibano miamala ya simu balaa

Kibano miamala ya simu balaa

Muktasari:

  •  Kuanzia siku sita zijazo makato katika huduma za miamala ya simu yatakuwa mara mbili zaidi ya kiwango kilichopo sasa, jambo ambalo wachambuzi wa mambo wanabashiri litapunguza kiwango cha watu kutumia huduma hizo muhimu.


Dar es Salaam. Kuanzia siku sita zijazo makato katika huduma za miamala ya simu yatakuwa mara mbili zaidi ya kiwango kilichopo sasa, jambo ambalo wachambuzi wa mambo wanabashiri litapunguza kiwango cha watu kutumia huduma hizo muhimu.

Hatua hiyo inatokana na bajeti kuu ya Serikali iliyopitishwa na Bunge mwezi uliopita ambayo ilipendekeza kuanza kutoza ya Sh10 hadi Sh10,000 katika kila miamala ya kutuma na kutoa fedha, kulingana na thamani ya muamala husika. Tozo hiyo ni tofauti na viwango vya sasa vilivyokuwepo hivyo itaongezeka juu yake.

Kuanza kwa tozo hizo ni utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/2022 ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alitoa siku 14 hadi Julai 15 kwa watoa huduma wote wa mitandao ya simu kurekebisha mifumo yao na kuanza kutoza tozo hiyo mpya.

Hata hivyo, taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata ni kwamba watoa huduma bado hawajaridhia viwango vilivyopelekwa kwao na siku ya kuanza kwa tozo hizo na mpaka sasa bado wapo katika majadiliano na Serikali ili kufikia mwafaka.

“Kwa makato yanayozidi Sh6,000 pamoja na yale makato yaliyokuwepo kama anayetumiwa yupo hapahapa mjini, mtu ataona ni bora amtume bodaboda. Mfano kumtumia mtu Sh1 milioni na yeye akaitoe jumla ya makato ni zaidi ya Sh31,000,” alisema bosi mmoja wa kampuni ya huduma za simu.

Kwa mujibu wa kanuni ambazo Mwananchi imeziona, zinaonyesha kuwa mtumaji na mtoaji wa fedha watakatwa viwango vinavyofanana.

Kanuni hizi zimesababisha mjadala kwa kuwa utaratibu wa sasa anayetuma fedha hutozwa fedha kidogo kuliko anayetoa.

Kwa kila atakayetuma kuanzia Sh1,000 hadi 1,999 atatozwa Sh10 na kwa muamala wenye thamani zaidi ya Sh3 milioni kiwango cha juu ni Sh10,000.

Kwa miamala ya kutuma fedha kwa sehemu kubwa tozo mpya inayotarajiwa kuanza ni kubwa kuliko yaliyokuwa makato ya awali, mfano kutuma Sh1 milioni M-pesa kwenda M-pesa makato yake ni Sh3,500, nje ya Mpesa ni Sh6,000 lakini kwa muamala huohuo Serikali itatoza Sh8,900 zaidi.

Kwa miamala ya kutuma na kutoa Sh20,000 ambayo haifiki Sh30,000, mtumiaji atatozwa Sh960 zaidi ya kiwango anachotozwa sasa katika mtandao anaoutumia.

Muamala wa kuanzia Sh50,000 hadi Sh99,999 makato ya zaidi ni Sh2,050 huku kwa miamala ya Sh500,000 hadi Sh599,99 makato yatakuwa Sh5,200.

Mkurugenzi wa Shahada za Juu wa Chuo cha Usimamizi wa Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory, alisema kuanza kwa tozo hizo kutafanya huduma za miamala kuwa ghali, hivyo kupunguza watumiaji na kiwango cha miamala inayofanyika.

“Ni kama vile kodi itakuwa inatozwa mara mbili, maana mimi nikimtumia mtu ninakatwa kwa muamala huo, naye akitoa atakatwa tena, huenda kwa baadaye watu wakaacha kutumia miamala hii ya simu na kurudi kwenye njia walizokuwa wakitumia zamani,” alisema Dk Pastory.

Vilevile alisema mara nyingi kuongezeka kwa kodi tozo katika eneo fulani huathiri matumizi katika eneo hilo na mara nyingine limekuwa likifanyika katika bidhaa za anasa, lakini katika miamala ambayo imesaidia kuongeza ushiriki wa watu katika huduma za kifedha kuna uwezekano ushiriki huo ukapungua.

Julai 2, wakati akizungumza na watoa Huduma wa Simu Tanzania, Waziri Mwigulu alisema tozo hiyo mpya ambayo amekuwa akiita ya kizalendo itasaidia Serikali kuanza kukusanya fedha hizo zitakazotumika kuboresha miundombinu na miradi ya maendeleo mbalimbali, ili kuwakwamua wananchi wanaopata adha.

Alisema Serikali imepanga kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ya wananchi na inayohitaji fedha nyingi na jukumu la kukamilisha mchakato huo ni la Watanzania wote wenye uchungu wa maendeleo.

“Fedha zitakazopatikana kwenye tozo hizo hazitatumika kulipa mishahara wala kugharamia matumizi mengine ya Serikali, bali zitapelekwa moja kwa moja kutatua changamoto za afya na elimu.

“Zitaboresha miundombinu ya barabara, miradi ya kimkakati kama ujenzi wa reli ya kisasa na bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere,” alisema Dk Nchemba huku akisisitiza kuwa lengo ni kila Mtanzania kuchangia mapato ya Serikali, huku akiongeza kuwa jambo linalotia moyo ni kuwa Watanzania wameunga mkono kutozwa kodi hiyo.

“Kampuni za simu msichukulie makato haya kama kodi nyingine mnazowatoza wateja wenu. Bali Serikali iliamua kuweka makato haya kwenye miamala ya kuweka muda wa maongezi na kufanya miamala kwa njia ya simu ili watumiaji wengine wa simu wachangie maendeleo ya nchi,” alisema Dk Mwigulu.