Kigogo aonya makundi, mizengwe kuikwamisha CCM chaguzi zijazo
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa (Mnec), Leonard Qwihaya akizungumza wakati alipotembelea ujenzi wa jengo la kitega uchumi cha chama hicho lililopo Kapriponti jijini humo.
Muktasari:
- Wanachama wa CCM mkoani Mwanza wameonywa kutoendeleza siasa za makundi wanapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mwanza. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi ( CCM) Taifa, Leonard Qwihaya ameeleza kukerwa na makundi ndani ya chama hicho, akisema yatakikwamisha chama hicho kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na ule mkuu wa 2025.
Ameyasema hayo jana Desemba 31, 2023 wakati wa kukabidhi vifaa vya ujenzi vyenye thamani zaidi ya Sh67 milioni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za chama kwenye kata 38 za Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela.
Qwihaya amewasihi viongozi wa chama hicho kujipanga na uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.
"Uchaguzi wa serikali za mitaa ni uchaguzi wa kutolea macho, tukikwama hapo maana yake uchaguzi mkubwa wa 2025 tunakwenda kuumia,” amesema.
“Ili usiwe mtoa taarifa, kwanza ondoa makundi, kwani jiji letu tunaumizwa sana na makundi kuna watu chungu nzima wanaipenda Mwanza, lakini wanashindwa kuja kusaidia kwa sababu ya maneno yetu.Mtu akitaka kufanya kitu anatengenezewa zengwe ili asifanye wakati ni ya kwetu sote," amesema Qwihaya
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omary Mtuwa amewataka viongozi na wanachama wa mkoa huo kuacha kuwaonea wivu, chuki na roho mbaya watu ambao wanatoa vitu vya kufanya maendeleo.
"Tatizo lililopo kwetu sisi vijana na baadhi ya viongozi wa CCM ni nongwa, wivu, chuki na roho mbaya. Mtu akifanya vizuri anatafutiwa zengwe.
“Leo mwenyekiti wa seneti na wenzake wameandaa hili hawana mpango wa kugombea ubunge au udiwani Nyamagana, wao wanatengeneza wasifu wao kwa baadaye," amesema Mtuwa.