Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kigogo wa Al-Qaeda aliyelipua ubalozi wa Dar auawa kijasusi

Muktasari:

  • Rais Joe Biden alisema ametoa kibali cha mwisho cha “mashambulizi ya usahihi” dhidi ya kiongozi huyo wa al-Qaeda baada ya miezi kadhaa ya kupanga shambulizi.

Rais Joe Biden alisema ametoa kibali cha mwisho cha “mashambulizi ya usahihi” dhidi ya kiongozi huyo wa al-Qaeda baada ya miezi kadhaa ya kupanga shambulizi.


Marekani. Zikiwa zimesalia siku 36 kabla ya kumbukumbu ya miaka 24 ya shambulio la bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika balozi za Marekani jijini Dar es Salaam na Nairobi Agosti 7, 1998, aliyekuwa kiungo muhimu katika shambulio hilo, Ayman al-Zawahiri, ameuawa.

Mauaji hayo yaliyofanywa katika shambulio la ndege isiyo na rubani lilitekelezwa na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Akithibitisha kuuawa kwa Zawahiri, Rais Joe Biden wa Marekani alisema huyo ndiye amekuwa akichangia mfululizo wa mauaji na ghasia dhidi ya raia wa Marekani.

Pia alihusika katika shambulio kubwa dhidi ya Marekani yenyewe Septemba 11, 2001, ambalo lilisababisha vifo vya watu 3,000 nchini Marekani.

Al-Zawahiri alikuwa daktari wa upasuaji wa macho ambaye alifanikisha kupatikana kwa kundi la wanamgambo wa Islamic Jihad la Misri. Baada ya Marekani kudai kuwa walimuua Osama bin Laden Mei 2011, Zawahiri alitwaa uongozi wa Al-Qaeda.

Maofisa wa CIA walisema Zawahiri alikuwa kwenye balkoni ya nyumba wakati ndege isiyo na rubani ilipomrushia makombora mawili na kufariki papo hapo.

Walieleza kuwa wanafamilia wengine walikuwepo wakati wa tukio hilo, lakini hawakujeruhiwa na ni Zawahiri pekee aliyeuawa.

Biden alisema ametoa kibali cha mwisho cha “mashambulizi ya usahihi” dhidi ya kiongozi huyo wa al-Qaeda mwenye umri wa miaka 71 baada ya miezi kadhaa ya kupanga. “Haijalishi itachukua muda gani, haijalishi utajificha wapi, ikiwa wewe ni tishio kwa watu wetu, Marekani itakupata na kukuondoa,” alisema Biden na kuongeza kuwa “hatutasita kutetea taifa letu na watu wake”.

Biden alisema Zawahiri pia alipanga vitendo vingine vya vurugu, ikiwa ni pamoja na shambulio la kujitoa mhanga kwa meli ya kivita ya USS Cole huko Aden mnamo Oktoba 2000 ambayo iliua mabaharia 17 wa Marekani.

Shirika la habari la CBC News limesema kuwa vyanzo vitatu vimethibitisha mauaji hayo ya kiongozi huyo wa al-Qaeda, vikiwamo New York Times, Washington Post na CNN vimenukuu vyanzo visivyojulikana vikimtambua muathiriwa.

Kwa mujibu wa habari hizo, maofisa wa Marekani walisema operesheni ya kumuua ilifanyika nchini Afghanistan na hakukuwa na raia waliojeruhiwa. Baada ya shambulio la Septemba 11, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa zawadi ya Dola za Marekani milioni 25 kwa taarifa au taarifa za kiintelijensia zitakazowezesha kukamatwa kwa Ayman Al-Zawahiri.

Katika taarifa kwa waandishi wa habari, Serikali ya Marekani ilisema operesheni hiyo ilifanikiwa na hakukuwa na majeruhi miongoni mwa raia.

Serikali hiyo imesema Al-Zawahiri aliuawa Julai 31 mwaka huu, lakini taarifa za kuuawa zilicheleweshwa kwa siku mbili ili kutoa muda wa uthibitisho sahihi operesheni hiyo.

Rais Joe Biden alitangaza katika Ikulu ya White House kuwa CIA ilikuwa imegundua Zawahiri alipokuwa akihamia katikati mwa jiji la Kabul mapema 2022 na aliidhinisha operesheni wiki moja kabla.

Rais Biden aliipongeza operesheni hiyo kama ushindi mkubwa katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi nje ya Marekani.

Biden alisema ana matumaini kuwa mauaji ya Al-Zawahiri yanaweza kutoa muda wa afueni kwa wanafamilia waliouawa katika mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001.

Rais Biden alifahamishwa kwa mara ya kwanza kuhusu alipo Al-Zawahiri Aprili na hatimaye alifahamishwa kuhusu operesheni iliyopendekezwa kuanza Julai 1, 2022, ofisa wa utawala aliwaambia waandishi wa habari.

Wajumbe na washauri wakuu wa Baraza la Mawaziri walikutana Julai 25 ili kupokea taarifa ya mwisho kuhusu tathmini ya upelelezi, ambayo ofisa huyo alisema iliendelea kuboreshwa kila siku.

“Rais alipokea ripoti ya utekelezaji ... Aliuliza tena kuhusu njia nyingine zozote ambazo zingepunguza majeruhi kwa raia. Alitaka kuelewa zaidi kuhusu mpangilio wa vyumba (vya nyumba ya Al-Zawahiri huko Kabul).

“Wakati wa kuhitimisha mkutano huo, Rais aliidhinisha shambulio la anga lililowekwa maalumu kwa sharti kuwa lipunguze kwa kadiri iwezekanavyo hatari ya vifo vya raia. Uidhinishaji huu ulimaanisha kuwa Serikali ya Marekani inaweza kufanya shambulio la anga pindi fursa itakapopatikana,” alisema ofisa huyo.

“Marekani ina imani kupitia vyanzo vya kijasusi na “mikondo mingi ya kijasusi kwamba aliuawa na hakuna mtu mwingine,” ofisa huyo alisema.

Shambulio dhidi ya Al-Zawahiri linakuja karibu mwaka mmoja baada ya Biden kusimamia uondoaji wa jeshi la Marekani kutoka Afghanistan kufuatia miongo miwili ya vita.


Mashambulizi ya Kigaidi Dar, Nairobi

Mashambulizi ya kigaidi katika balozi za Marekani zilizoko Dar es Salaam na Nairobi yalifanyika mchana wa Ijumaa ya Agosti 7, 1998 kwa wakati mmoja. Zaidi ya watu 200 waliuawa katika shambulio hilo

Mashambulizi hayo yaliyodaiwa kutekelezwa na kundi la Al-Qaeda yaliongozwa na Osama bin Laden na Ayman Al-Zawahiri na kulifanya Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kumweka Bin Laden kwenye orodha yake ya watu kumi wanaotafutwa zaidi duniani.

Kulingana na mwandishi Lawrence Wright katika kitabu chake, ‘The looming tower: Al-Qaeda and the Road to 9/11’, oparesheni ya Nairobi ilipewa jina la ‘Kaaba Takatifu’ na mlipuko wa bomu Dar es Salaam uliitwa ‘Operesheni al-Aqsa’.

Ilidaiwa kuwa mtu aliyeitwa Sheikh Ahmed Salim Swedan alinunua lori la aina ya Toyota Dyna jijini Nairobi na lori la friji la Nissan Atlas la mwaka 1987 jijini Dar es Salaam. Magari hayo ndiyo yalitumika kubeba mabomu hayo kwenda katika balozi hizo.

FBI ilisema Juni 1998, mtu aliyeitwa KK Mohamed alikodisha nyumba namba 213 wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, kama kilomita sita kutoka ubalozi wa Marekani, na alikuwa akitumia gari aina ya Suzuki Samurai nyeupe kubebea vifaa vilivyotengeneza mabomu hayo, vilivyofichwa kwenye magunia ya mchele kufikishwa nyumbani hapo.

Katika miji ya Nairobi na Dar es Salaam, Mohammed Odeh alisimamia ujenzi wa mabomu hayo ambayo jumla yake yalikuwa na kilo 900.

Agosti 7 washambuliaji wa kujitoa mhanga wakiwa kwenye malori yaliyoegeshwa nje ya balozi hizo za Dar es Salaam na Nairobi yaliyokuwa na vilipuzi na yalilipuka kwa wakati mmoja. Watu 213 waliuawa katika mlipuko wa Nairobi, huku 11 wakiuawa Dar es Salaam.