Kigwangalla afichua maumivu aliyopata kwa kukosa uwaziri

Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk Hamisi Kigwangalla akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa gazeti la Mwananchi.

Na Noor Shija

Dodoma. “Kukosa uwaziri kuliniumiza ama la. Sidhani kama ni jambo ambalo ninaweza nikalielezea, ila kuna baadhi ya mambo yaliyoendana na mimi kukosa uwaziri, kwa kweli yaliniumiza,” hiyo ni kauli ya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla.

Kigwangalla aliyeanzia nafasi ya naibu waziri wa afya na baadaye kuteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake jijini Dodoma.

Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa iwapo ameumia kukosa kuteuliwa nafasi ya uwaziri na hasa alivyopotea kwa muda kwenye akaunti yake ya ‘twitter’ ambako baadhi ya wafuasi wake walidai kukosa uwaziri kumemfanya aumie moyoni.

Rais wa tano, John Magufuli alimteua Kigwangalla kwenye baraza lake la kwanza la mawaziri kwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Oktoba, 2017 Rais Magufuli alifanya mabadiliko kwenye baraza la mawaziri na kumteua Kigwangalla kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, lakini baada ya Uchaguzi Mkuu 2020, Rais Magufuli hakumteua kwenye nafasi ya uwaziri.

Kigwangalla kwa mara ya kwanza aliingia bungeni katika Uchaguzi Mkuu 2010 baada ya CCM kumteua kugombea ubunge jimbo la Nzega, lakini Rais aliyekuwa madarakani wakati huo, Jakaya Kikwete hakumteua kushika nafasi ya uwaziri.

Chaguo la wana Nzega kwa wakati huo lilikuwa Hussein Bashe, ambaye katika kura za maoni alishinda na kuwaacha mbali mbunge aliyekuwa akimaliza muda wake, Lucas Selelii, huku Kigwangalla akishika nafasi ya tatu.

“Kwa hivyo mimi nilisemwa mambo mengi na watu kutoana na kukosekana kwenye baraza la mawaziri baada ya Mheshimiwa Magufuli kuunda upya Serikali yake.

“Maneno niliyosemwa ni mengi na unajua kwenye siasa mtu hujifunza kwa kipindi kifupi nilichojaaliwa kukaa huko ndani ni kwamba ukishasemwa, ukishachafuka huna namna ya kujisafisha. Yaani kilichosemwa ndio hicho. Kwa hivyo wewe kama una hekima na busara ni kunyamaza kwa sababu hautoweza kusema upande wako wa hadithi na ukaeleweka hususani kwenye social netwok,” alisema Kigwangalla amabye kwa sasa ni mbunge wa Nzega Vijijini.

Kuukosa uwaziri

“Sidhani kama ni jambo ambalo ninaweza nikalielezea, ila kuna baadhi ya mambo yaliyoendana na mimi kukosa uwaziri, kwa kweli yaliniumiza.

“Kwa mfano, unajua kwa bahati mbaya sisi viongozi tukiwa kwenye Serikali kule jambo likishasemwa na mkubwa hata kama haliko sahihi huwezi kulifafanua kwa kuwa limetoka kwenye kinywa cha bosi, mtu mkubwa, huwezi kufafanua.

“Kwa hiyo kuna jambo linaweza likasemwa siyo kweli, siyo sahihi, lakini kwa sababu limesemwa na mkubwa, kiutumishi, kiungwana, maadili ya kitaaluma ya utendaji kazi ndani ya Serikali yanakuzuia wewe kufafanua.

“Kwa hivyo unatulia, akiamua yeye yule mkubwa baada ya kupata ukweli ama baada ya wewe kuja kinyumenyume na kumletea taarifa sahihi, akafuatilia akaelewa kinachoendelea ama kilichotokea, akipenda anaweza akarekebisha kauli aliyotoa mwanzo ama anaweza akaacha kama ilivyo, lakini akachukua hatua tofauti na zile ambazo alizichukua mwanzoni.

“Kwa hivyo, kuna baadhi ya mambo yalisemwa kwa kweli yaliniumiza ambayo sitopenda kuyajadili kama nilivyosema kwa heshima ya mamlaka, lakini hayo ndiyo yaliyoniumiza,” alisema Kigwangalla.

Kwa nini hakuumia

Pia, Kigwangalla alisema kwa namna nyingine hakuumia baada ya kuachwa na Rais Magufuli kwenye baraza la mawaziri baada ya kuchaguliwa kuongoza nchi kwa kipindi cha pili. Kwa sasa Rais Magufuli ni marehemu.

“Kwamba niliteuliwa au sikuteuliwa, sikuumia kwa sababu unapokuwa mwanasiasa hususani sisi tunaomba nafasi ya ubunge ama uwakilishi wa wananchi, hii nyongeza aidha umeteuliwa kuwa naibu waziri ama umeteuliwa kuwa waziri ni majaaliwa yanayojitokeza baadaye.

“Lakini kazi ya uhakika uliyoomba ni ule ubunge, lakini pia katika Bunge ambalo lina wabunge takriban 392, mamlaka ya uteuzi kwa maana ya Rais kwa nafasi ile ambayo nilikuwa nayo kipindi kilichopita ya uwaziri, ina ‘choice’ (uchaguzi) kubwa, ina ‘choice’ pana.

“Lakini pia mamlaka ile hailazimishwi, ichague, ama iteue viongozi hao kutoka tu ndani ya Bunge. Nafikiri umeona imeteua wengine nje ya Bunge, kutokana na nini utashi wake, lakini pia inavyojisikia, yaani wanasema ‘at the presure of the president’. Unakuwa waziri ama unakuwa siyo waziri kwa raha ya Rais.

“Kwa hivyo, kama ikimpendeza Rais akakuteua utakuwa waziri na anaweza akapendezwa kuteua waziri nje ya wale wabunge 392. Kwa maana hiyo ana uwanda mpana wa takriban watu milioni 60 kuteua mawaziri labda 40 ama 60 kutegemea anavyotaka Serikali yake iwe kubwa kiasi gani.

“Kwa hiyo siyo jambo la kukusononesha, kukuumiza kwa sababu Rais ana miaka mitano, wakati wote huo anaweza kurekebisha Serikali yake, inaweza ikatokea akamteua mtu ambaye hakumteua mwanzoni na akamtoa mtu aliyemteua mwanzoni na hakuna atakayehoji, kwa nini kamteua huyu kwa nini kamuacha huyu.

“Hakuna mtu atakayehoji kwa watu wanaoelewa, kwa mtu asiyeelewa anasema Kigwangalla alikuwa sahihi, lazima alikuwa apate uwaziri, kwa nini Kigwangalla ameachwa.

“Sasa ni utashi wao siyo utashi wa mamlaka na huwezi kupigia ramli hilo jambo kwamba nitakuwa waziri tu, hapa kama unajielewa na bahati nzuri mimi siyo mgeni kwenye siasa sasa huu ni mwaka wa wangu wa 11.