Kiini tozo za simu zilizozua mjadala

Muktasari:

  • Mjadala wa tozo katika miamala ya simu umeshika kasi, ulifikia katika kikao cha mawaziri kilichokuwa na lengo na kufanya mapitio baada ya malalamiko ya wananchi.

Dar es Salaam. Wakati wananchi wakisubiri matokeo ya mapitio ya Serikali kuhusu malalamiko ya tozo za miamala ya simu, watu kadhaa watabaki katika historia kama wahusika muhimu kwa namna walivyoshiriki katika mjadala huo uliolitikisa Taifa.

Ni kutokana na mjadala huo ulioanzia kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, uhusika wa watu hao umesababisha hadi Rais Samia Suluhu Hassan kuwaagiza mawaziri husika kulifanyia kazi suala hilo.

Wakizungumza juzi kupitia televisheni ya Channel Ten, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na mwenzake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile walieleza jinsi watakavyoshirikiana kutekeleza maagizo hayo ya Rais Samia.


Sakata lilipoanzia

Februari 2021, Dk Mwigulu akiwa Waziri wa Katiba na Sheria alimwakilisha aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (sasa makamu wa Rais) kuwasilisha bungeni mwongozo wa maandalizi ya mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.

Katika mwongozo huo, Mwigulu alisema Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh36.26 trilioni ikiwa na vipaumbele vya ukuaji uchumi, utawala bora na maendeleo ya watu.

Baada ya Rais Samia kuchukua madaraka Machi 19 kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, Machi 31 alitangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kumkabidhi mikoba ya Wizara ya Fedha, Dk Mwigulu.


Bunge lapitisha tozo

Dk Nchemba aliingia wizarani wakati Bunge la Bajeti likiendelea jijini Dodoma na maandalizi ya Bajeti ya Serikali yakiendelea huku akikuna kichwa kupata vyanzo vya mapato.

Katikati ya mjadala, Aprili 20, Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu aliishauri Serikali kutoza watumiaji wa simu Sh50 kila siku ikiwa ni sehemu ya vyanzo vya kuongeza mapato ya Serikali.

“Miaka yote tunapigania ada ya simu. Ethiopia miradi yote inaendeshwa na tozo katika simu. Tukitoza Sh50 tuna wenye kadi (laini za simu) wasiozidi milioni 52, tuchukue watu wachache kama milioni 30, wale ambao wataweza kulipa Sh50 kwa siku, tutaishia kupata Sh540 bilioni.

“Tutafute vyanzo vipya, TRA msidumae tu kukamata Bakhresa, Mohamed Dewji, tafuteni vyanzo vipya, kuna fedha nyingi kwenye simu,” alisema Zungu.

Kwa kuonyesha kukubaliana na wazo la Zungu, akisoma Bajeti ya Serikali Juni 10, Dk Mwigulu alipendekeza kuingiza tozo kwenye miamala ya simu na muda wa maongezi.

Alipendekeza tozo ya Sh10 hadi Sh10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa.

“Kiasi cha tozo kinatofautiana kulingana na thamani ya muamala wa fedha unaotumwa au kutolewa. Pendekezo hili litaongeza mapato ya Serikali kiasi cha Sh1.265 trilioni,” alisema Dk Nchemba.

Pia, alipendekeza kutoza kati ya Sh10 hadi Sh200 kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji akisema pendekezo hilo lingeongeza mapato ya Serikali Sh396.306 bilioni.”

Baada ya mjadala mrefu, Bunge lilipitisha Bajeti kwa asilimia 94 ya wabunge 361 wakikubali huku wengine 23, sawa na asilimia 6 wakipiga kura ya kutokuwa na upande.

“Kwa asilimia hii ya upitishaji wa bajeti, maana yake Bunge lina imani kubwa sana na Serikali,” alisema Spika Job Ndugai alipotangaza matokeo ya kura za kupitisha Bajeti hiyo Juni 22, kabla ya Sheria ya Fedha kusainiwa na Rais Samia Juni 30.


Watetea tozo

Baada ya kupitishwa kwa Bajeti hiyo, ndipo mjadala ukaibuka, hasa kuhusu makali ya tozo kwenye miamala ya simu.

Kwa upande mmoja, Dk Mwigulu na baadhi ya wabunge wamekuwa wakieleza umuhimu wa tozo hiyo, huku wadau wengine, hasa wanaharakati na wasomi wakieleza maumivu yake.

Katika maelezo yake alipofanya mahojiano katika kipindi cha 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Dk Mwigulu aliita tozo hiyo ya “mshikamano”.

“Kwenye chungu, ni lazima bajeti, fedha zitatoka wapi ni lazima tutoe kodi, mwaka huu tumeleta kodi ya miamala, ni vizuri sana mjue hili la kwenye miamala si tu kodi, hili tunatunisha mfuko, ni solidarity fund, huu ni mfuko wa mshikamano wa Watanzania,” alisema Dk Mwigulu.

Mbali na Mwigulu, baadhi ya wabunge walionekana wakipigia kampeni tozo hiyo, akiwamo Mariam Ditopile, Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Dodoma.

“Tumuunge mkono Rais Samia katika hili la ukusanyaji wa kodi za miamala, tukumbuke wakati Rais anahutubia Bunge alitueleza wazi kuwa uchumi wetu umeshuka kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 4.7 kutokana na athari za corona. Hivyo ni lazima Serikali ichukue hatua za kurejesha uchumi wetu,” alisema Ditopile.

Naye Mbunge wa Buchosa, Erick Shigongo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Julai 18, alisema suala la tozo lilipoletwa bungeni walilikubali ili kuepusha nchi isiwe masikini.

“Tukasema tuna uamuzi mmoja wa kuwaomba Watanzania kama alivyosema Baba wa Taifa (Julius Nyerere) mwaka 1979 wakati wa vita ya Uganda, akasema ‘fungeni mikanda kwa miezi 18’, tukasema tutafunga mikanda kwa miezi 18 au zaidi, lakini tukusanye fedha tusiache uchumi uanguke,” alisema Shigongo.

Alisema yeye kama mbunge aliunga mkono tozo hiyo akiamini ni mateso ya muda.

“Baadaye tutakapoanza kuuza umeme wetu, wawekezaji watakapokuja, shida hii tunayoipata itakwisha,” alisema.


Maumivu yalipoanza

Tozo hiyo imeanza kutumika Julai 15 na hapo ndipo wadau, zikiwemo kampuni za simu, mawakala wa mitandao ya simu na watumiaji wa huduma za fedha za simu walipiga kelele mitaani na kwenye vyombo vya habari.

Akizungumzia usawa wa kodi, Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPFS), Francis Nanai alisema mfumo mzuri wa kodi ni ule unaowahusisha watu wengi, huku kodi ikitozwa kwa viwango vidogo.

“Wazo la kuanzisha kodi ya miamala lilikuwa zuri ila viwango vinavyotozwa ndio si rafiki. TPSF tunasikia malalamiko lakini tunaamini hakuna linaloshindikana. Serikali ikae na wadau kujadili upya viwango hivi na benki zisiachwe katika hili.

“Kutokana na teknolojia, simu nayo ni benki. Wapo watu wanakopa au kuweka akiba kwenye simu zao,” alisema Nanai.


Serikali yajirudi

Baada ya kilio kukolea, Julai 19, Dk Mwigulu na Dk Ndugulile walitangaza kupewa agizo la Rais Samia kufanyia kazi malalamiko hayo.

Wakati suala hilo pia likishughulikiwa chini ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msingwa amesema lengo la tozo hiyo ilikuwa ni kuboresha huduma za kijamii, hususan maeneo ya vijijini na ilianzishwa ikiwa ni juhudi za Serikali kupanua wigo wa kodi ili kupata fedha za kuhudumia wananchi...tuna tatizo kubwa la barabara vijijini.

Hili jambo ukikaa huku Dar es Salaam unaweza kuliona kama dogo, lakini vijijini huko hakuna barabara,” alisema.