Kijana aua mpenzi wa mama, kisa anapendelewa

Muktasari:

  •  Idrisa Baltazari aliyekuwa na umri wa miaka 30 alimuua Manzi Yambayamba aliyekuwa akiishi na mama yake mzazi. Idrisa alikasirishwa na mahusiano hayo na kumshambulia Yambayamba kwa mpini wa jembe. Hukumu ya Jaji Eliamin Laitaika imemhukumu Idrisa kifungo cha miaka minne jela kwa kukiri kosa la kuua bila kukusudia.

Moshi. Kwa mila na tamaduni za Kitanzania, si hulka ya mtoto wa kiume kupinga mahusiano ya mama yake na mwanamume, lakini si kwa Idrisa Baltazari, ambaye hakuridhishwa na uamuzi wa mama kuishi kinyumba na Manzi Yambayamba.

Hii ilimfanya Idrisa ambaye alikuwa na umri wa miaka 30 kumuua Yambayamba aliyekuwa akiishi kinyumba na mama yake mzazi, Salima Seleman ambaye ni mjane, akimtuhumu mama yake kumpendelea mwanamume huyo.

Leo hii, Idrisa ambaye ana umri wa miaka 34, mkazi wa Kijiji cha Moneka, wilayani Newala mkoani Mtwara, anatumikia kifungo cha miaka minne jela kwa kukiri kosa dogo la kumuua Yambayamba pasipo kukusudia, Oktoba 12, 2019.

Hukumu hiyo ambayo ilipatikana jana Februari 6, 2024 katika tovuti ya Mahakama, ilitolewa Septemba 22, 2023 na Jaji Eliamin Laitaika wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, ambaye alisema sheria inataka watu waishi kwa kuvumiliana.

“Kila mmoja anapaswa kuheshimu chaguo la mwenzake. Hata pale chaguo hilo linakuwa halikubaliki, hakuna mtu mwenye haki ya kujichukulia sheria mkononi ili tu kushinikiza kile ambacho hakubaliani nacho,” anasema Jaji katika hukumu hiyo.

“Hii ni kweli hasa inapokuja kwa mzazi kufanya chaguo ambalo haliwaridhishi watoto. Katika shauri hili, kijana alijichukulia sheria mkononi kupinga chaguo la mama yake kuishi na mwanamume mwingine baada ya kuwa mjane. Alimuua mpenzi wa mama yake katika ugomvi wa kitoto,” alieleza Jaji Laitaika.

Ilikuwaje?

Kulingana na taarifa isiyobishaniwa iliyotengenezwa kwa kuegemea mwenendo wa usikilizwaji wa awali (PH) na aliposomewa mashtaka Mei 3, 2023 ni kwamba, marehemu na mshtakiwa ni watu waliokuwa wanafahamiana vyema kijijini.

Hukumu ya Jaji Laitaika inaeleza mshtakiwa ni mtoto wa kiume wa Salima Selemani, ambaye ni mjane, aliyekuwa akiishi kinyumba na Yambayamba (sasa marehemu).

“Inavyoonekana mshtakiwa hakufurahishwa na mahusiano hayo, kwa hiyo siku ya tukio alienda nyumbani kwa mama yake usiku wa manane, akafungua mlango na kukutana na baba yake wa kambo akiwa amelala,” inaeleza hukumu.

Jaji katika hukumu anaeleza, “Mama yake alikuwa macho. Mshtakiwa akaamuru apewe sigara na Yambayamba. Mama yake akajibu kuwa amelala na kulikuwa hakuna sigara. Mshtakiwa alishikwa hasira, akamtuhumu mama yake kwa kumpendelea Yambayamba.”

Hapo akaanza kumpiga mama yake kwa kutumia mikono, mama yake akajaribu kumwamsha mpenzi wake lakini hakuamka kwa vile alikuwa amekunywa pombe ya kienyeji mchana kutwa katika sherehe iliyokuwa imefanyika kijijini hapo.

Ili kuokoa maisha yake, mama wa mshtakiwa aliamua kutoroka eneo hilo na kumwacha mshtakiwa na Yambayamba ndani ya nyumba na inavyoonekana, baadaye kuliibuka ugomvi baina yao, huku mwanamume huyo akiwa mlevi.

“Katikati ya ugomvi huo, mshtakiwa alichukua mpini wa jembe na kumshambulia Yambayamba kwenye paji la uso. Baada ya kuona mgomvi wake amepoteza fahamu, alimbeba na kuenda kumtupa kwenye shamba la mikorosho,” inaeleza hukumu.

Mwili wa marehemu ulipatikana na mshtakiwa akakamatwa na kushtakiwa.


Ilivyokuwa mahakamani

Septemba 12, 2023 kesi hiyo ilipoitwa Mahakama Kuu Mtwara kwa ajili ya kusomewa shtaka la kuua kwa kukusudia, mshtakiwa aliyekuwa akitetewa na wakili Emmanuel Ngongi, badala yake alikiri kosa la kuua pasipo kukusudia.

Hapakuwa na pingamizi kutoka kwa mawakili wa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu, Wilbroad Ndunguru aliyeshirikiana na wakili wa Serikali Edson Mwapili na hivyo Jaji Laitaika alimtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Akiwasilisha maombolezo kwa niaba ya mteja wake, Wakili Ngongi aliiomba mahakama imwachie huru na hata kama itaamua kumpa adhabu ya kifungo, basi impe kidogo ikizingatiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza.

Pia aliiomba mahakama izingatie muda aliokaa rumande wa takriban miaka mitatu.

Hata hivyo, kwa upande wao mawakili wa Jamhuri waliikumbusha mahakama juu ya Ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania ambayo inatoa haki ya mtu kuishi na hakuna mtu mwenye haki ya kuondoa uhai wa mtu kama alivyofanya mshtakiwa.

Pia Wakili Ndunguru kwa niaba ya Jamhuri, alieleza kuwa matukio ya mauaji yanaongezeka si kwa Mtwara tu, bali hata maeneo mengine ya Tanzania hivyo mahakama itoe adhabu kali itakayotuma ujumbe kwa jamii kuheshimu sheria.

Baada ya kusikiliza maombolezo hayo, Jaji Laitaika alisema hakuna ubishi kuwa kitendo cha mshtakiwa kumshambulia Yambayamba akiwa usingizini, amelewa na hana msaada na kumpiga kwa mpini ni cha kutisha na kisicho cha kibinadamu.

Jaji alisema kama kesi hiyo ingeenda hadi hatua ya kusikiliza ushahidi na kupokea vielelezo, kama mshtakiwa angetiwa hatiani angehukumiwa kifungo cha maisha.

Hata hivyo, Jaji alisema kwa kukiri kosa imepunguza kiwango cha adhabu na kulingana na mwongozo wa adhabu kifungo kinaanzia miaka 10 kushuka chini hivyo, anapunguza miaka mitatu aliyokaa gerezani na miaka mingine mitatu.

Kwa msingi huo, Jaji alimhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne jela.