Kikeke wa BBC kurejea nchini baada ya miaka 17

Salim Kikeke

Muktasari:

  • Miaka 17 ya utumishi wake katika studio za Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) imemfanya kuwa miongoni mwa Watanzania wenye mafanikio zaidi katika fani ya uandishi wa habari na utangazaji.

Dar es Salaam. Jina la Salim Kikeke ni maarufu katika uga wa habari ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Miaka 17 ya utumishi wake katika studio za Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) imemfanya kuwa miongoni mwa Watanzania wenye mafanikio zaidi katika fani ya uandishi wa habari na utangazaji.

Mtangazaji huyu mahiri wa kipindi cha Dira ya Dunia, alitua Jiji la London nchini Uingereza mwaka 2003 na alianza kuaminiwa taratibu katika shirika hilo.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Kikeke anaweka wazi nia yake ya kurejea Tanzania ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kupokea wito wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai. Anarejea nyumbani si kwa kustaafu BBC bali kuja kulitumikia Taifa kwa umri wake usiofikia miaka 50.

“Ni kweli, mapema mwaka huu nilipokuwa Dodoma kwenye shughuli zangu za kikazi, nilipata heshima ya kualikwa na Spika Job Ndugai bungeni. Nilikuwa na mpiga picha wangu Nicholaus Mtenga na tulikaribishwa kwenye ‘gallery’.”

“Kualikwa na Spika kwa ajili ya kutushukuru kazi nzuri tunayofanya na kuwakilisha Taifa kimataifa ni tunu kwangu na heshima kubwa. Mimi niko tayari kurudi Tanzania. Nimekuwa tayari kwa muda mrefu tu, ni wakati muafaka ndio nilikuwa nasubiri na nadhani muda huo pengine uko karibu kuliko ninavyofikiri,” alisema.

“Tanzania ni nyumbani. Na waswahili wanasema, nyumbani ni nyumbani. Kwa hiyo utayari upo na ulikuwepo tangu siku ya kwanza nilipopanda British Airways kuelekea London miaka takriban 17 iliyopita. Mwezi Mei mwaka huu natimiza miaka 18 Uingereza.”

Kikeke alisema angependa kurejea hata leo lakini kuna mambo lazima ayakamilishe na kwamba kabla ya mwaka huu kumalizika atarejea nchini.

Kuhusu kilichomvutia kurejea nchini alisema, “kurejea nyumbani huhitaji kushawishiwa. Mkataa kwao daima ni mtumwa, kwa hiyo sikulazimika kushawishiwa wazo la kurudi Tanzania. Tangu naondoka nilikuwa najua fika kuwa iko siku nitarejea wakati muafaka utakapowadia. Wito wa Spika Ndugai kwa kweli naweza kusema umechochea zaidi hamu yangu ya kutaka kurejea mapema zaidi kuliko nilivyotarajia.”

Alisema amekuwa akirudi likizo nchini kila mwaka na wakati mwingine zaidi ya mara moja kwa mwaka.

“Huwa natazama hali yangu kama ya mtu aliyetoka mkoani na kwenda Dar es Salaam kutafuta maisha, utaona baadhi inapofika wakati fulani huamua kurejea makwao kuwekeza au kuishi baada ya kupata uzoefu wa kutosha,” alisema

Kuhusu kurejea kwake nchini kufanya kazi serikali au kwenye taasisi yoyote alisema, “kuna mashirika kadhaa yameonesha nia ya kufanya kazi na mimi, ingawa hakuna mikataba yoyote ambayo imesainiwa mpaka sasa. Kama nilivyodokeza mapema, kuna masuala kadhaa ambayo nahitaji kuyakamilisha kwanza kabla ya kurejea. Serikalini? Sina uhakika, siijapata ‘ofa’ yoyote, lakini nadhani nitakuwepo zaidi katika fani ambayo nimekuwepo ya utangazaji na uandishi wa habari.”

Akieleza anachojivunia miaka 17 BBC alisema, “kikubwa naweza kusema ni uzoefu ambao nimeupata. Kufanya kazi katika ngazi ya kimataifa inakupa fursa ya kufahamu mengi na kutazama katika jicho na mtazamo tofauti.”

“Nafurahi kuwa nimeweza kupata nafasi ya kuwakilisha taifa langu kimataifa na kupeperusha bendera kama balozi wa nchi yangu kwenye fani ya utangazaji na uandishi wa habari. Fursa ya kutangaza katika BBC World News TV na BBC World Service Redio” alisema