Kikwete ang’ara tuzo za TMA, apewa tuzo ya heshima

Rais wa awamu nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete akichangia hoja katika moja ya mikutano aliyohudhuria. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), limempa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete tuzo ya heshima na kutokana na mchango wake katika tasnia ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amepewa tuzo ya heshima na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) usiku wa kuamkia leo Aprili 30, 2023 kutokana na mchango wake katika tasnia ya sanaa.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kikwete amesema amefarijika kuona tasnia ya Sanaa Tanzania inaendelea vizuri kwa kupiga hatua kila siku.
“Napenda kuwashukuru wale wote waliotambua mchango wangu katika tasnia hii ya sanaa natumaini muziki wa Tanzania utaendelea kufika mbali,” amesema.
Kikwete ameyasema hayo katika hafla ya ugawaji wa tuzo za muziki Tanzania (TMA) zilizoandaliwa na Basata katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini hapa.
Akizungumzia mchango wa Rais Kikwete katika tasnia hiyo, Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mbunge wa Muheza mkoani Tanga, Hamis Mwinjuma amesema Kikwete alibadilisha mtazamo wa Serikali kuhusu tasnia hiyo.
“Amefanya mengi katika tasnia hii, alihakikisha wasanii wanapata vyombo vya muziki vya kisasa katika awamu yake,” amesema.
Pia, amesema Kikwete hata baada ya kustaafu amekuwa akishirikiana na wasanii katika hali zote kutokana na mapenzi yake katika tasnia ya sanaa.
“Jakaya amekuwa mwepesi kushirikiana na wasanii kwa kuwa anaamini katika sanaa, amekuwa akiandaa tamasha la kuuaga na kuukaribisha mwaka mpya nyumbani kwake Msoga huku akiwakaribisha wasanii mbalimbali ili kutoa burudani,” amesema Mwinjuma.