Kikwete: Sina undugu na Membe

Muktasari:

  • Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amefafanua ukaribu wake na mwanasiasa Benard Membe, akieleza kuwa hana undugu naye kama ambavyo wengi wanazungumza.


Dar es Salaam. Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amefafanua ukaribu wake na mwanasiasa Benard Membe, akieleza kuwa hana undugu naye kama ambavyo wengi wanazungumza.

Akizungumza leo Oktoba 7, na Clouds Media Group ikiwa ni siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 72, Kikwete amesema huwa anashangaa kusikia kwamba Membe ni ndugu yake.

“Huu undugu huwa siuelewi, Membe sio ndugu yangu yeye Mmwera, mimi mkwere sasa undugu huo vipi? Membe nilikuja kufahamiana naye baadaye sana katika harakati za kazi.

 “Tena wengine wanakwenda mbali unasikia wanasema ni ndugu yake wa damu kabisa sasa sijui kuna ambacho tumefanana kiasi cha kuunganishwa namna hiyo,” amesema.

Kuhusu uteuzi wa kumpata mgombea urais kupitia CCM mwaka 2015 yeye akiwa mwenyekiti amesema alitimiza wajibu wake.

“Walikuwa wagombea 42 mimi kama mwenyekiti nikachagua watano kati yao na kushauri kwa kila mmoja na sifa zake,” amesema Kikwete.