Kila baada ya saa moja watu wanane wanaambukizwa Ukimwi Tanzania

New Content Item (1)
Kila baada ya saa moja watu wanane wanaambukizwa Ukimwi Tanzania

Muktasari:

  • Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Tanzania Dorothy Mwaluko amesema watu wanane wanaambukizwa Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi (VVU) kila saa nchini.

Dodoma. Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji),   Dorothy Mwaluko amesema hali ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini bado ni tishio na kwamba watu wanane kila saa wanaambukizwa virusi hivyo.

Akizungumza leo Ijumaa Novemba 20 2020, kuhusu maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani, yatakayofanyika Desemba Mosi, 20202 mkoani Kilimanjaro, Dorothy amesema takwimu zinaonyesha kuwa takribani watu 72, 000 hupata maambukizi mapya nchini kwa mwaka.

 “Hii ni sawa na wastani wa watu 6, 000 kwa mwezi ama watu 200 kwa siku au watu wanane kwa saa,” amesema.

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa kundi la vijana wa umri wa miaka kati ya 15 hadi 24 linachangia maambukizi mapya kwa asilimia 40 na hivyo kulifanya kundi hilo kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya VVU.

Amesema kutokana na takwimu hizo kila mmoja ana wajibu wa kutekeleza kwa nguvu zote mikakati ya kutokuwa na maambukizi mapya.

Kuhusu maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani, Dorothy amesema maadhimisho hayo yatakayoanza Novemba 25 na kufikia kilele chake Desemba Mosi, 2020 yatafanyika mkoani Kilimanjaro.

Amesema mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya mshikamano wa kimataifa ni 'Tuwajibike kwa pamoja' atakuwa Waziri mkuu,  Kassim Majaliwa.