Kilio cha maji chapungua wilayani Nyang’wale

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kiwilaya katika Kata ya Kharumwa wilayani Geita. Picha na Rehema Matowo.

Muktasari:

  • Mwaka 2020 vijiji vilivyokuwa na huduma ya maji vilikuwa viwili sasa vimeongezeka na  kufikia 31 hali iliyowezesha  wakazi  zaidi ya 150,000 kati ya 225,000 wa wilaya hiyo kupata huduma hiyo.

Geita. Upatikanaji wa huduma ya maji safi na Salama wilayani Nyang’wale mkoani Geita umeongezeka kutoka asilimia 39 mwaka 2020 hadi asilimia 70 mwaka 2024.

Vijiji vilivyokuwa na huduma ya maji navyo vimeongezeka kutoka viwili mwaka 2020 hadi 31 mwaka 2024 na kuwezesha wakazi  zaidi ya 150,000 kati ya 225,000 wa wilaya hiyo kunufaika na huduma hiyo.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 23, 2025 na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) wilayani Nyang’hwale, Moses Mwampunga katika maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kiwilaya katika Kata ya Kharumwa wilayani Geita.

Mwampunga amesema lengo ni kufikia asilimia 85 ya upatikananaji wa maji safi na salama ifikapo 2025.

Amesema ili kufikia lengo hilo, visima 20 vitachimbwa wilayani humo ifikapo mwaka 2025  na kwa kuanzia mwaka huu, Sh250 milioni zitatumika kujenga visima vitano vitakavyowanufaisha wananchi zaidi ya 15,000.

Akizungumza katika maadhimisho hayo ayaliyoambatana na shughuli ya kuliombea Taifa, Mkuu wa wilaya hiyo, Grace Kingalame amesema dhamira ya Serikali ni kumtua mwanamke ndoo kichwani.

“Shughuli za uchotaji wa maji zinafanywa na wanawake na pale yanapokuwa hayapatikani shida anaipata mwanamke na mtoto wa kike; ndio maana Serikali imedhamiria kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa karibu, hii itamwezesha mama kuwa mwangalizi mzuri wa familia.

“Atatumia muda wake kufanya shughuli za kujiongezea kipato badala ya kushinda kutafuta maji,” amesema.

Kingalame amesema wilaya hiyo imepiga hatua ya maendeleo ikiwemo uboreshwaji wa huduma za afya kwa kuwa sasa wanatibiwa wilayani humo baada ya ujenzi wa hospitali ya wilaya na vituo vya afya kukamilika, badala ya kusafiri hadi Wilaya ya Geita kupata huduma hapo awali.

Amesema ili kuwawezesha vijana kujiajiri, Serikali imetoa Sh3 bilioni zitakazotumika kujenga Chuo cha Ufundi (Veta) ambacho kitakuwa mkombozi kwa wale wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne na kushindwa kuendelea na elimu ya juu.

Mbunge wa Nyag’hwale (CCM), Hussein Kasu amesema wakati Taifa likiadhimisha miaka 60 ya Muungano, wilaya hiyo ina shule za msingi 74 na Sekondari 14, ambazo amesema zimewasaidia watoto wengi kupata elimu na kuondoa changamoto ya watu kutokujua kusoma na kuandika.

Mwananchi Digital ilizungumza na Kamde Muasa mkazi wa Kata ya Kharumwa wilayani Nyang’hwale, ambaye amesema katika miaka 60 ya Muungano wanajivunia kuona maendeleo ndani ya wilaya ikiwemo uwepo wa shule ya kidato cha tano na sita n maji, jambo ambalo halikuwahi kuwepo.

“Sisi wanawake wajasiriamali sasa tunapata tunapata maji karibu, ile changamoto ya kutumia maji kwenye madimbwi imeisha. Ulikuwa ukienda kuchota maji unatumia nusu siku ukirudi nyumbani unapigwa, mwanaume anaona ulienda kuzurura lakini sasa ndoa zetu zina amani,” amesema Kamde.