Kilio cha wananchi Busega kuhusu umeme chatua CCM

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohammed (mwenye kilemba cheusi) akisistiza jambo alipokuwa akitoa maelekezo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya chama hicho inayotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Simiyu. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, Dk Yahaya Nawanda. Picha na Samirah Yusuph. 

Muktasari:

Wakazi wa Kijiji cha Milambi Wilaya ya Busega mkoani Simiyu wamewasilisha kilio cha kwa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo wakiiomba iisimamie Serikali kuharakisha utekelezaji wa mradi wa umeme kijini hapo.

Kilio cha wananchi Busega kuhusu nguzo za umeme chatua CCM

Busega. Wakazi wa Kijiji cha Milambi Wilaya ya Busega mkoani Simiyu wamewasilisha kilio cha kwa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo wakiiomba iishinikize Serikali kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa kuwafikishia huduma ya umeme.

Wakizungumza mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Simiyu waliotembelea kijiji hicho leo Jumatano Desemba 4, 2023, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema kasi ya utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme kwenye maeneo yao hauridhishi kutokana na uchache wa nguzo.

"Nguzo zimeishia kwenye baadhi ya maeneo, wengine tumekosa licha ya kuhitaji huduma; tunaiomba CCM iisimamie Serikali iongeze nguzo katika maeneo ya vijijini kuwezesha kila mwenye uwezo kuunganishiwa huduma ya umeme,’’ amesema Ilanga Nyanda, mkazi wa kijiji cha Milambi

Mwananchi huyo amesema tayari ameunganisha mfumo wa umeme katika nyumba yake lakini hajapata huduma hadi sasa huku sababu ikidaiwa kuwa nguzo zimeisha.

Kauli hiyo imeungwa mkono na mkazi mwingine wa kijiji hicho, Helena James akisema kupatikana kwa huduma ya umeme siyo tu itaongeza shughuli za uzalishaji mali kupitia miradi inayohitaji umeme, bali pia itaongeza na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kijijini hapo.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) Wilaya ya Busega, Edward Kweka amesema mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi Sh122.8 milioni unatarajiwa kunufaisha kaya zaidi ya 130 kijijni hapo.

"Tayari kaya 35 zimeunganishiwa huduma na kazi inaendelea kuunganisha kaya nyingine zaidi; nawaomba wananchi waendelee kujitokeza kuomba na kukamilisha taratibu za kuunganishiwa huduma ya umeme,’’ amesema Kweka.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk Yahaya Nawanda ameuagiza uongozi wa Tanesco mkoani humo kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme kukamilisha lengo la kufikisha huduma katika vijiji 430 vya mkoa huo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohammed ameunga mkono agizo hilo la RC Nawanda huku akiahidi kuwa chama hicho katika ngazi zote kuanzia tawi, kata, wilaya hadi mkoa kitafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo kwa lengo la kutimiza ahadi na ilani ya uchaguzi.