Kimeumana, Mbowe ajibiwa kila kona

Wednesday April 14 2021
kimeumana pc
By Waandishi Wetu

Dodoma/Dar. Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kutoa madai mbalimbali yakiwemo ya kufungiwa akaunti zake zote na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na fedha zote kuchukuliwa,  Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba amesema akaunti za wafanyabiashara zilizofungwa zimeanza kufunguliwa.

Mbali na majibu hayo, katika kile ambacho kwa lugha ya mtaani vijana wangesema “kimeumana”, pia Mamlaka ya Mapato za Tanzania imezidi kutoa majibu kuhusu madai hayo huku Spika wa Bunge, Job Ndugai naye kwa upande wake akirusha vijembe dhidi Mbowe.

Mwigulu alitoa kauli hiyo jana jioni bungeni wakati akifanya majumuisho kwa kujibu hoja za wabunge kuhusu Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/22-2025/26). Bunge jana lilipitisha mapango huo.

Bila kutaja jina la Mbowe, Mwigulu alisema mbali na kufunguliwa akaunti pia Serikali imeanza kufuta kesi za uonevu ambazo walifunguliwa watu mbalimbali.

“Mheshimiwa Rais Samia (Samia Suluhu Hassan) alitoa dira kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Mwigulu.

Mwigulu alisema dira aliyoitoa Rais Samia ni Watanzania kushikamana na kuwa atasimama imara kwenye mapato na matumizi ya fedha za Serikali.

Advertisement

“Rais alisema pia atasimama imara kwenye rushwa, alisema kodi za dhuluma sasa basi, CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) asiwe na ulimi wa kigugumizi, miradi mikubwa iendelee, haki kwamba kesi za uonevu zifutwe na watu hawana fedha mifukoni,” alisema Mwigulu.

Waziri wa fedha alisema Rais Samia alitoa dira hiyo kwa Watanzania na baadhi ya mambo yameanza kutekelezwa ikiwamo kufunguliwa akaunti na kesi kufutwa.

Juzi Mbowe na Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) waliozungumza kwa nyakati tofauti kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa ikiwa ni pamoja na yale yanayohusu utawala wa Hayati John Magufuli, utendaji wa TRA na ripoti ya CAG na kusababisha mjadala kukolea bungeni jana.

Kufuatia hoja hizo na hasa ile ya ripoti ya CAG, Spika wa Bunge Job Ndugai amezitaka Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zichambue ripoti ya CAG kuiwakilisha bungeni katika mkutano wa nne badala ya mkutano wa tano, akidai kuwa inapotoshwa.

Juzi, Zitto wakati anazungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alibainisha kuwa hoja zenye mashaka zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) zina thamani ya Sh3.6 trilioni na Dola za Marekani 596 milioni (Sh1.375 trilioni) ambazo kati yake, Sh2.2 trilioni hazikupita mfuko mkuu wa Hazina.

Zitto pia amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya majaji kupitia malalamiko ya watu waliolipishwa fedha kwa mtindo wa kukiri makosa yao na kulipa fedha serikalini kupitia ofisi ya DPP.

Kwa upande wake, Mbowe aliyehutubia Taifa kupitia vyombo mitandao ya jamii, alisema pamoja na mambo mengine, TRA, ilimbambika kodi ya Sh2 bilioni alipokuwa rumande gerezani mwaka 2018 na kama hiyo haitoshi, mamlaka hiyo ilizifunga akaunti zake na za kampuni zake ikiwamo ya binafsi aliyokuwa anapokelea mshahara wa ubunge.

Mbali na TRA, Mbowe pia alichambua utendaji wa Bunge la Jamhuri ya Muungano akidai kuwa limegeuka kuwa chombo cha propaganda cha Serikali.


Majibu ya Ndugai

Akizungumza jana bungeni jijini Dodoma Ndugai alisema kuna watu wanaopotosha ripoti ya CAG na kuzitaka kamati za PAC na LAAC kuzichambua na kuwziwasilisha bungeni mapema iwezekanvyo.

Amesema si watu wengi wenye uelewa wa kuchambua taarifa za kihasibu na kunaweza kukawa na ujenzi wa kituo cha afya wa Sh 500 milioni lakini Sh499 milioni zimetumika vizuri kabisa.

Hata hivyo, alisema kati ya fedha hizo Sh1 milioni ikikosa kiambatanisho fulani ni kawaida wakaguzi wanahoji fungu zima la Sh500 milioni.

Alisema kwa hiyo unaposoma mtaani unaona Sh500 milioni zimeibwa lakini kumbe pale ni Sh1 milioni ndio hazina risiti.

Alisema kamati hizo zitaanza mapema kuchambua ripoti hizo ili waangalie ratiba yao na kuwaelimisha watu kuhusiana na ripoti ya CAG ambayo ni taarifa nzuri lakini baadhi ya watu wanabeba na kupotosha tu.

Huku akimtaja Mbowe, Ndugai alisisiza kuwepo wapotoshaji wa ripoti hiyo.

“Watu wanabeba tu mabilioni yameibiwa sasa huyo rafiki yangu Freeman Mbowe alikuwa Ulaya huko sasa katumwa na watu wake huko anapotosha mambo,” alisema Ndugai.


TRA wafuatilia

Akizungumzia madai ya Mbowe kubambikwa kodi baada ya kuulizwa kwa simu jana, Kamishna msaidizi wa TRA, Msafiri Mbibo alisema watasikiliza hotuba ya Mbowe ili kujua anachokilalamikia.

“Mtu anaweza kutoa maoni yake hadharani, japo siwezi kusema kuwa Mbowe amefanya hivyo kwa sababu sijaisikiliza hotuba yake. Kwa hiyo, ngoja kwanza nisikilize ili nijue kama suala lenyewe linaweza kusemwa hadharani,” alisema.

Alisema sheria inawazuia kutoa taarifa za walipa kodi hadharani isipokuwa kwa mamlaka zilizoruhusiwa kisheria.

Kuhusu barua iliyodaiwa kutumwa na TRA hivi karibuni kwa Mbowe, Mbibo alisema mamlaka hiyo inazo ofisi nchi nzima na kwamba inachukua muda kwa barua hizo kufika makao makuu hivyo inakuwa vigumu kupata ushahidi wa madai hayo.


Mbunge CCM acharukia

Wakati majibu hayo yakitolewa, bungeni nako hoja kama hizo ziliibuka ambapo Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Judith Kapinga alisema tafsiri ya Sheria ya uhujumu uchumi imesababisha watu kupokonywa mali zao na kuadhibiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha ambayo ni vigumu kuyathibitisha.

Judith alisema hayo jana wakati akichangia Mpango wa tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano (2021/22 hadi 2025/26).

Mbunge huyo alieleza kuwa Sheria ya uhujumu uchumi ililetwa kutokana na shinikizo la mataifa ya nje.

Imeandikwa na Noor Shija, Sharon Sauwa na Elias Msuya.


Advertisement