Kina Mbatia wamlalamikia msajili, yeye awajibu

Kaimu Katibu Mkuu, Anthony Komu

Muktasari:

  • Wakati Chama cha NCCR-Mageuzi upande wa Mwenyekiti, James Mbatia wakiilalamikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kubariki kufanyika kwa mkutano mkuu, Ofisi hiyo imesema ratiba ya mkutano huo ilipangwa kabla ya kesi kwenda mahakamani.


  

Dar es Salaam. Wakati Chama cha NCCR-Mageuzi upande wa Mwenyekiti, James Mbatia wakiilalamikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kubariki kufanyika kwa mkutano mkuu, Ofisi hiyo imesema ratiba ya mkutano huo ilipangwa kabla ya kesi kwenda mahakamani.

Septemba 7, 2022, Kambi ya Mbatia ilifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ikipinga uhalali wa kambi ya kina Joseph Selasini na mamlaka ya kuitisha na kuendesha vikao vya chama na ikafungua maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa kujishughulisha na shughuli za chama.

Hata hivyo, Mahakama hiyo ilitoa amri ya zuio la muda kuhusu vikao vilivyoitishwa na kambi ya Selasini katika mkutano wake na vyombo vya habari hadi maombi hayo ya zuio yatakaposikilizwa pande zote.

Uamuzio huo ulitolewa na Jaji Edwin Kakolaki anayesikiliza shauri hilo baada ya kukubaliana na hoja za wakili wa wadai, Juma Nassoro kusikilizwa kwa dharura, wakati maombi hayo yalipotajwa mahakamani hapo.

Akizungumza na wanahabari leo Ijumaa Septemba 23, 2022 Kaimu Katibu Mkuu, Anthony Komu amesema pamoja na zuio la Mahakama wamepata taarifa ya watu walioko Dodoma wakiandaa mkutano wa Halmashauri Kuu pamoja na mkutano mkuu.

"Tunavyoongea kuna maandalizi ya mkutano katika ukumbi wa St Gasper Dodoma na waratibu ni hawa waliokatazwa na Mahakama," amesema Komu.

Amesema hata alipomtafuta Msajili wa Vyama Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alimwambia taarifa na ratiba ya mkutano huo ilimfikia kabla ya kesi kufunguliwa mahakamani.

"Kutokana na presha ya wanachama wengine hawezidi kuvumilia kuona chama chao kinavurugwa, lolote linaweza kutokea, nimeongea na msajili anasema mkutano huo aliuruhusu kabla ya kesi kwenda mahakamani," amesema.

Mwananchi Digital ilipomtafuta Jaji Mutungi kuzungumzia suala hilo amekiri kuwasiliana na Komu na kumshauri kwenda mahakamani kwani ratiba ya mkutano ilimfikia kabla ya kufungua kesi.

Alisema mtu hawezi kuwa mgonjwa na wakati huohuo akaenda kwa mganga kwakuwa walikuwa na mkutano na pande zote mbili lakini kilichojiri ni wao kwenda mahakamani.

"Niliwaambia kwa kuwa wamechagua kwenda mahakamani mimi nimefungwa mikono sasa wanarudi kwangu kufanya nini, walipokuja nimewashauri warudi kulekule kwa kuwa siwezi kuliongelea," amesema Jaji Mutungi.

Hata hivyo, Mwananchi liliitafuta kambi inayoungwa mkono na Selasini bila mafanikio baadabya simu zao kuita bila kupokelewa.

Mei 21, 2022, Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi iliitisha mkutano katika ukumbi wa Jeshi la Wokovu Kurasini miongoni mwa agenda zilizojadiliwa ni pamoja na kumsimamisha mwenyekiti wa cha hicho, James Mbati kujihusisha na shughuli za chama, kutokana na sababu mabalimbali ikiwemo kuchochea migogoro.