Kina Mdee wamekwama aisee!

Muktasari:

  • Jumla ya wajumbe 423 walishiriki kikao cha Baraza Kuu, kati yao 413 sawa na asilimia 97.6 walikubaliana na uamuzi wa kamati ya kuu ya Chadema ya kuwavua uanachama, wakati watano sawa na asilimia 1.2 hawakukubaliana na uamuzi huo.


Dar es Salaam. Unaweza kusema wamekwama na sasa hatima ya ubunge wa waliokuwa wanachama wa Chadema, Halima Mdee na wenzake 18 imebaki mikononi mwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Hatua hiyo ilifikiwa jana baada ya maombi yao ya kutaka kufungua shauri Mahakama Kuu kupinga kuvuliwa kwao uanachama na ubunge kutupwa.

Kufuatia maombi hayo, Chadema iliwawekea pingamizi ikiiomba mahakama isiyasikilize maombi hayo kwa madai kuwa yalikuwa na kasoro za kisheria, huku mawakili wao na wale wa Serikali wakipinga hoja sita zilizoibuliwa na chama hicho.

Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa jana na Jaji John Mgetta, iliyatupilia mbali maombi hayo baada ya kukubaliana na hoja moja kati ya sita, kuwa waombaji hao walikosea katika kuandika jina la mjibu maombi wa kwanza, pia ikatupilia mbali ombi la kuwekea zuio ubunge wao.

Katika shauri hilo, Mdee na wenzake walimtaja mjibu maombi wa kwanza kwa jina la Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa Kiingereza, (The Board of Trustees, Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema).

Hata hivyo, Chadema kupitia jopo la mawakili wake ilipinga ikidai kuwa waombaji wameishtaki taasisi isiyokuwepo.

Wakili Peter Kibatala wa Chadema alifafanua kuwa kisheria jina halisi ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema iliyosajiliwa kama The Registered Trustees, Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema).

Jaji Mgetta katika uamuzi wake alikubaliana na hoja za wakili Kibatala akisema ni matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 21(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kuwa chama cha Siasa kikipata usajili sharti kiteue bodi na bodi hiyo lazima isajiliwe chini ya Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini.

Alisema baada ya kusajiliwa ni takwa la kisheria kuwa jina lake lazima itajwe kwa kuanza na maneno “The Registered ...)

Jaji Mgetta alikataa hoja za jopo la mawakili wa kina Mdee kuwa katika marekebisho ya mwaka 2019 ya Sheria ya Vyama vya Siasa iliondoa takwa la lazima la matumizi ya neno “The Registered” na kwamba kwa sasa inatamkwa tu kuwa The Board of Trustee”.

Jaji Mgetta alikubaliana na hoja za Kibatala kuwa marekebisho ya mwaka 2019 ya sheria hiyo hayakuathiri wala kuondoa matumizi ya maneno “The Registered” baada ya bodi za wadhamini kusajiliwa.

Kwa sababu hizo, Jaji Mgetta alisema hiyo ni dosari kubwa na tiba yake ni kuyatupilia mbali maombi hayo huku akirejea uamuzi na msimamo wa Mahakama ya Rufani katika hoja kama hiyo ambayo katika moja ya hukumu zake imesisitiza matumizi ya maneno “The Registered.”

Sambamba na maombi hayo ya kibali, pia Jaji Mgetta alitupilia mbali maombi ya kina Mdee ya zuio la muda dhidi ya Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua hatua yoyote kuhusu nafasi zao kusubiri kuamuliwa kwa maombi hayo ya kibali.

“Kwa kuwa maombi haya ya zuio yanatokana na maombi ya msingi ya kibali na kwa kuwa maombi ya kibali yameondolewa, basi maombi haya ya zuio nayo yanakosa miguu ya kusimamia mahakamani. “Hivyo nayo yanatupiliwa mbali,” alisema Jaji Mgetta.

Kwa uamuzi huo, ubunge wa Mdee na wenzake umebaki unaelea kuanzia sasa, huku hatima yao ikibakia mikononi mwa Spika ambaye anapaswa kuiandikia NEC kuijulisha kuwa nafasi zao ziko wazi.

Tayari Chadema walishamwandikia Spika kumjulisha kuwa Mdee na wenzake wamevuliwa uanachama na Spika akajibu kuwa hawezi kuchukua hatua hiyo kwa kuwa alikuwa amepata taarifa kuwa kina Mdee wamefungua maombi mahakamani kwa lengo la kupinga uamuzi wa kuvuliwa uanachama.

Hivyo, Spika sasa yuko huru kuchukua hatua zaidi.

Jaji Mgetta katika uamuzi wake alikataa hoja nyingine za Chadema huku akikubali baadhi ya kasoro, lakini akasema zilikuwa hazimalizi shauri badala yake akatoa maelekezo ya kuzifanyia marekebisho.

Wakati hali ikiwa hivyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa kina Mdee, Aliko Mwamanenge aliliambia Mwananchi kuwa vita haijafika mwisho kwa kuwa wanakwenda kufanya marekebisho ya kasoro zilizojitokeza na kurudi tena mahakamani.

Wakati kina Mdee wakiwa na maoni hayo, Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika alisema kuwa kwa kuwa uamuzi umeshatoka, anaamini Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataupeleka kwa Spika wa Bunge.


Wenyewe walikuwa bungeni

Wakati uamuzi dhidi yao unasomwa baadhi ya wabunge hao walikuwa bungeni wakiendelea katika mjadala wa bajeti.

Walioonekana jana ni pamoja na Sophia Mwakagenda, Grace Tendega, Hawa Mwaifunga, Cecilia Pareso na Conchester Rwamlaza na Anatropia Theonest.
Wengine ni Tunza Malapo, Asya Mohamed, Felista Njau na Kunti Majala huku Halima Mdee na Esther Bulaya wakiwa hawajahudhuria kikao cha jioni.

Si Spika Tulia wala Katibu wa Bunge Nenelwa Mwihambi aliyepatikana jana kueleza nini kinafuata baada ya hapo.

Katibu mukhtasi wa katibu wa Bunge alisema bosi wake alikuwa katika kikao.


Safari ya siku 605 bungeni

Katikati ya sintofahamu ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 na Chadema ikisema haingepokea mazao yote ya uchaguzi huo, Mdee na wenzake waliibuka ghafla bungeni na kuapishwa na aliyekuwa Spika Job Ndugai nje ya ukumbi wa Bunge kama ilivyozoeleka kwa wabunge Novemba 24, 2020.

Kufuatia hayo, Novemba 27 mwaka 2020, Kamati Kuu ya Chadema iliwavua uanachama wabunge hao baada ya kubainika kukiuka katiba na kanuni za Chadema kwa uamuzi wao wa kwenda kuapishwa bila chama hicho kuwapitisha.

Hata baada ya Chadema kulitaarifu Bunge kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu, Spika hakuutambua.

“Kwa wale waliokuwa na wasiwasi wale wabunge 19 kuna hili kuna lile, niwahakikishie kuwa wale ni wabunge kamili wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania. Nawaomba Watanzania wote tupige vita na tukatae ukandamizaji dhidi ya wanawake katika jamii yetu kwa kisingizio chochote,” alisema.

Baada ya uamuzi huo, Mdee na wenzake walikata rufaa katika Baraza Kuu la Uongozi wakipinga uamuzi wa kamati kuu ya kuwavua uanachama hadi Mei 11 2022, Baraza hilo lilipokubaliana uamuzi uliotolewa na kamati ya chama hicho, na wao kuchukua mkondo wa mahakama.

Jumla ya wajumbe 423 walishiriki kikoa cha Baraza Kuu, kati yao 413 sawa na asilimia 97.6 walikubaliana na uamuzi wa kamati ya kuu ya Chadema ya kuwavua uanachama, wakati watano sawa na asilimia 1.2 hawakukubaliana na uamuzi huo. Ambao hawakufungamana na upande wowote ni watano, sawa na asiliamia 1.2.

Imeandikwa na James Magai, Bakari Kiango, Fortune Francis na Sharon Sauwa.