Kinana awapa ujumbe viongozi wa Serikali

Muktasari:
- Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana ameanza ziara mkoani Rukwa akitokea Katavi na kesho Jumatano atakuwa Songwe kisha Mbeya.
Rukwa. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kuhakikisha wanarahisisha ufanyaji wa shughuli za wananchi kwa kuwaondolea vikwazo kwa kuwa sekta binafsi inaanza na wao.
Kinana ameyasema hayo leo Jumanne, Julai 26, 2022 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Nkasi Kaskazini eneo la Lyazumbi wakati wa mapokezi ya kuanza ziara Mkoa wa Rukwa akitokea Katavi.
"Serikali inafanya jitihada za kuimarisha na kuboresha mazingira ya sekta binafsi nchini ili ifanye vizuri, sasa sekta binafsi inaanza na wananchi wa kawaida,” amesema Kinana na kuongeza:
“Tuwaondolee kero wananchi wetu na tuwarahisishie kufanya shughuli zao iwe ni wakulima, wafugaji, bodaboda, wamachinga au wafanyabishara."
Akimkaribisha mkoani Rukwa, Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Rainer Lukalah amemueleza Kinana hali ya siasa katika mkoa huo ni shwari na wanaridhishwa na kasi ya maendeleo inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
Kinana ameingia mkoani Rukwa ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya uimarishaji wa chama na ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM akiwa ameambatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka.