Kindamba: TTCL pesa inazidi kukua, tuko vizuri

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba

Muktasari:

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba amesema Huduma za TTCL pesa zinazidi kukua huku akiwataka watu kuondoa hofu juu ya gawio wanalolitoa kwa Serikali

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba amesema huduma ya TTCL pesa imezidi kukua huku wateja wakiwa wamefikia 400,000, mawakala 11,000 huku mtaji unaozunguka sokoni ukiwa zaidi ya Sh4 bilioni.

Ameyasema hayo leo Jumanne ya Mei 21, 2019 katika hafla ya utoaji wa gawio kwa Serikali iliyoenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya huduma ya video conference.

Kindamba amesema huduma hiyo imeongeza usalama wa fedha na kutoa huduma za gharama nafuu kwa Watanzania jambo ambalo linachangia kusukuma azma ya kwenda Tanzania ya viwanda.

“Wateja waliopo sasa bado wanaendelea kuongezeka hivyo ni matumaini yetu tutazidi kukua zaidi.”

“Kumekuwa na maswali mengi juu ya namna gani taasisi iliyokuwa hoi kiuchumi na kupotea katika ramani kutoa gawio lakini niseme ukweli, TTCL mahesabu haya hayajatengenezwa na mzee Nundu, wala Waziri Kindamba bali na wahasibu wabobezi ndani ya TTCL.” Amesema Kindamba

Amesema baada ya mahesabu hayo kutengenezwa hukaguliwa na mkaguzi wa ndani na baadaye hupitiwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambaye ndiye huthibitisha hesabu hizo kama kitabu hicho ni kisafi au kichafu ikiwa na majibu ya faida au hasara.

“Baada ya kupata kauli ya CAG ndiyo tulipeleka maombi katika bodi ya kutoa gawio kwa Serikali, gawio (Sh2.1 bilioni) ambalo utalipokea hivi punde kwa sababu kufanya hivyo ni matakwa ya kisheria na miongozo ambayo umekuwa ukiitoa mara kwa mara.” Amesema Kindamba.