Kitambulisho cha uraia kutumika uhakiki wamiliki wa ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kigoto kata ya Kirumba mkoani Mwanza kabla ya kiwakabidhi ankara kwa ajili ya kulipia hati za viwanja vyao vilivyomaliza kupimwa. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Ili kukomesha utapeli na umiliki hewa wa ardhi nchini, Julai  mosi, 2021 Serikali itaanza upya uhakiki wa wamiliki wa ardhi nchini kwa kutumia kitambulisho cha uraia ambacho taarifa za wahusika zitakuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Mwanza. Ili kukomesha utapeli na umiliki hewa wa ardhi nchini, Julai  mosi, 2021 Serikali itaanza upya uhakiki wa wamiliki wa ardhi nchini kwa kutumia kitambulisho cha uraia ambacho taarifa za wahusika zitakuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Akizungumza leo Alhamisi Februari 4, 2021 mkoani hapa  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  William Lukuvi amesema kuna migogoro na malalamiko ya wananchi kunyang'anywa ardhi na watu wasiotambulika serikalini kama wamiliki halali wa ardhi hizo.

Amebainisha kutokana na mfumo wa sasa wa utoaji hati unaotumia cheti cha kuzaliwa kumilikisha ardhi kwa wananchi, baadhi wanatumia majina bandia kumiliki ardhi na kukaa muda mrefu bila kulipa kodi ya pango.

"Pia kupitia mfumo wa kutumia cheti cha kuzaliwa kimesababisha watu wasiyo Watanzania kumiliki ardhi nchini jambo ambalo ni hatari hata kwa usalama wa nchi huku wazawa wakiwa hawana umiliki wa maeneo yao.”

"Kwenye uhakiki huu tutakuwa tunafuatilia kila kitu ikiwemo namba ya simu na mmiliki wa eneo anayekabidhiwa hati lazima atoe taarifa zake za benki ili iwe rahisi kumlipisha kodi ya adhi," amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuwaonya baadhi ya maafisa ardhi wanaotumiwa na wenye fedha kuwalaghai wananchi na kuuza maeneo yao kinyume na utaratibu.