Kituo cha umeme Ifakara kumaliza kero ya wananchi

Muktasari:

  • Wananchi Wilaya tatu Morogoro sasa wanatarajia kuondokana na adha ya kukatika kwa umeme baada ya kuwashwa kwa kituo cha Ifakara.

Morogoro. Tatizo la katikakatika kwa Umeme lililokuwa likizikabili wilaya za  Kilombero, Ulanga na Malinyi na kuwatesa wawekezaji na wananchi kushindwa kufanya maendeleo,  limepata ufumbuzi, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa  kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara na sasa kuwashwa.

Akizungumza Desemba 4,2023 wakati wa tukio la kuwasha  umeme katika kituo cha kupoza umeme Cha Ifakara (Ifakara Substation) kilichojengwa katika  kata ya Kibaoni Halmashauri ya Mji wa Ifakra, Meneja Msimamiza wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) mhandisi Romanus Rwena, amesema kituo hicho kimejengwa kwa ufadhili wa Umoja wa wa Ulaya (EU)kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya Sh25 bilioni.

Rwena amesema lengo la kujengwa kwa kituo hicho cha umeme Ifakara ni kutokana na awali Wilaya tatu za Kilombero, Malinyi na Ulanga zilikuwa zikipata umeme kutoka kwenye msongo wa 33kv kutoka Kidatu ambao uwezo wake ulikuwa mdogo ukilinganisha na mahitaji.


”Uwezo wa laini hii ni mdogo pengine zaidi unaweza kubeba megawati saba mpaka nane,ikizidi umeme unakatika na kwa mahitaji ya wilaya hizo ni zaidi ya megawati nane”amesema Rwena.

Umoja wa nchi za Ulaya (EU) wametoa kiasi cha Sh18 bilioni huku Serikali ya Tanzania ikichangia Sh7 bilioni.

"Hapo awali kulikuwa kukitokea hitilafu katika moja ya hizo wilaya hulazimika kukosa umeme jambo ambalo kwa sasa halitokuwepo kwani kukitokea tatizo maeneo mengine yatabaki kuwa na umeme,"amesema.

Naye Meneja Miradi kutoka Umoja wa Ulaya anayesimamia upande wa Nishati ya Umeme Mhandisi Francis Songela, amesema EU, wamekuwa washirika wakubwa na Serikali katika sekta mbalimbali ukiwemo mradi huo wa kupoza umeme na kusambaza wilaya za Kilombero,Malinyi na Ulanga  ambao utasaidia kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika.

”Ninyi mtakuwa ni mashahidi mtu kuwekeza kwenye viwanda vya kati na vikubwa changamoto ya umeme ilikuwa ni kubwa lakini kwa sasa itabaki kuwa historia,”amesema Songela. 

Kaimu mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa umeme Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu amesema umeme waliokuwa wakiutumia wa megawati sita hadi saba, ulikuwa ukikwamisha shughuli za uwekezaji katika wilaya hizo.

"Serikali imeona haja kujengwa kituo hicho ili kuongeza nguvu ya umeme unaopatikana ili wawekezaji waweze kuwekeza kwa wingi na wilaya hizi ziendelee kimaendeleo," amesema.