Korea Kusini watoa msaada wa vifaa vya zaidi ya Sh1 bilioni kwa Tantrade

Mkugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis (katikati) akiwa na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania, Kim Sun Pyo (wa pili kushoto) na Mkurugenzi na Kamishna wa Biashara kutoka KOTRA, Wohn Young. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi TanTrade Mary Fedilis pamoja na Naibu balozi wa Korea nchini Tanzania Seungyun Lee wakiwa katika picha ya pamoja baada ya hafla ya makabidhiano.
Dar es Salaam. Serikali ya Korea Kusini imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kwa ajili ya kuboresha Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba.
Vifaa hivyo vilivyotolewa na nchi hiyo kupitia Taasisi yake ya Biashara Korea Kusini (KOTRA) ni vibanda vya kisasa 500, kompyuta za mikononi 10, kompyuta za mezani 30, skana 30 pamoja na genereta lenye ukubwa wa kilovoti 60.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne Machi 19, 2024 mara baada ya kupokea msaada huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Latifa Khamis amesema vibanda hivyo vilivyotolewa vitaongeza ufanisi, mapato kwa nchi pamoja na idadi ya wadau mbalimbali kutoka mikoani kushiriki katika maonesho hayo ya Kimataifa ya Sabasaba.
“Msaada huu hauna masharti yeyote, hata hivyo wadau wengi walikuwa wanataka kushiriki maonesho lakini nafasi zilikuwa hakuna, lakini kupitia kuwepo kwa vibanda hivi tutaongeza ufanisi na idadi ya washiriki hatimaye kupata fedha zitakazoendelea kukuza uchumi wa nchi.
“Wadau wetu tunapenda kuwakaribisha kuja kwa wingi kwani uwezo wetu umeongezeka kutokana na kuwepo kwa vifaa hivi hivyo kwa mwaka huu maonesho yataimarika na kuwa yenye mvuto mkubwa,” amesema.
Aidha amesema yapo mazungumzo ambayo wanayafanya baina yao na Kotra ambayo yanalenga kuboresha utendaji kazi ili kuweza kuwavutia zaidi wafanyabiashara.
Naye Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Kim Sun Pyo amesema ni muhimu kuendelea kuwahimiza watanzania kusafirisha zaidi bidhaa kwenda kuuza Korea na wao watawahamasisha wananchi wao kununua bidhaa hizo.
“Tunahitaji kuhamasisha uhusiano wa pande zote mbili, tunao wajibu wa kuwahimiza Watanzania kusafirisha bidhaa na kuzipeleka Korea kwa ajili ya kuziuza na tuwahamasishe wananchi wa Korea kununua bidhaa zinazotoka Tanzania,” amesema Balozi Pyo.