Kortini kwa tuhuma za kujipatia Sh12.5milioni kwa udanganyifu

Muktasari:
- Mtafya anadaiwa kujipatia fedha hizo, mali ya Priscillah Mollel ili amnunulie nguzo za umeme, lakini hakufanya hivyo.
Dar es Salaam. Mkazi wa Iringa, Anania Mtafya, amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, akikabiliwa na shtaka la kujipatia Sh12.5 milioni kwa udanganyifu.
Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hiyo, mali ya Priscillah Mollel ili amnunulie nguzo za umeme huko Iringa, lakini hakufanya hivyo na badala yake alitoweka na fedha hizo.
Mtafya amefikishwa mahakamani hapo leo, Januari 21, 2025 na kusomewa shtaka na karani wa mahakama hiyo, Aurelia Bahati mbele ya Hakimu Gladness Njau.
Akimsomea shtaka lake, karani Bahati amedai mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 10, 2024, saa 9:34 alasiri eneo la Samora, kata ya Kivukoni, Wilaya ya Ilala.
Inadaiwa siku hiyo, mshtakiwa alijipatia kwa udanganyifu Sh12.5 milioni, mali ya Priscillah Mollel ili amnunulie nguzo za umeme huko Iringa, lakini hakufanya hivyo na matokeo yake alitokomea na fedha hizo.
Mshtakiwa, baada ya kusomewa shtaka lake, alikana kutenda kosa hilo na kuomba dhamana.
Hakimu Njau alitoa masharti ya dhamana ambayo alimtaka mshtakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh500,000.
Mshtakiwa amepata dhamana na kesi imeahirishwa hadi Februari 27, 2025 kwa ajili ya kusikilizwa.