Kufa kwa biashara, uhamishaji wa matumizi, kwachefua wabunge
Muktasari:
- Akisoma taarifa ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Raphael Chegeni alisema taasisi tatu ikiwamo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) yanajiendesha kwa hasara.
Dodoma. Serikali kuchelewa kulipa fedha za mifuko ya hifadhi na mashirika ya umma, kuzorota kwa kwa biashara katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam na fedha za miradi ya maendeleo kwenda kwa kiwango kidogo katika maeneo mbalimbali pamoja na ongezeko la mafungu ya fedha kwa baadhi ya taasisi za umma ni miongoni mwa mambo yaliyozua mjadala mkali bungeni jana.
Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde alikwenda mbali akisema mtu wa kwanza kupelekwa jela baada ya Rais John Magufuli kuondoka madarakani atakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dotto James.
Akichangia mjadala wa taarifa za kamati za Bunge za Bajeti na Uwekezaji wa Mitaji wa Umma (PIC), Silinde alisema katika matumizi, Hazina walitakiwa kupewa Sh144 bilioni ndani ya nusu mwaka, lakini hadi sasa wamepewa Sh414 bilioni (sawa na asilimia 286).
Alitoa mfano mwingine wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwamba ilitakiwa kupewa Sh1.2 bilioni kwa nusu mwaka wa fedha, lakini imepewa Sh8.3bilioni sawa na asilimia 676.
Mbunge huyo alisema, “Siku ambayo Rais Magufuli atamaliza utawala wake, wa kwanza kwenda jela atakuwa katibu mkuu Hazina na msimdanganye atakwenda, kwa sababu Rais akishaondoka madarakani hana power (nguvu) tena ya kumlinda mtu,” alisema Silinde.
Alisema anashangaa ni kwa nini kuna uhamishaji wa matumizi ya fedha bila Bunge kupata taarifa.
“Mwakani, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), badala ya Sh1.5 trilioni itakuja Sh8 trilioni, kwa nini Bunge haliletewi kitabu kinachoonyesha kuwa Serikali imehamisha fedha?” alihoji mbunge.
“Ni kwa nini Serikali haijapeleka pia fedha Sh60 milioni zilizopitishwa katika robo ya mwaka jana kwa ajili ya majaribio ya Sh50 milioni za kila kijiji.”
Mbunge wa Nkenge (CCM), Dk Diodorus Kamala alisema kiasi cha fedha asilimia 202 zilizopelekwa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinatosha, sasa zipelekwe sekta nyingine.
“Ukiangalia taarifa ya fedha za maendeleo zinavyokwenda, ukiisoma vizuri na ukawa mkweli, utoaji wa fedha za maendeleo hautolewi sawasawa.
“Ukiangalia Wizara ya Mambo ya Ndani imepata asilimia 202 ya bajeti ya miradi ya maendeleo, ni jambo jema lakini unapoangalia sekta nyingine ambazo ni muhimu fedha hazijaenda kama inavyotakiwa,” alisema.
Wabunge walionya pia tabia inayojengeka kwa baadhi ya viongozi wa Serikali ya kuwaona wafanyabiashara ni wezi na wabaya, wameitaka kubadilika.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba alisema kwa bahati mbaya, maneno hayo ya wafanyabiashara kuwa ni ‘wezi na wabaya’ yanatamkwa na baadhi ya viongozi wakubwa serikalini.
“Leo Kariakoo imekufa. Mimi nitasema sababu chache zilizosababisha hali hiyo. Wafanyabiashara wadogo wanaenda China wanaleta glasi ya Sh1,000 na Sh10,000, lakini akija mtu wa kodi anasema glasi zote ni za Sh10,000, wanakadiriwa kodi kubwa, kwa mtindo huu mfanyabiashara ataendelea kweli?” alisema.
Mbunge huyo alisema kutokana na hali hiyo, wengi wao wanaamua kuuza bidhaa za bei kubwa ambazo wengi hushindwa kuzimudu.
Pia, alihoji kitendo cha mamlaka zisizo husika na utozaji wa kodi kuwanyanyasa wafanyabiashara huku akitolea mfano wa Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Shughuli ya kodi inasomewa, watu wanakaa darasani wanapata degree ya kodi. Tuwaombe polisi na vyombo vyote vya ulinzi na usalama wafanye kazi walizosomea waachane na hii ya kodi,” alisema.
Hussein Bashe (Nzega Mjini- CCM) alisema Dola moja ya Marekani hivi sasa inauzwa hadi Sh2,400 na hiyo inamaana kwamba gharama ya kuagiza bidhaa nje inazidi kupaa na kuifanya shilingi kuwa dhaifu.
Alisema hali hiyo inasababisha bei za mazao nchini na bidhaa zingine kuendelea kuporomoka, hali ambayo ni hatari kwa uchumi wa nchi huku akisema hali hiyo imekuwapo tangu mwaka 2016.
“Ukienda katika takwimu za TRA, ukuaji wa makusanyo kwa kipindi cha miezi sita ulikuwa ni asilimia 18.5 tu, lakini umekuwa kwa asilimia mbili. Ukienda katika mabenki mikopo inayokua ni ya mtu mmojammoja kama ya wafanyakazi ambayo inaishia kwenye kujikimu na si uzalishaji. Mipango yote ya Wizara ya Fedha ni mipango ya kiutawala si ya kukuza biashara,” alisema Bashe na kushauri kukaa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kuja na mkaati wa kukuza biashara.
Mashirika matatu yajiendesha kihasara
Akisoma taarifa ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Raphael Chegeni alisema taasisi tatu ikiwamo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) yanajiendesha kwa hasara.
Dk Chegeni alisema kwa miaka mitatu mfululizo tangu 2015 hadi 2016/17, matumizi ya TPDC yanaongezeka ikilinganishwa na mapato yaliyokusanywa hali inayolifanya liingie hasara.
Alisema mwaka 2015/16, TPDC imeingia hasara ya Sh374.62 bilioni na mwaka 2016/17, Sh157.18 bilioni.
“Kupatikana kwa hasara ya muda mrefu kwa baadhi ya taasisi na mashirika ya umma, kunachangiwa na uendeshaji wa kusuasua kwa taasisi hizo hususan katika miradi ya maendeleo isiyoendesheka,” alisema.