Kuondoka na kurudi kwa kundi la Taliban

Kuondoka na kurudi kwa kundi laTaliban

Muktasari:

  • Habari zinazojulikana zaidi kwa sasa duniani ni zile za kundi la Taliban kutwaa madaraka nchini Afghanistan, wiki mbili kabla Serikali ya Marekani haijakamilisha taratibu za kuyaondoa majeshi yake nchini Afghanistan, baada ya kukaa huko kwa miongo miwili.

  

Habari zinazojulikana zaidi kwa sasa duniani ni zile za kundi la Taliban kutwaa madaraka nchini Afghanistan, wiki mbili kabla Serikali ya Marekani haijakamilisha taratibu za kuyaondoa majeshi yake nchini Afghanistan, baada ya kukaa huko kwa miongo miwili.

Taliban walivamia nchi nzima, wakiteka miji yote mikubwa katika muda wa siku chache na kuvishinda vikosi vya usalama vya Afghanistan, vilivyopewa mafunzo na jeshi la Marekani na washirika wake pamoja na kupatiwa zana kali za kivita. Sasa wameanza kufanya doria ya nyumba kwa nyumba.

Taliban ambayo sasa imeidhibiti nchi hiyo, iliondolewa madarakani mwaka 2001, wakati Marekani walipoivamia nchi hiyo wakidai kuwasaka magaidi waliofichwa na utawala huo. Miaka 20 baadaye wameirejesha tena Afghanistan kwenye himaya yao.

Ingawa hakuna takwimu kamili za nguvu za Taliban kijeshi, inakadiriwa kuwa kikundi hicho kina karibu wapiganaji 150,000, ikiwa ni karibu asilimia 50 ya wanajeshi wote wa jeshi la Afghanistan.

Pamoja na kwamba wapiganaji wa Taliban wanatawaliwa na ukoo wa Pashtun, kuna wapiganaji wengine kutoka makabila mengine na pia nchi nyingine za Kiislamu.

Kihistoria, Pashtun ni kundi au ukoo unaotawala nchini Afghanistan na wamepigana kwa nguvu kutunza ukuu wao katika historia ya Afghanistan.

Mwandishi Raghav Sharma katika kitabu chake, ‘Nation, Ethnicity and the Conflict in Afghanistan: Political Islam and the Rise of Ethno-Politics 1992-1996’, ameandika kuwa kabla ya mwaka 1978 Pashtuns walikuwa karibu asilimia 40 ya idadi ya watu wote wa Afghanistan.

Baada ya uvamizi wa Urusi ulioanza Jumatatu ya Desemba 24, 1979, asilimia 85 ya zaidi ya wakimbizi 3,000,000 wa Afghanistan waliokimbilia Pakistan walikuwa Wapashtun ambao siku zote wamejiona kuwa jukumu lao kubwa nchini Afghanistan ni kushiriki siasa za nchi hiyo “kwa gharama zozote”, na nafasi yao kubwa imekuwa kichocheo kikubwa katika mizozo ya Afghanistan.

Taliban ambayo muundo wake ni tofauti na vikundi vingine vya wapiganaji na yenye uongozi wa kimfumo, inaongozwa zaidi na makamanda ambao walipigana vita dhidi ya Urusi katika miaka ya 1990.

Makamanda wao wana uzoefu wa jinsi ya kupambana na wanajua njia rahisi za kushambulia miji muhimu ya Afghanistan. Inasemekana wanaweza kushinda vita kwa sababu wanajua kupigana msituni, milimani na mijini. Idadi kamili ya vifaa vyao vya kijeshi haijulikani.

Kiongozi wao wa sasa, Hebatullah Akhundzada, alichukua uongozi wa Taliban nchini Afghanistan kuanzia Jumatano ya Mei 26, 2016, wakati alipoteuliwa na baraza la ushauri la wanaharakati hao.

Uteuzi huo ulifanyika baada ya kiongozi wa zamani wa kikundi hicho, Akhtar Mohamed Mansour, kuuawa katika shambulio la anga lililofanywa na Marekani siku nne kabla ya uteuzi huo, Jumapili ya Mei 22, 2016.

Ingawa simulizi kadhaa za kihistoria zinadai kuwa Hebatullah alizaliwa mwaka 1961, tovuti ya Taliban inasema Hebatullah alizaliwa Alhamisi ya Oktoba 19, 1967 katika wilaya ya Bajway ya mkoa wa Kandahar na ana asili ya Pashtun.

Wapiganaji wa Taliban waliibuka mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakianzia kaskazini mwa Pakistan. Waliibuka baada ya kumalizika kwa vita vya Umoja wa Kisovieti huko Afghanistan.

Kama ilivyoelezwa hapo juu, washiriki wengi wa Taliban ni kutoka kabila la Pashtun, ambalo ni kabila kubwa zaidi nchini Afghanistan na inaaminika kuwa kwa mara ya kwanza, walifadhiliwa na Saudi Arabia ili kupambana na majeshi ya Urusi yaliyoivamia nchi hiyo Desemba 1979.

Mwishoni mwa Septemba 1996, baada ya miaka minne ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Afghanistan, Taliban ilifanikiwa kuteka mji wa Kabul na kisha kumuua Rais wa zamani Mohammad Najibullah kabla ya kutundika mwili wake kwenye nguzo ya barabara.

Picha za kushtua za rais aliyeuawa zilituma ujumbe kwa raia wa Afghanistan na dunia kwa ujumla kwamba Taliban sasa wameiteka nchi na kuweka “mfumo kamili wa Kiislamu” kwa Afghanistan. Bendera za Taliban zilianza kupepea juu ya ofisi za serikali huko Kabul, na wapinzani wao wa kijeshi walikimbilia ngome zao kaskazini.

Wakati wa utawala wao nchini Afghanistan, Taliban walipiga marufuku kusikiliza muziki na kwenda kwenye sinema.

Nchi zilizotambuliwa wakati wa utawala wa Taliban ni pamoja na Pakistan, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu.

Taliban waliendelea kuitawala Afghanistan hadi yalipotokea mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani Septemba 11, 2001.

Kisha, karibu mwezi mmoja baadaye, Oktoba 7, 2001, Marekani ikisaidiwa na washirika wake-Uingereza, Canada, Australia, Ujerumani na Ufaransa, ilianza kuishambulia nchi hiyo kwa kile kilichodaiwa kuwa ni “Vita dhidi ya ugaidi” kulipiza kisasi na hatimaye kuuondoa madarakani utawala wa Taliban.

Taliban baada ya miaka 20

Lakini miaka 20 baadaye, Taliban wameitwaa tena nchi hiyo baada ya kuanzisha mashambulizi nchi nzima, hususan baada ya wanajeshi wa Marekani kushindwa kuzingatia tarehe ya mwisho ya kuondoka Afghanistan ambayo ilikuwa ni Mei Mosi mwaka huu.

Vikosi vya usalama nchini Afghanistan vilijikuta kwenye mapambano makali dhidi ya Taliban, walioanzisha operesheni kubwa ya kijeshi katika mkoa wa kusini wa Helmand.

Vikosi vya usalama vya Afghanistan vilianzisha mashambulizi ya anga na kupeleka kikosi maalumu cha makomando katika eneo hilo, lakini walizidiwa na wimbi kubwa la mashambulizi na milio ya silaha nzito nzito na milipuko katika mji huo na milio ya silaha ndogo zilizosikika.

Maswali muhimu

Lakini je, hawa Taliban ni nani? Nini historia yao? Kwanini wanaonekana wana nguvu sana katika nchi ya Afghanistan? Kwanini magaidi wengi hudaiwa eti hutokana na kundi hilo? Nani anawapa silaha? Kwanini daima wamejiona kuwa jukumu lao ni siasa za Afghanistan?

Kuyajua yote haya, endelea na simulizi hii kesho.