Kutimuliwa kina Mdee kwaibua hoja ya Katiba

Muktasari:

  • Wakati baadhi ya wachambuzi wakipongeza uamuzi wa Chadema kuwafukuza wabunge 19 wa Viti Maalumu, wengine wanaona haja ya mabadiliko ya Katiba ili kuruhusu wawakilishi wa wananchi kuendelea na kazi zao bila kudhaminiwa na vyama.

  

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wachambuzi wakipongeza uamuzi wa Chadema kuwafukuza wabunge 19 wa Viti Maalumu, wengine wanaona haja ya mabadiliko ya Katiba ili kuruhusu wawakilishi wa wananchi kuendelea na kazi zao bila kudhaminiwa na vyama.

Baraza Kuu la Chadema lilithibitisha kuwafuta uanachama wabunge hao 19 juzi, baada ya kipindi cha mwaka mmoja cha kusubiri rufaa waliyokata kutokana na uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema wa kuwafuta uanachama Novemba 27 mwaka jana.

Awali baada ya kutolewa kwa uamuzi wa rufaa yao, Mdee akiwa na wenzake 18 katika viunga vya Mlimani City alisema atazungumza kwa kina wakati muafaka, lakini akasema, “sentensi moja ninayosema ni hivi, si tupo chini ya jua hapa, tunamuamini Mungu mmoja sio? Kilichofanyika pale ni uhuni hata Mbowe anajua.”

Baada ya kueleza hayo kwa wanahabari, Mdee alipigiwa makofi na wenzake waliosikika wakisema ‘imeisha hiyo….’ kisha wakapanda basi maalumu walilokuja nalo mchana na kuondoka eneo hilo.

Akizungumza kwa simu jana na Mwananchi kuhusu mwelekeo wao baada ya uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema, mmoja wa wabunge hao 19, Salome Makamba alisema kwa sasa wanajipanga kuona nini watafanya na baadaye watatoa taarifa.

“Tunajipanga, tutazungumza kujua nini tutafanya na tutatoa taarifa… hii ndiyo taarifa ninayoweza kukupa kwa sasa,” alisema.

Walipopigiwa simu kwa nyakati tofauti, wabunge wengine Grace Tendega na Sophia Mwakagenda, walijibu si mamlaka yao kuzungumza, mwenye dhamana hiyo ni mwenyekiti wao, Halima Mdee.

Alipotafutwa kwa simu Halima, simu yake iliita bila majibu na hata ujumbe kwa njia ya WhatsApp aliotumiwa haukujibiwa.

Wakati hayo yakijiri, Chama cha ACT-Wazalendo juzi kilitangaza utayari wa kuwapokea na kuwapa fursa ya kuendelea kufanya siasa baada ya uamuzi wa Baraza Kuu.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu jijini Mwanza mwishoni mwa wiki, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema uamuzi wa kuwapokea wabunge hao haumaanishi kwamba chama chake hakitambui au kinabariki makosa yao yaliyosababisha wavuliwe uanachama, bali unalenga kuwapa fursa ya kuendelea kufanya siasa.

“Utayari wa ACT-Wazalendo kuwapokea haumaanishi tunakubaliana na njia walizotumia kupata ubunge. Ni dhahiri walikiuka kanuni za siasa ya uwajibikaji wa pamoja katika uamuzi wa vikao na misimamo ya kitaasisi,” alisema Zitto.

Waipongeza Chadema

Baadhi ya wachambuzi wameipongeza Chadema, akiwemo Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema Baraza Kuu la chama hicho limepigia msumari uamuzi wa Kamati Kuu.

Kwa kuwa wanachama hao walijitwalia madaraka ya kwenda bungeni bila idhini ya chama chao, alisema kitendo hicho hakivumiliki, hivyo ilikuwa muhimu wachukuliwe hatua iliyochukuliwa.

“Ilikuwa muhimu chama kuchukua uamuzi huo, ukizingatia kina taratibu zake za kuteua wabunge wa Viti Maalumu lakini hawa walijiamulia wenyewe, ni makosa,” alisema.

Lakini, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema baada ya uamuzi huo wabunge hao wana nafasi ya kufungua shauri la rufaa mahakamani.

“Kama ni rufaa watakata mahakamani iwapo hawajaridhishwa na uamuzi wa Baraza la Chadema au kuna mapungufu wameyaona,” alisema.

Alisema baada ya Spika kupokea taarifa rasmi ya kufukuzwa uanachama kutoka Chadema bila shaka atawaondoa bungeni.

Lakini mwandishi wa habari mkongwe na Wakili, Jenerali Ulimwengu amelitazama suala hilo tofauti akisema, “Katiba yetu ina vifungu vigumu ambavyo ili uwe mbunge ni lazima udhaminiwe na chama cha siasa.

“Wakati wetu nilipokuwa mbunge, tulipinga hicho kifungu, lakini waliokuwa upande wa Serikali walishinda. Kimsingi tulisema Mtanzania yeyote ana haki ya kuwa mbunge na hivyo hakuna haja ya udhamini,” alisema.

Alikumbusha kisa cha aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbulu enzi za Mwalimu Julius Nyerere, Hermangild Sarwatt, ambapo kamati kuu ya Tanu iliengua jina lake na kumweka kiongozi aliyeitwa Amri Dodo na ndipo Sarwatt aliamua kugombea kama mgombea huru na kushinda.

“Nawaheshimu sana hawa wanawake, wamefanya kazi kubwa na kuleta matokeo makubwa nchini na kwa kweli wameonyesha mfano, kwa hiyo kuwaondoa bungeni ni pigo kubwa, japo wamekwenda kinyume na chama chao,” alisema.


Si wa kwanza kufukuzwa

Mbali na kina Mdee, Chadema iliwahi kumfuta uanachama aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini na naibu katibu mkuu, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Kitila Mkumbo mwaka 2015, kwa madai ya usaliti.

Hatua hiyo ilikomesha ubunge wa Zitto na nafasi ya Profesa Kitila ndani ya Chadema na baadaye waliibukia katika chama kipya wakati huo cha ACT-Wazalendo.

Chama cha Mapinduzi (CCM) pia kiliwahi kufanya hivyo mwaka 1988 kilipowafukuza wanachama wake, Maalim Seif Sharif Hamad, Hamad Rashid Mohamed, Juma Duni Haji, Shaban Mloo, Ali Haji Pandu, Khatib Hassan, Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid na Ali Salim kwa madai ya kuufitini uchaguzi wa mwaka 1985, kutokana na kutoridhika na uamuzi wa chama hicho, kumpitisha Abdul Wakili, kuwa mgombea urais wa Zanzibar.

Sophia Simba aliukosa ubunge wa Viti maalumu na nafasi ya uenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), baada ya CCM kumfuta uanachama mwaka 2017.