Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu aibua mapya mahakamani, ataka fidia

Muktasari:

  • Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.




Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameiomba Mahakama ya Rufani imwamuru Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kumlipa fidia kwa madai ya kuchelewesha usikilizwaji wa kesi dhidi yake na kumfanya aendelee kusota mahabusu.

Lissu ambaye amekuwa mahabusu tangu Aprili 10, 2025 kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya uhaini, alitoa ombi hilo jana wakati wa usikilizwaji wa shauri la mapitio, lililofunguliwa na Jamhuri dhidi yake.

Tangu alipofikishwa mahakamani hadi leo, ana siku 450 (mwaka mmoja, miezi miwili na siku 24). Kesi hiyo, kwa nyakati tofauti tangu ikiwa Mahakama ya Kisutu na Mahakama Kuu imekuwa ikisikilizwa na kuahirishwa mara kadhaa.

Akijibu hoja za Jamhuri kuhusu mapitio, Lissu ameiomba mahakama hiyo itupilie mbali ombi hilo, akisema halina msingi, bali limelenga kuchelewesha usikilizwaji wa kesi kumfanya aendelee kusota mahabusu.

Jamhuri ilifungua shauri hilo la maombi ya mapitio Februari 24, 2026, ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam kukataa maombi yake ya ruksa ili kuingiza ushahidi wa nyongeza katika kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa huyo.

Shauri hilo la mapitio namba 7203216/2026 limesikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Zainabu Muruke na Amour Khamis, sambamba na pingamizi lake dhidi ya shauri hilo.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga aliieleza Mahakama ya Rufani kuwa walitoa notisi ya kuongeza ushahidi wa nyongeza lakini Mahakama Kuu ikaukataa.

Alidai ushahidi hukataliwa baada ya kuwasilishwa mahakamani na kupimwa kwa vigezo vya kisheria kuona kama una uhusiano na kesi na iwapo shahidi anayekusudiwa kuutoa ana nguvu ya kisheria.

"Waheshimiwa majaji ndiyo maana lalamiko letu ni kwamba tumenyimwa haki ya kusikilizwa, ambayo ni haki ya Kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 13(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Katuga.

Alidai maelezo ya Mahakama Kuu kuukataa kwa maelezo kwamba ni ushahidi mpya kabla ya kuwasilishwa mahakamani kwanza, haikuwa sawa.

"Kwa hiyo, tumenyimwa haki ya kusikilizwa, sasa hili jukumu tutalitimizaje. Ndiyo maana tunasema ni jambo la hatari ushahidi kukataliwa kabla haujawasilishwa," amesema Wakili Katuga na kuhitimisha:

"Kwa hiyo tunasema maombi yetu ni ya msingi na chini ya kifungu cha 6 (3) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa (AJA) mahakama hii ina mamlaka ya kuyasikiliza."


Majibu ya Lissu

Akijibu hoja za Jamhuri, Lissu baada ya kunukuu uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika moja ya mashauri iliyokwishayaamua, amedai pale ambapo mamlaka ya Mahakama imezuiwa na sheria mdaawa hawezi kuruhusiwa kwa ujanja wa kuandaa nyaraka.

Huku akiisomea Mahakama Kuu mwenendo wa kesi ya msingi ya uhaini, Lissu amesema notisi ya Jamhuri ilisikilizwa rasmi Februari 23, 2026 na baada ya kusikiliza hoja za pande zote, ndipo Mahakama ilitoa uamuzi wake wa kuikataa.

"Haya yako kwenye kumbukumbu za mahakama. Mawakili wa Serikali wanakuja kuieleza mahakama hii kuwa hawakusikilizwa," amesema Lissu na kuongeza kwa sababu ya maombi hayo leo ni siku ya 139 bila kesi kusikilizwa.

Amesema ni kweli kwamba haki ya kusikilizwa ni ya Kikatiba lakini akahoji kwa ushahidi huo wanasemaje kuwa hawakusikilizwa, akisisitiza kwa mujibu wa kumbukumbu hizo za mahakama, Jamhuri haina hoja yoyote ya maana.

Amedai kuwa katika uamuzi huo mahakama kuu hakuna mahali iliposema kuwa ushahidi huo haufai, bali ilisema kuwa ushahidi huo ni mpya.

"Waheshimiwa naomba nimalizie kwa kusema maombi haya yameletwa kwa lengo la kuchelewesha kesi ya msingi na ukichelewesha kesi ya msingi, mjibu maombi anaendelea kukaa mahabusu. Leo ni siku ya 139, kesi ya msingi haisikilizwi na mimi nakaa gerezani, sina hatia," amesema Lissu na kuhitimisha:

“Ninachoomba si tu kukataa maombi haya, bali pia ninaiomba Mahakama yenu itumie mamlaka yake chini ya 367 CPA kutoa amri ambazo zinatolewa na Mahakama Kuu, kwa kumuamuru DPP anilipe fidia kwa kuchelewesha usikilizwaji wa kesi yangu kwa siku 139 kutokana na maombi hayo.”

Mbali na ombi hilo, Lissu amesema maombi ya mapitio ambayo Jamhuri imewasilisha Mahakama ya Rufani, hayana msingi wa kisheria kwa sababu yanapinga uamuzi wa Mahakama Kuu, ambao hauwezi kukatiwa rufaa wala kufanyiwa mapitio  kwa sababu yanalenga uamuzi wa muda, ambao haukuhitimisha kesi ya msingi.

Akinukuu uamuzi mbalimbali wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, Lissu amesema ni msimamo wa mahakama hizo kuwa uamuzi unaoweza kukatiwa rufaa au kufanyiwa mapitio ni ule unaohitimisha haki za pande zote katika shauri.

Kwa mujibu wa Lissu, uamuzi unaopingwa ulikataa notisi ya kuwasilisha ushahidi wa nyongeza, huku kesi ya msingi ikiendelea kama kawaida.

Pia amedai kuwa Jamhuri haina mamlaka ya kuiomba Mahakama ifanye mapitio ya mwenendo wa shauri katika mazingira hayo, kwa kuwa mamlaka hayo ni ya Mahakama yenyewe.


 Akijibu hoja za Lissu

Wakili Katuga amesema Lissu anaposema walisikilizwa, hakuwaelewa, akifafanua kuwa hoja yao ni kwamba hawakulisikilizwa kuhusu ushahidi walioomba kuuongeza na si kuhusiana na notisi ya kuongeza ushahidi huo.

Pia amepinga madai ya Lissu kuwa maombi hayo yameletwa kwa ajili ya kuchelewesha kesi, akisema si nia ya DPP, na kuwa kifungu alichokitumia Lissu kuomba fidia hakitumiki katika mazingira ya shauri hilo.

Amefafanua kuwa kifungu hicho kinatumika pale ambapo mahakama inakuwa imesikiliza kesi na kuamua kuwa haina msingi.

“Tunasisitiza, maombi yetu ni ya msingi na mahakama hii ina mamlaka ya kuhakikisha kuwa mwenendo wa Mahakama Kuu unakwenda kwa usahihi na kwa mujibu wa sheria,” alisema Wakili Katuga.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote imeahirisha shauri hilo mpaka itakapotoa uamuzi wake kwa tarehe ambayo wadaawa watajulishwa.


Kilichotokea mahakama kuu

Chanzo cha mvutano hadi Mahakama ya Rufani,  ni uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Februari 24, 2026 baada ya Jamhuri kuomba iruhusiwe kuwasilisha ushahidi wa nyongeza chini ya kifungu cha 308(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Upande wa mashtaka, Wakili Katuga, uliieleza Mahakama kuwa Februari 18, 2026 uliwasilisha notisi ya kuongeza ushahidi ambao haukusomwa wakati wa mwenendo wa ukabidhi, uliofanyika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Alieleza kuwa Mahamba alikuwa kiongozi wa timu ya upelelezi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na baada ya uchaguzi, kwamba ushahidi huo ulibainika Februari 16, 2026 walipokuwa wakimwandaa shahidi huyo.

Lakini Lissu alipinga maombi hayo akisema kifungu cha 308(1) cha CPA kinahusu ushahidi uliokuwapo wakati wa mwenendo wa ukabidhi lakini haukusomwa, si ushahidi uliopatikana baadaye.

Alisema kosa analokabiliwa nalo linadaiwa kutendeka Aprili 3, 2025 na alifikishwa mahakamani Aprili 10, 2025, ilhali ushahidi mpya unaoombea kibali kuingizwa unahusu matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Alieleza kuwa ushahidi wa ACP Mahamba ulishasomwa kwenye mwenendo kabidhi, hivyo mlango wake wa kuleta ushahidi mpya umeshafungwa.

Hivyo mahakama, ilikubaliana na Lissu na kukataa notisi hiyo, ikisema inakwenda kinyume na kifungu cha 308 cha CPA, ndipo Jamhuri ikafungua shauri hilo la mapitio Mahakama ya Rufani.