Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu aweka tumaini kuhusu Katiba Mpya

Muktasari:

Wakati Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akitarajia kurejea nchini Januari 25 mwaka huu, amesema Katiba mpya ni miongoni mwa kazi zinazomrejesha.

Dar es Salaam. Wakati Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akitarajia kurejea nchini Januari 25 mwaka huu, amesema Katiba mpya ni miongoni mwa kazi zinazomrejesha.

Lissu ameyasema hayo leo, Januari 13, 2023 alipozungumza na Watanzania kwa njia ya mtandao akiwa nchini Ubelgiji.

Amesema 2023 ni mwaka wenye historia nzuri ya nchi na iwapo watu wataamua Katiba mpya itapatikana, akisisitiza hata kurejea kwake ni kwa kazi hiyo.

“Ni mwaka ambao, kama tukiamua kwa dhati ya mioyo yetu, tutapata Katiba Mpya na ya kidemokrasia, yenye mfumo huru wa uchaguzi, inayojali na kulinda haki za wananchi na inayoweka misingi imara ya uwajibikaji wa viongozi wetu kwa wananchi na wawakilishi wao.

“Mimi binafsi na chama chetu tuko tayari na tumejiandaa kwa safari hiyo, kwa hiyo ninarudi nyumbani kwa ajili ya safari hiyo,” amesema Lissu.

Amelisisitiza hilo akirejea uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia mchakato huo, akisema ni wajibu kwa waliobaki kumuonyesha utayari kwa vitendo.

“Mimi binafsi na chama chetu tuko tayari na tumejiandaa kwa safari hiyo. Kwa hiyo ninarudi nyumbani kwa ajili ya safari hiyo. Ninarudi kwa ajili ya kazi kubwa iliyoko mbele yetu, kazi ya Katiba Mpya na mwanzo mpya kwa taifa letu,” amesema.

Hata hivyo, ameonyesha wasiwasi kuwa pamoja na ahadi za Rais Samia siku zijazo hazitakuwa rahisi, hivyo nia ya dhati ya kuifikia safari hiyo ndiyo silaha pekee.

“Ninajua kuwa tutakabiliwa na majaribu ya kila aina na tutapitishwa katika tanuru kubwa la matatizo na magumu mengi. Lakini licha ya mazingira hayo magumu na mbele ya changamoto kubwa na nyingi zitakazotukabili.

“Ninaamini kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yeremia, Mwenyezi Mungu anatuwazia sisi Watanzania mawazo ya kutustawisha na wala sio ya kutuumiza, mawazo ya kutupa tumaini kwa siku zetu zijazo. Tukiweka nia ya dhati na kuitekeleza kwa dhati, tutayashinda majaribio na magumu yaliyo mbele ya safari yetu,” ameeleza.