Lugangira: Matumizi hasi ya mitandao yaweza kukunyima fursa

Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira katika uzinduzi wa jukwaa la Dada’s Rise Coalition linalowanguanisha wanawake vijana viongozi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Muktasari:
- Vijana nchini wamehimizwa kutumia mitandao ya kijamii kwa usahihi kwani inaweza kuwa moja kati ya kisababishi cha kupata au kukosa fursa inapojitokeza.
Dar es Salaam. Vijana wametakiwa kuwa makini na kile wanachokiweka katika mitandao ya kijamii kwani kinaweza kuwa kisababishi cha wao kupata au kukosa fursa mbalimbali zinazojitokea katika safari yao ya maisha.
Wito huo umetolewa leo Novemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam na Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira katika uzinduzi wa jukwaa la Dada’s Rise Coalition linalowanguanisha wanawake vijana viongozi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya kidigitali Lugangira anaifananisha mitandao ya kijamii na wasifu binafsi (CV) unaotembea.
Lugangira amewahimiza vijana kabla ya kuweka kitu katika mitandao ya kijamii kutafakari kwa kina faida na hasara zake kwa sasa na baadae.
Anasema katika baadhi ya taasisi ili waweze kukupatia fursa fulani akitolea mfano ajira pia hupitia katika kurasa za mitandao ya kijamii ya muhusika.
Anaongeza kuwa kama ni mtu wa kuweka mambo yasiyofaa katika mitandao unaweza kujikuta unapoteza fursa hiyo ya kupata ajira.
“Hata katika baadhi ya nchi ili waweze kukupa visa huwa wanapitia katika kurasa zako za mitandao ya kijamii hivyo unaweza kujikuta unaikosa nafasi ya kupata visa kutokana na maudhui unayoweka katika mitandao”anasema.
Anaongeza kuwa matumizi sahihi ya mitandao katika zama hizi yanaweza kuchochea mabadiliko makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa, uchumi na kupunguza umaskini katika jamii.
Wanawake na uongozi
Lugangira pia alitumia fursa hiyo kuhimiza wanawake kuchangamkia fursa za uongozi na masuala ya siasa zinapojitokeza ili kufikia usawa wa kijinsia katika eneo hilo.
Pia amewataka kuondoa dhana kuwa ili uweze kuchaguliwa kuwa kiongozi katika upande wa siasa ni lazima uwe na historia ya muda mrefu katika siasa.
“Vilevile wanapojitokeza kuwania nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali jamii pamoja na wadau mbalimbali waweze kuwaamini na kuwawezesha kulifikia hilo”anasema.
Akizungumza kwa niaba ya waanzilishi wa jukwaa la Dada’s Rise Coalition linalounganisha viongozi mbalimbali wanawake vijana, Dk Jackline Tung’ombe amesema licha ya jitihada zinazofanyika bado kumekuwa na changamoto mbalimbali katika kufikia usawa wa kijinsia katika masuala ya uongozi.
Tung’ombe ametaja mfumo dume ambao unaanzia katika ngazi ya familia kama moja ya kikwazo kufikia usawa wa kijinsia katika masuala ya uongozi.
Anasema katika baadhi ya jamii bado hawaamini kama mwanamke anaweza kuongoza na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Bado elimu inatakiwa kuendelea kutolewa katika jamii ili kuondoa dhana potofu zilizopo ili kufikia usawa wa kijinsia katika masula ya uongozi”anasema.
Anasema hiyo ni moja ya sababu iliyowasukuma kuanzisha jukwaa hilo ili kuwajengea uwezo wanawake vijana viongozi katika taasisi mbalimbali.
Nae Naibu Mwakilishi Mkazi kutoka Un- Women, Katherine Gifford amewahimiza wanawake ambao wako katika nafasi mbalimbali za uongozi kuwa kiingizo chema kwa mabinti wanaotamani kuwa viongozi.
Pia kila mmoja kwa nafasi yake ajione ana wajibu wa kuwashika mkono na kuwaongoza ili waweze kuzifikia ndoto zao.