Maafa Hanang yafupisha mkutano wa Rais Samia Dubai
Muktasari:
- Maporomoko ya matope katika Wilaya ya Hanang iliyosababisha vifo na uharibifu wa mali za watu, yamemfanya Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa Dubai kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) arejee nchini kushughulikia kwa ukaribu janga hilo.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefupisha ratiba ya kuendelea kukaa Dubai kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) kufuatia tukio la maporomoko ya matope wilayani Hanang yaliyoua watu 49 na kujeruhi zaidi ya 80.
Maporomoko hayo yalitokea jana Jumapili, Desemba 3, 2023 alfajiri katika maeneo ya Katesh na Gendabi wilayani Hanang mkoani Manyara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 4,2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Zuhura Yunus ilieleza kuwa, Rais Samia amesikitishwa na hilo na ametoa pole kwa wafiwa wote kutokana na msiba mkubwa uliowakumba.
“Rais Samia ameamua kufupisha safari yake na kurejea nchini haraka iwezekanavyo ili kushughulikia kwa ukaribu janga hilo,”ameeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Samia amewahakikishia wananchi walioathirika kuwa Serikali iko pamoja nao na itahakikisha inawashughulikia masuala yote yaliyotokana na janga hilo.
Wakati huo huo Rais Samia kupitia taarifa hiyo ametoa maelekezo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa Serikali itagharamia mazishi ya wote waliopoteza maisha kutokana na mvua hizo.
“Majeruhi wote waliopo kwenye hospitali mbalimbali wapate matibabu yote yanayostahili kwa gharama ya Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kutoa msaada wa dharura na uokoaji,”imesema
Pia Rais Samia ameielekeza Serikali ya Mkoa wa Manyara na kitengo cha maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwasitiri.
Rais Samia amelekeza “Tathimini ya kina ifanyike juu ya maafa hayo na vitengo na taasisi zote za Serikali zinazohusika kuwepo kwa eneo la tukio na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali inarejea kawaida,”imesema taarifa hiyo
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maafa hayo yameathiri mji wa Katesh hususan vijiji vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta na pia vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay, na Sebasi.
Nyumba na mifugo ni miongoni mwa mali zilizoathirika na janga hilo huku kaya 1,150 zikiguswa na watu walioathirika hadi sasa ni 5,600 na inakadiriwa ekari 750 za mashamba zimeharibika.