Maalim Seif, hayupo lakini yupo

Muktasari:

  • Kongamano la tatu la kumuenzi Maalimu Seif Sharif Hamad litafanyika kwa siku mbili kuanzia kesho Jumamosi na litahusisha washiriki 180 wakiwemo wanasiasa wakongwe na wasomi.

Dar es Salaam. Wananchi wa Zanzibar na Bara kwa ujumla wanajiandaa kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi. Ni mapinduzi yenye historia ya kuvutia kwani, ndiyo yaliyoleta ukombozi kwa wanananchi wa visiwa hivyo maarufu duniani ambavyo baadaye viliungana na Tanganyika na hapo ikazaliwa Zanzibar.

Lakini, kuanzia kesho Jumamosi Novemba 25, 2023 kutakuwa na tukio kubwa linalotarajia kuwakusanya wanasiasa nguli, wasomi na wananchi kumjadili mtu mmoja mwenye historia yake kwa Zanzibar.

Huyu ni Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye hayupo duniani kwa sasa, lakini fikra, misimamo na dhamira yake kwa Zanzibar ipo na inaendelea kuishi.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akiwa na wanasiasa na wasomi, atakuwa miongoni mwa watu watakaoongoza kongamano la tatu la kumuenzi Maalim, ambaye aliaga dunia Februari 17, 2021 akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Mbali na Zitto, pia watakuwepo Profesa Kitila Mkumbo (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji), Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu, Chadema Zanzibar), Balozi Ali Karume, Mohamed Aboud Mohamed na Jenerali Ulimwengu.

Kwa upande mwingine wanasiasa vijana watakaoshiriki kongamano hilo ni pamoja na Rehema Sombi (Makamu wa Mwenyekiti wa UVCCM), Twaha Mwaipaya (Mratibu wa Uhamasishaji wa Bavicha), Mwanaisha Mndeme (Katibu wa Ngome ya Vijana ACT- Wazalendo).

Kwa upande wa wanahabari na wanaharakati ni pamoja na Tike Mwambipile Absalom Kibanda, Ezekiel Kamwaga, Salma Said, Maxence Melo, Hawra Shamte na Hamza Kasongo ambapo mada itakayojadiliwa ni ‘Siasa, Uongozi na Utawala - Tumekosea wapi, Tujisahishe vipi!

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa ya Ismail Jussa, ambaye ni Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maalim Seif, amesema kongamano hilo litahusisha washiriki 180 na litafunguliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, huku Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla akitarajiwa kutoa salamu maalumu. Othman ndiye aliyerithi mikoba ya Maalim Seif kwenye nafasi hiyo baada ya kifo chake.

Jussa amesema wameshirikiana na Tasisi ya Friedrich Neumann kuandaa kongamano hilo linalolenga kutafakari na kutathmini maudhui hayo kwa kuangalia mwenendo wa siasa na uongozi kitaifa na kimataifa, yakiwemo masuala ya kutetereka kwa maadili na misingi ya siasa na uongozi.

"Mambo haya yanaathiri ushindani ulio sawa katika uwanja wa siasa ikiwemo kuangazia mageuzi ya kisiasa na kiuchaguzi yanayofanyika iwapo yanakidhi haja na ushindani wa kisiasa,” amesema Jussa na kuongeza;

"Kwa upande wa kijamii tutaangalia namna ya kurudisha hamu na ushiriki wa rika la vijana katika siasa na uongozi, pia kuoanisha siasa na maendeleo.

Amesema masuala hayo yatachambuliwa na kujadiliwa kupitia uwasilishaji wa mada na mijadala ya jopo itakayowahusisha wanasiasa wazoefu, viongozi wa dini na asasi za kiraia, wasomi, waandishi wa habari, wanadiplomasia na wanasiasa vijana.

"Imani yetu mkutano wa mwaka huu utaendeleza sifa ile ile na kutoa fursa muhimu ya kujadili maudhui yaliyochaguliwa na kutoa mchango adhimu kwenye maendeleo ya siasa, uongozi na utawala ndani na nje ya nchi yetu," amesema Jussa.

Kwa mujibu wa Jussa, kongamano hilo litahudhuriwa na Mmusi Maimane ambaye ni Kiongozi wa Chama cha Build One South Afrika (Bosa) cha nchini Afrika Kusini.


Kuhusu Maalim Seif

Huwezi kuzungumzia historia ya Zanzibar bila kumtaja Maalim Seif, ni mmoja wa viongozi waliofanya mabadiliko makubwa katika visiwa hivyo tangu akiwa ndani ya chama tawala, serikalini kisha kuhamia upinzani.

Maalim Seif aliyezaliwa Oktoba 22, 1943 na kufariki Februari 21, 2021, amekuwa ni alama ya mabadiliko ya Zanzibar akishiriki kikamilifu kusimamia kile anachomiani kina manufaa kwa Wazanzibar.

Maalim Seif alianza kujifunza masuala ya uongozi wa Serikali mwaka 1975 alipoteuliwa kuwa Msaidizi binafsi wa Rais wa Zanzibar wakati huo, Aboud Jumbe ambapo aliifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977. Mwaka 1977, aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu wa Zanzibar hadi mwaka 1980.

Februari 1984, aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Maalim Seif amekuwa Waziri Kiongozi katika kipindi chote cha mwaka mmoja cha uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi kama Rais wa Zanzibar.

Mwaka 1985 Idris Abdul Wakil alipochaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, alimteua Maalim Seif kuwa Waziri Kiongozi na alishikilia wadhifa huo hadi Januari 1988 alipoondolewa kwenye Baraza la Mawaziri na baadaye kufukuzwa ndani ya CCM.

Kwa hivyo, mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar kuanzia mwaka 1977 – 1988.

Maalim Seif na wenzake kadhaa walifukuzwa CCM mwaka 1988 baada ya kutofautiana kimsimamo. Alikuwa mmoja wa waanzilishi wa vuguvugu la “Kamahuru” la Zanzibar lililoungana na CCW (Chama Cha Wananchi) ya Tanzania Bara na kuunda Chama Cha Wananchi (Cuf) ambapo yeye alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kwanza.

Kiongozi huyo alihudumu katika wadhifa huo hadi mwaka 1999 alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Cuf hadi Machi 2019 alipotangaza kujiunga na chama cha ACT Wazalendo baada ya Mahakama Kuu kumthibitisha Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa Cuf.

Akiwa upinzani, Maalim Seif alikuwa kwenye ushindani mkali na marais wanne wa Zanzibar: Salmin Amour, Amani Abeid Karume, Dk Ali Mohamed Shein na Dk Hussein Mwinyi, ambaye ni Rais wa sasa wa Zanzibar.

Maalim Seif amegombea urais mara sita katika maisha yake tangu ulipoanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Amekuwa sehemu ya mabadiliko ya kisiasa visiwani hapa na amekuwa chachu ya kubadilishwa katiba na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Baada ya machafuko yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001 kutokana na uchaguzi uliofanyika mwaka 2000, Maalim Seif pamoja na Rais Karume walikubaliana kukaa meza moja kuzungumza ili kupunguza joto la kisiasa.

Mazungumzo hayo maarufu kama “Mwafaka” wa CCM na Cuf, ndiyo yaliyopelekea mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 kuruhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambapo mgombea anayeshika nafasi ya pili anakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Maalim Seif alishika nafasi ya pili na kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, nafasi ambayo ameitumikia kwa miaka mitano hadi mwaka 2015.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, Maalim Seif alikataa kurudi kwenye uchaguzi baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi. Katika marudio hayo, Dk Shein alishinda, nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ikawa wazi kwa miaka yote mitano baada ya Maalim kugomea.

Mwakama 2020, Maalim Seif aligombea tena urais wa Zanzibar kupitia chama chake kipya cha ACT Wazalendo na kushika nafasi ya pili baada ya ushindi wa Dk Mwinyi. Maalim Seif akawa Makamu wa Kwanza wa Rais, nafasi ambayo aliitumikia hadi umauti ulipomfika Februari 17, 2021.

Historia inashuhudia kuwa Maalim Seif ndiye kiongozi mwenye uzoefu mkubwa wa kisiasa miongoni mwa viongozi wa upinzani. Ameshiriki siasa za Tanzania Bara na Zanzibar kwa zaidi ya miongo minne mfululizo.

Zaidi ya yote, amethibitika kuwa ni kiongozi mwenye msimamo usioyumba. Kwa hatua hiyo, ni vigumu na pengine haiwezekani kuandika historia ya Zanzibar bila kumtaja Maalim Seif.