Maaskofu Katoliki watoa waraka mzito

Saturday February 29 2020
pic maaskofu

Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini.

Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa waraka wa Kwaresima 2020 ambao mbali na masuala ya uinjilishaji, umezungumzia utawala wa kisiasa, wakisema unatakiwa ufanyike ndani ya mipaka ya sheria ya kimaadili.

Waraka huo wenye kichwa cha habari “Ujumbe wa Kwaresima 2020: Ufalme Wako Ufike”, umetolewa na maaskofu wote 33 wa majimbo ya kanisa hilo nchini Tanzania, wakiongozwa na Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, rais wa TEC.

Tofauti na miaka mingine, waraka mpya umetumia mada za Kibiblia, za kijumla, ukigusia masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ya nchi bila ya kunyoosha kidole.

Alipoulizwa kuhusu waraka huo ambao umechapishwa kwa ukamilifu na tovuti ya Redio Vatican, katibu mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima alisema ni kweli umetolewa na baraza hilo na umeshasambazwa katika parokia za kanisa hilo nchini.

“Ndiyo ni waraka wetu. Ujumbe wake unasema ‘Ufalme Wako Ufike’. Huwa tunautoa kila mwaka wakati wa Kwaresima, ila kila mwaka unakuwa theme (mada) tofauti ambayo maaskofu wanataka waumini waitafakari,” alisema Dk Kitima.

Alipoulizwa njia wanazotumia kuusambaza kwa wananchi, alisema wameuchapisha na unauzwa makanisani na kila kiongozi wa parokia anaufafanua kadri anavyoona inafaa.

Advertisement

Ujumbe uliomo katika waraka huo umeelekezwa kwa “wanafamilia ya Mungu – mapadre, watawa, waamini walei na watu wote wenye mapenzi mema”.

“Utawala wa kisiasa, uwe unatekelezwa na jumuiya yenyewe au na vyombo vinavyowakilisha dola, ni lazima daima ufanyike ndani ya mipaka ya sheria ya kimaadili,” unasema waraka huo.

Maaskofu hao wametoa ushauri huo wakirejea maazimio ya mkutano mkuu wa maaskofu wa dunia nzima (Mtaguso wa Pili wa Vatican), uliotoa maelekezo kuhusu ufalme wa Mungu na utawala wa watu.

Wanasema katika mkutano huo, uliofanyika kati ya Oktoba 11 1962 - Desemba 8, 1965), ilitolewa Hati ya Kichungaji juu ya Kanisa na ulimwengu, inayotambua hadhi ya binadamu na kuamsha juhudi za kuunda utaratibu wa kisiasa na kisheria, na kwamba haki za binadamu katika maisha ya hadhara zinalindwa vema zaidi

Hati hiyo, maaskofu hao wanasema, inasisitiza kuwa utekelezaji wa madaraka ya kisiasa daima unatakiwa ukusudie katika kumuunda mtu mwadilifu, mtulivu, na mkarimu kwa wote, kwa manufaa ya familia nzima ya wanadamu.

Pia wanasema “Ili kukuza maisha ya hadhara ya kisiasa, sharti ipatikane miundo ya kisiasa na kisheria inayowawezesha zaidi na zaidi raia wote – bila ubaguzi wowote – kushiriki kwa uhuru na kwa matendo katika kutengeneza misingi ya kisheria ya jumuiya ya kisiasa”.

Waraka huo umetolewa katika kipindi ambacho kuna kilio cha kutaka misingi ya sheria iimarishwe kwa kuandika Katiba mpya, na pia kutaka misingi ya haki katika uchaguzi iimarishwe kwa kuipa tume ya uchaguzi uhuru, mambo ambayo wanaoyadai wanasema yatawezesha ushiriki sawa wa wananchi katika masuala ya kisiasa.

Maaskofu hao wanasema lengo la miundo hiyo ya kisiasa na kisheria, ni kuongoza mambo ya dola, katika kuainisha uwanja wa kazi na mipaka yake kwa taasisi mbalimbali, na hatimaye katika kuwachagua viongozi.

Kwa sababu hiyo, waraka huo unawataka raia wote wakumbuke haki yao, ambayo pia ni wajibu, wa kutumia kura yao huru kwa minajili ya kuhamasisha manufaa ya wote.

“Kanisa linasifu na kuwathamini wale ambao, kwa ajili ya kuwatumikia wanadamu, wanajitoa kwa manufaa ya dola na kubeba uzito wa wajibu husika,” wanasema maaskofu hao.

Haki za binadamu

Maaskofu hao vilevile wamesema katika utambuzi wa hadhi ya binadamu, mtaguso unasisitiza wajibu wa kuhakikisha haki za binadamu katika maisha ya hadhara zinalindwa vema zaidi.

Wanazitaja haki hizo kuwa ni haki za kujumuika na kuunda umoja kwa uhuru, haki ya kila mmoja kutoa maoni yake na kukiri imani yake akiwa peke yake au hadharani.

“Ulinzi wa haki za binadamu ni sharti la lazima ili raia, kila mmoja peke yake au kama wanachama, aweze kushiriki kimatendo maisha ya umma na uongozi wa mambo yanayowahusu,” wanasema.

Siasa safi

Pia, maaskofu hao wamerejea ujumbe wa kiongozi wa kanisa hilo duniani, Papa Francis, alioutoa katika Siku ya kuombea amani duniani Januari 1, 2019 kuhusu umuhimu wa siasa safi kama huduma ya amani.

Wanasema katika ujumbe wake Papa alisema “siasa safi ni nyenzo inayosaidia ujenzi wa huduma kwa binadamu, lakini siasa ikitumiwa vibaya inaweza kuwa chombo cha dhuluma, mipasuko na hatimaye kusababisha madhara makubwa kwa jamii”.

Pia wanasema:“Amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu, hasa kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka, na matokeo yake ni matumizi mabaya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu.”

Katika ujumbe huo, Papa Francis ananukuliwa akimwelezea mwanasiasa bora kuwa ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii na anayeaminika na kuthaminiwa na jamii.

Pia kwamba mwanasiasa safi ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mwaminifu katika ahadi zake kwa waliomchagua na anayejitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano.

Suala hilo pia limekuwa likizungumzwa na wanasiasa wa upinzaninchini ambao wamekuwa wakitaka mazungumzo ya pamoja ili kuimarisha mshikamano katika nchi.

Maaskofu hao wanasema suala la siasa safi pia liliwahi kuzungumziwa na Papa Paulo VI kuwa “ikichukuliwa katika umuhimu wake kuanzia ngazi ya kijiji, kimkoa, kitaifa na kidunia - ni kukubali wajibu wa kila mtu kukiri ukweli na thamani ya uhuru ambao unatolewa kwake na jamii kuufanyia kazi kwa manufaa mazuri ya mji, taifa na binadamu wote”.

Mungu hutoa mamlaka

Viongozi hao wa dini wamezungumzia mamlaka ya watawala kuwa yametoka kwa Mungu kulingana na maandiko, lakini mamlaka hayo yanatakiwa yatekelezwe kadri ya mpango wa Mungu.

“Iwapo raia watakosea, basi namna inayofaa kadiri ya mpango wa Mungu, itumike kuwakosoa,” wanasema. “Watawala wameshirikishwa hadhi ya baba mwenye upendo na huruma ambaye anahukumu kwa haki na ambaye anakemea na kukaripia kwa uvumilivu na mafundisho.

Pia wanasema “watawala wanalo jukumu la kuwaadhibu watu waovu kwa mujibu wa sheria halali za nchi, pia wamesisitiza kuwa raia hawana ruhusa ya kuwatii viongozi pale wanapowaamuru kutenda kinyume na amri za Mungu.

“Ni muhimu kuzingatia kuwa kujiweka chini ya mamlaka haya hakumaanishi kwamba ni lazima tutii kama vipofu amri inayotolewa na dola ambayo ni mbaya au inakwenda kinyume na amri ya Kristo ya kuwapenda jirani zetu,” unaeleza waraka huo.

Wanasema raia wanapotii mamlaka iliyoko, mamlaka hiyo nayo lazima imtii Mungu.

“Hivyo, mamlaka inapoacha kutunuku matendo mema au tabia njema, au inapoacha kuadhibu maovu, na badala yake ikaamrisha mambo yaliyo kinyume, mamlaka hiyo inapoteza nguvu au uwezo wake wa kimaadili wa kuongoza watu,” unasema waraka huo.

Advertisement