Mabarobaro 130 wafungishwa ndoa, watakiwa kudumisha ndoa
Muktasari:
- Vijana hao 130 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam na nje ya mkoa huo wamejumuika katika ukumbi wa DYCCC uliopo Wilaya ya Temeke na kufungishwa ndoa na viongozi mbalimbali wa dini.
Dar es Salaam. Mabarobaro 130 walioomba msaada wa kulipiwa mahari na Taasisi ya Al Hikma Foundation, wamefungishwa ndoa kwa pamoja, huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi akiahidi taasisi hiyo kuunganishwa na mamlaka zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi na ajira ili kuwawezesha vijana hao kumudu familia.
Vijana hao wamefikia kigezo cha kufungishwa ndoa, baada ya Taasisi ya Al Hikma Foundation, Machi mosi mwaka huu katika mashindano ya kimataifa ya Quran, kutangaza kusaidia vijana wenye nia ya kuoa.
Kundi ambalo limetajwa la vijana, ni wale ambao wamekwama kulipa mahari na sharti ni mwanamke kwenda kuchukua fomu kwa niaba ya mtarajiwa wake.
Sharti lingine, lilikuwa lazima mwanamume awe anajishughulisha na kazi yeyote, wazazi wa pande mbili waridhie ndoa hiyo, hivyo ni baadhi ya vigezo ambavyo vimewezesha vijana 130 kupatikana.
Hadi sasa jumla ya vijana wa kiume 500 wamelipiwa mahari kwa ajili ya kuoa na taasisi hiyo tangu 2023.
Leo Jumapili, Juni 7, 2026 wilayani Temeke ambapo vijana hao kwa pamoja kutoka ndani na nje ya Dar es Salaam wamefungishwa ndoa, Katambi amesema kwa upande wa Serikali vijana ambao wamekuwa kwenye biashara, kilimo na sekta zingine Serikali inawapa fursa.
Maharusi wa kiislamu 130 wakiwa katika hafla ya kufungishwa ndoa ya pamoja, ambayo imeandaliwa na taasisi ya Al-Hikma Foundation, jijini Dar es Salaam, Juni 7, 2026.
"Kwa kutumia fursa hizi, tutaunganisha taasisi ya Al Hikma Foundation na mamlaka zote zinazotoa mikopo, ajira na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ili hawa vijana waliooa leo ambapo wanakosa fedha za mkupuo waingie kwenye fursa mbalimbali za kiuchumi za Serikali," amesema.
Katambi amesema vijana waliojitambua na wenye malengo, lazima Serikali iwatengenezee mazingira wezeshi na kwa Wilaya ya Temeke, ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuanza kuwezesha vijana hao kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
Waziri huyo amesema hatua ya taasisi hiyo kufungisha vijana hao ndoa ni muhimu kwa Serikali kwa sababu ni kiunganishi muhimu ya masuala ya amani nchini.
Amesema maadili kwenye jamii huanzia ngazi ya familia, akisisitiza familia ndio msingi mkuu wa maadili kwa Taifa lolote.
"Ukizungumzia ulinzi wa Taifa letu tunaanzia kwenye familia, kama hakuna maadili kwenye familia tutarajie mama muhalifu na baba muhalifu na watoto watakaozaliwa watakuwa wahalifu na kuingia kwenye migogoro ya kuvunja sheria za nchi, kwa hiyo maadili ni msingi mkuu wa maendeleo la Taifa lolote," amesema.
Kwa upande mwingine, Katambi ametaja sababu ya ndoa kuvunjika ni tamaa na kukosa uaminifu kwani watu wanashindwa kuvumiliana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Al Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki amesema vijana hao kabla ya kuozeshwa wamepewa elimu ya ndoa na hata wanapokwenda kuanzisha familia wakipata changamoto hutakiwa kurudi kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya utatuzi.
Amesema lengo la kuweka kigezo kijana kuwa na shughuli ya kujiingizia kipato, ni kusaidia ndoa hiyo kudumu kwani bila kipato wakifungishwa ndoa huvunjika ndani ya muda mfupi.
Baadhi ya maharusi wa kiislamu 130 wakiwa katika hafla ya kufungishwa ndoa ya pamoja, ambayo imeandaliwa na taasisi ya Al-Hikma Foundation, jijini Dar es Salaam, Juni 7, 2026.
"Tumeamua kuwalipia vijana hawa mahari kwa sababu, tumegundua wengi wapo tayari kuoa lakini wamekosa fedha za pamoja kulipa mahari, tukaona ni muhimu kuichangia jamii kupunguza maovu, ndoa husaidia kulinda maadili kwenye nchi na jamii," amesema.
Akizungumzia shughuli ya kuwaozesha vijana hao, Sheikh wa Mkoa Dar es Salaam, Walid Alhad Omar amesema ndoa kwa vijana inasaidia kupunguza makundi maovu kwenye jamii hususan panya rodi.
Pamoja na faida hiyo, amenukuu taarifa aliyoitaja ni ya Wizara ya Katiba na Sheria mwaka jana ambayo ilionyesha ongezeko la ndoa kuvunjika kutoka 70 kwa mwaka juzi hadi kufikia 1,180 mwaka jana akiwataka vijana kupunguza kasi ya kuvunja ndoa.
"Mwanamke anahitaji zaidi kuolewa lakini akiingia kwenye ndoa anataka kuachika, kwa hiyo lazima wanaume muitunze ndoa," amesema.
Akitoa darasa kwa vijana hao namna ya kulinda ndoa zao, Sheikh Mahara Mziwanda amelitaka kundi hilo kuzingatia mambo matano ikiwemo kuhakikisha mwanamke aliyemuoa anakuwa moyoni, kwani ndoa nyingi hazidumu kutokana na mwili kutotumika ipasavyo kwenye ndoa.
“Ndoa ni ulimi wako, jeraha la ulimi linaumiza zaidi kuliko mikuki, hakuna kitu wanachopenda wanawake kama kusifiwa na mwanamke asiposifiwa haamini kama yupo na wewe.”
"Pia ndoa ni akili, ni namna gani unafikiri kuiboresha kupitia maneno unayonena kwa mke wako lakini pia si kila jambo utakayosikia kuhusu mke wako au mume wako na kufanyia kazi," amesema.
Naye Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ali Ngeruko amesema Taasisi ya Al Hikma inatengeneza Taifa bora kutokana na kazi wanazofanya.
Amesisitiza kuwa wakati umefika kuwashirikisha vijana katika mambo mbalimbali kwa kiwango kikubwa kwani ili kuwa na Taifa salama lazima kuwa na vijana wenye matunzo.