Machifu Mbozi wajitosa kutetea haki za wanawake

Machifu kutoka maeneo mbalimbali Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufanya kikao kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuunda kamati itakayosimamia haki za wanawake katika wilaya hiyo.
Muktasari:
- Ili kukomesha ukatili na kuhamasisha usawa wa kijinsia katika jamii, Machifu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wameunda kamati ambayo itayosimamia utekelezaji wa maazimio ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia na kutetea haki za wanawake na wajane.
Mbozi. Ikiwa baadhi ya mila na desturi za baadhi ya jamii nchini Tanzania zinaathiri usawa wa kijinsia, viongozi wa kimila maarufu machifu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wameunda kamati ambayo itasaidia kusimamia mambo mbalimbali yanayomkandamiza mwanamke ikiwamo kuwatetea katika masualaya umiliki wa mali, ardhi, ushiriki katika maamuzi na kutetea haki zao.
Machifu ni miongoni mwa viongozi wa jamii ambao wanatoa na kusimamia utekelezaji wa maagizo ya kimila ambayo yakitekelezwa yanaweza kuathiri au kuleta afya katika maendeleo ya mwanamke.
Miaongoni mwa baadhi ya mila katika jamii zimekuwa kikwazo zikiwazuia wanawake kushiriki katika vikao vya maamuzi, umiliki wa mali hata kama amezalisha yeye pamoja na umiliki wa ardhi.
Katika kuondoa dhana hiyo, machifu wa Wilaya ya Mbozi wameunda kamati ambayo itasimamia mambo mbalimbali ambayo yanakuwa kikwazo cha kumuinua mwanamke.
Kamati hiyo ambayo ina wajumbe 15 imetangazwa katika kikao cha machifu kilichofanyika katika ukumbi wa Shimoni Village Vwawa mjini wilayani Mbozi Julai 9, 2022.
Katika kikao hicho ambacho kilikuwa na ajenda kuu nne ikiwemo kutetea haki za kina mama, wajane na watoto waliozaliwa nje ya ndoa kiliwakutanisha machifu 23 wa Wilaya ya Mbozi.
Katibu wa machifu Wilaya ya Mbozi, Galifunga Nzowa amesema kuwa miongoni mwa maazimio yao ni kuunda kamati ambayo imepewa jukumu la kusimamia na kutetea haki za wanawake hasa wa vijijini ambao wanadhulumiwa mali zao.
Amesema kamati hiyo pamoja na mambo mengine itafuatilia, kusimamia maelekezo ya machifu hasa katika maeneo ya vijijini ambapo wanawake wengi wanakosa elimu ya kutambua haki zao.
Chifu Galifunga amesema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya ndugu kuwadhulumu wanawake wajane pale waume zao wanapofariki huku wanawake hao wakikosa sehemu za kuwasilisha malalamiko yao.
“Ukiangalia sisi machifu ndio wasimamizi wa mila katika maeneo yetu, tumeipa jukumu kamati kwenda kutoa elimu kwa wanawake ambao wanaonewa ili waweze kupata haki zao" amesema kiongozi huyo wa kimila na kuongeza;
"Kwa kuwa machifu tunaheshimika sana kwenye jamii tumeona tuwe na mkakati wa kuwatetea wanawake. Kamati hii itakutana na kina mama katika maeneo mbalimbali na kuzungumza nao kuwasikiliza shida zao na kuwapa njia. Pengine changamoto hizo zinaweza kutatuliwa huko huko" amesema
Akizungumzia mkakati huo wa kutetea haki wanawake, Chifu Galifunga amesema pamoja na kuunda kamati lakini kila chifu ametakiwa kuhakikisha katika eneo lake anatoa matamko yanayopinga dalili za ukandamizaji wa mwanamke.
"Sisi kama viongozi wa kimila tuna matamko yetu ambayo tukiyatoa mtu akiyakiuka anaweza kupata matatizo.
Tumekubaliana tukawaelimishe wananchi wetu kupinga ukatili dhidi ya mwanamke, wajane na watoto. Hili litasaidia sana" amesema katibu huyo wa viongozi wa kimila wilaya ya Mbozi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati hiyo ya machifu, Chifu Hazole Msyete amesema wananchi watatambulishwa kamati hiyo ili iwe rahisi kupata ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.
“Inatakiwa wananchi watambulishwe kamati, mkuu wa Mkoa na wilaya wameshatupa rungu kwa hiyo inabidi tulitumie” amesema Chifu Hazole ambaye amebainisha kuwa viongozi wa Serikali mkoani hapo wamepewa mamlaka ya kusaidia kutetea haki za wanawake katika jamii yao.
Akizungumza namna ya kurahisisha kamati hiyo kuwafikia wananchi, Chifu Hazole amesema wameandaa utaratibu wa kupita katika kila kata ambapo mwenyeji atakuwa chifu wa kata husika ili kusikiliza wanawake ambao wanachangamoto.
“Kila kata tutafika na mwenyeji atakuwa chifu wa eneo husika, tutazungumza na wanawake ambao wanachangamoto hasa wale ambao wamedhulumiwa mali. Lakini piua tutatumnia mikutano ya hadhara kutoa elimu” amesema mjumbe huyo wa kamati ya kutetea haki za wanawake ya machifu ambaye pia ni chifu wa kata ya Vwawa.
Ushiriki wa wanawake
Ili kuhakikisha kuwa wanawake wanahusishwa katiaka kufikia maamuzi ya changamoto zinazowakumba, Chifu Msyete ameeleza kuwa baadhi ya wanawake watashirikishwa katika vikao vya usuluhishi na utatuzi wa migogoro.
Pia, amesema kuwa anaamini kuwa pale pale anapodhulumiwa mwanamke mmoja lazima kuna wengine ambao watakuwa wanajua changamoto hiyo hivyo watawatumia kama mashahidi.
“Tunachotaka ni kuwafanya wanawake wajisikie huru, tutawaita kutoa Ushahidi lakini hata kwenye kufikia maamuzi tutawashirikisha. Hii itakuwa ni njia ambayo tunaona watajisikia faraja” ameeleza
Mwenyekiti wa machifu Wilaya ya Mbozi, Mswaula Shitindi amesema kuwa kamati hiyo imeelekezwa kwenda kuwasikiliza wanawake hasa wale wanaopitia changamoto za kudhulumiwa mali walizochuma.
“Kuna changamoto kubwa hasa vijijini, mama anazalisha mazao lakini hana mamlaka nayo.
Unakuta mzee ndio anakuwa na sauti baadha ya kuvuna, huu ni uonevu hivyo tumeona tuwe na mkakati wa kukutoa elimu kwa wanawake waamke na wajue haki zao” ameeleza Chifu Shitindi ambaye pia ni kiongozi wa kimila wa kata ya Iyula.
“Wanawake wajane wananyanyasika baada ya wenza wao kufariki dunia ambapo baadhi yao wananyang’anywa mali ambazo wamepata pamoja na wenza wao, hili haliwezi kuvumiliwa. Ndio maana tumekuja na mkakati huo wa kuteua kamati” amesisitiza.
Akizungumza katika kikao hicho Chifu wa Iwalanje kata ya Igamba, Msulwa Mwalembe amesema kuwa wanawake wengi wanapitia changamoto katika familia hivyo viongozi hao wa kimila wahakikishe maazimio yanayofikiwa wayasimamie ipasavyo.
“Sisi machifu tunaogopwa kwenye maeneo yetu. Kama tumeamua kuanza kuwatetea wanaweke tujitolee kweli na tusimamie maazimio yetu ipasavya,
“Tunatakiwa kwenye vikoa tutakavyofanya vya kamati tunawashirikisha baadhi ya wanawake ili waone kuwa tunamaanisha tunachokifanya.
Tukiwatenga bado itakuwa haileti picha ya kuwatetea” amesema Chifu Mwalembe ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo.
Wanawake wafunguka
Wakizungumza na Mwananchi kuhusu mkakati wa machifu wa kutetea haki za wakinamama, baadhi ya wanawake wamesema kuwa mpango huo kama utatekelezwa unaweza kuwa chachu ya maendeleo kwa wanawake.
Mkazi wa kata ya Hezya wilayani Mbozi, Anna Mwashitete amesema kuwa wanawake wengi wamekuwa wakionewa na waume zao lakini wanavumilia kutokana na kukosa sehemu za kueleza shida zao.
“Kama machifu wameamua kuingilia kati, hili linaweza kuzaa matunda kwa sababu wakati mwingine unaweza ukapitia changamoto ukafikiria uende kushitaki lakini ukikumbuka kuwa kuna mambo ya mila unaamua kuacha,
Kwa vile viongozi hao ndio wameamua wenyewe hii itaturahisishia sisi tukikumbana na manyanyaso tunajua wapi pa kukimbilia” ameeleza.
Halima Haziko ambaye ni mkulima wa kahawa na mkazi wa kata ya Msia amesema kuwa mkakati huo umemfurahisha kwa kuwa miaka miwili iliyopita alipitia changamoto ya kudhulumiwa mali baada ya mume wake kufariki dunia kutokana na mambo ya kimila.
“Mimi mume wangu alifariki mwaka juzi, baada ya hapo ndugu walichukua mali karibia zote. Hali hiyo iliniumiza sana ukizingatia nipo kwenye majonzi lakini pia mali zinachukumiwa. Kuna mila zingine hazifai” amesema Halima ambaye ni mama wa watoto watatu.
Maoni ya Anna na Halima yanaendana na Stela Mwaikambo ambaye anapongeza jitiuhada hizo za viongozi wa kimila za kutetea haki za wanawake katika wilayaya mbozi.
Stela anasema kuwa hali hiyo itawatia nguvu wanawake katika kuongeza jitihada za uzalishaji ili kuleta maendeleo.
“Kuna wakati mtu unapitia changamoto mpaka unakata tamaa. Unalima lakini unajua tukivuna mzee atauza na kutumia hela kwenye ulevi na ukimuuliza unaambulia kipigo. Hili la machifu kuingilia kati limeleta sura mpya kwa wanawake wa Mbozi” amesema
Wadau wawapa tano machifu
Baada ya machifu hao kuunda kamati hiyo ya kutetea haki za wanawake wa Wilaya ya Mbozi, baadhi ya wadau wameeleza kuwa hatu hiyo inaweza kuwa chachu ya mafanikio ya wanawake huku wakitaka wajumbe hao kufika maeneo ya vijijini ambayo elimu ya haki za wanawake inahitajika zaidi.
Mbunge wa jimbo la Vwawa, Japhet Hasunga amewawapongeza machifu hao kwa kufikia maazimio hayo ambayo kama yatatekeleza vizuri yatasaidia kutokomeza ukatili wa kijinsia katika wilaya hiyo.
“Nawashukuru kwa kufanya kikao na naamini kwa kikao hiki kinakuja kuleta mafanikio ya kuigwa.
Tunatamani tuwe na Mbozi yenye usawa wa kijinsia hivyo kwa kuanza na ninyi (machifu) mtakuwa mmetengeneza njia,
Jitihada hizi ni sawa na malengo ya Serikali ambayo inatamani kufikia asilimia 50/50 kati ya wanaume na wanawake katika fursa mbalimbali.
Niwapongeze sanba machifu kwa kuliona hili” amesema Mbunge huyo ambaye alihudhuria katika kikao hicho.
Mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake kutoka Wilaya ya Mbozi, Leah Mwansojo amesema kuwa jituihada hizo za machifu zinatakiwa kuungwa mkoo na jkilka mmoja.
Leah ambaye ni miongoni mwa waaznzilishi wa tuzo zinazotolewa kwa kila mwaka kwa wanawake wanaojitahidi katika Nyanja mbalimbali katika Mkoa wa Songwe amesema kuwa “Binafsi nawapongeza machifu kwa hatua hiyo.
Unajua kuna wakati mambo ya kimila ndio yanakuwa kikwazo cha maendeleo ya mwanamke lakini ukiona viongozi hao wamefikia hatua ya kuunda kamati basi ujue kuna kitu wamekiona;
“Ninachowaomba waanzie kwenye ngazi ya familia, mwanamke anapopewa elimu akafahamu hakizake ni rahisi kusimama.
Wanawake wengi wanapitia changamoto na hawana pa kusemea ndio maana hata sisi kwa Mkoa wa Songwe kila mwaka tunaandaa semina, matamasha na tuzo.
Tunafanya hivi kuwaamsha wanawake na wakihudhuria unaona kabisa kuna mabadiliko” amesema Leah
Wakili wa kujitegemea, Emmanuel Mwazembe amesema kuwa inawezekana uamuzi wa machifu hao umesukumwa na ukatili unaofanyika katika jamii.
“Unajua kuna kesi nyingi sana za ukatili. Mara mwanamke amenyang’anya mali, mara amepigwa yote hay ani kumkandamiza mwanamke. Kama viongozi wa kimila nao wameliona basi inaweza kusaidia kutatua changamoto hiyo” amesema wakili huyo.