Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madaktari bingwa kutoka Muhimbili watibu 410 kambi ya matibabu Tabora

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Dk Respicious Boniface akitoa taarifa kuhusu kambi ya siku tano ya matibabu iliyoshirikisha Madaktari bingwa kutoka taasisi hiyo na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga. Picha na Robert Kakwesi.

Muktasari:

Kambi hiyo ya matibabu ya siku tano imewashirikisha Madaktari Bingwa watano kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwemo wataalam wabobevu wa mishipa ya fahamu na dawa za usingizi.

Tabora. Wagonjwa 410 wameonwa na kupatiwa matibabu na Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wakishirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga wakati wa kambi ya matibabu ya siku tano.

Akitoa taarifa ya kambi hiyo leo Ijumaa Machi 31, 2023, Mganga Mkuu Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, Dk Tito Chaula amesema wagonjwa hao ni kutoka mikoa ya Kanda ya Magharibi ambapo wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji akiwemo mtoto mdogo aliyekuwa na tatizo la mgongo wazi.

Dk Chaula ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi amewashauri Watanzania kujenga utamaduni wa kupima na kujua afya zao ili kupata tiba mapema ugonjwa ukiwa katika hatua za awali.

“Muitikio wa wagonjwa kuja kupimwa na kutibiwa umekuwa mkubwa katika wiki moja ya kambi yetu ya matibabu, hali inayodhihirisha mahitaji ya huduma za matibabu ya kibingwa,” amesema Dk Chaula

Amesema Hospitali ya Rufaa ya Nkinga inayotoa huduma za kibingwa katika maeneo kadhaa inafanya jitihada za kuanzisha huduma za kibingwa katika mfumo wa mishipa ya fahamu ambayo kwa sasa haijaanza kutolewa.

“Tumeanza kuwajengea uwezo wataalam wetu kufikia hatua ya huduma za kibingwa katika mfumo wa mishipa ya fahamu ambayo bado haipatikana katika hospitali yetu,” amesema Dk Chaula

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Dk Respicious Boniface amesema kambi za matibabu ya kibingwa inalenga kutekeleza kwa vitendo maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kwaa Waziri wa Afya, Ummy  Mwalimu ya kufikisha huduma hiyo kwa wananchi hadi maene ya vijijini.

“Kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Rufaa Nkinga tumeweza siyo tu kuhudumia zaidi ya wagonjwa 400, bali pia tumebadilishana uzoefu wa kitaaluma,” amesema Dk Boniface

Ameahidi kuwa MOI na Hospitali ya Rufaa Nkinga wataendeleza ushirikiano kwa kubadilishana uwezo na utaalam kuhudumia wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa.

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, Victor Ntundwe ameushukuru uongozi wa MOI kwa kukubali kushiriki kambi hiyo ya matibabu huku akifchua kuwa uwepo wa madaktari Bingwa wa MOI umewawezesha wenzao wa Nkinga kupata uzoefu.

 “Madaktari wa Hospitali ya Rufaa Nkinga wamenufaika kwa kupata ujuzi na uzoefu kutoka kwa wenzao wa MOI ndani ya siku hizi tano za kambi ya huduma ya matibabu ya kibingwa. Ni rai yangu kwamba ushirikiano huu unapaswa kuwa endelevu kuwezesha wananchi kupata huduma za kibingwa katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri hadi Dar es Salaam,” amesema Ntundwe

Kambi hiyo ya siku tano imewashirikisha Madaktari Bingwa watano kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwemo wataalam wabobevu wa mishipa ya fahamu na dawa za usingizi.