Madaktari bingwa wa meno kupiga kambi ya siku tano Tosamaganga

Muktasari:
Huenda ikawa ni ahueni kwa wagonjwa wa mataya na wale wa magonjwa ya kinywa baada ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakishirikiana na Taasisi ya Pindi Chana na Taasisi ya Give A Future kujipanga kutoa huduma bure
Dar es Salaam. Wakazi wa Tosamaganga mkoani Iringa wanatarajia kunufaika na kambi ya siku tano ya madaktari bingwa wa kinywa na taya kwa kupatiwa matibabu bila gharama yoyote.
Kambi hiyo itakayofanyika katika Hospitali ya Tosamaganga inajumuisha uchunguzi wa kinywa, taya na upasuaji kwa watakaobainika kuwa na matatizo huku ukiwalenga watu wa rika zote.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Pindi Chana na Taasisi ya Give A Future jana, Aprili 9, 2024 inaeleza kuwa Aprili 15 na 16, 2024 itakuwa ni kwa ajili ya uchunguzi kwa wagonjwa watakaofika hospitalini.
“Halafu Aprili 17 hadi 19 itakuwa ni maalumu kwa wagonjwa watakaobainika kuhitaji msaada wa upasuaji, wagonjwa hawa watapokewa hospitalini kwa matibabu kulingana na tarehe zilizotajwa,” amesema Rishen Patel ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Give A Future.
Kwa mujibu wa Patel wagonjwa watakaoonwa katika kambi hiyo ya upasuaji wa magonjwa ya kinywa na mataya watapewa matibabu bure.
Akitaja miongoni mwa magonjwa yatakayofanyiwa matibabu ni uvimbe wa mataya, vidonda vya kinywa, matatizo ya fizi pamoja na matatizo mengine yanayohusu meno na kinywa.
“Lengo letu kuu ni kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora za kimatibabu bila kugharamia chochote kutoka mfukoni kwao ili kuongeza ubora wa maisha yao,” amesema Patel.
Kambi hii inakwenda kufanyika ikiwa ni siku chache tangu dunia iadhimishe siku ya kinywa ambayo hufanyika Machi 20 kila mwaka.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa watu bilioni 3.5 wana matatizo ya kinywa na meno huku wito ukitolewa kwa watu wote kuzingatia utunzaji mzuri wa kinywa ili kuepuka magonjwa hayo.
Moja ya njia ya kuepuka matatizo ya kinywa na meno ni kuzingatia usafi ikiwamo kupiga mswaki mara mbili kwa siku au kila baada ya kula.
WHO inatoa wito kuhakikisha mswaki sahihi unatumika na unatunzwa kwa mujibu wa kanuni za afya na kinywa angalau kila baada ya miezi mitatu mswaki ubadilishwe.