Kuna uhusiano mkubwa kati ya afya ya kinywa na mwili

Muktasari:
- Kwa lugha nyingine ni kwamba, kinywa ni zaidi ya tabasamu zuri la mwanadamu yeyote yule duniani. Ukiamka kisha ukaondoka nyumbani bila kusafisha kinywa chako kwa kupiga mswaki, siyo tu kwamba utakuwa kero kwa utakaozungumza nao kutokana na harufu mbaya, bali utajiondolea amani na furaha yako kwa kuona haya kuzungumza mbele ya watu.
Huwezi kujiachia kwa kicheko kama kinywa chako siyo kisafi na kinatoa harufu.Tabasamu la kila mtu hutegemea zaidi usafi wa kinywa chake na hata mng’ao wa meno.
Kwa lugha nyingine ni kwamba, kinywa ni zaidi ya tabasamu zuri la mwanadamu yeyote yule duniani. Ukiamka kisha ukaondoka nyumbani bila kusafisha kinywa chako kwa kupiga mswaki, siyo tu kwamba utakuwa kero kwa utakaozungumza nao kutokana na harufu mbaya, bali utajiondolea amani na furaha yako kwa kuona haya kuzungumza mbele ya watu.
Kiuhalisia, kinywa kichafu ni kero kwa wale unaozungumza nao au walio karibu nawe.
Mkazi mmoja wa Ubungo Msewe, Dar es Salaam, Hilda Justine anasema wakati alipokuwa mjamzito alishawahi kutapika baada ya kukutana na kinywa kilichokuwa kikitoa harufu kwa sababu ya sigara, pombe na uchafu.
“Siku moja nilijikuta natapika katikati ya safari baada ya kukodi bodaboda ambayo dereva wake alikuwa amekunywa pombe halafu akaamka bila kupiga mswaki na kuingia kazini. Harufu ya kinywa chake ilikuwa mbaya sana na nilijisikia vibaya mno,” anasema Hilda.
Anasema baada ya kutapika, alimweleza ukweli dereva huyo athali za kinywa chake kuachwa bila kusafishwa jambo lililomfanya akiri kutosafisha kinywa chake kwa sababu ya haraka ya kuwahi wateja.
Ili kuelimisha umma, hivi sasa madaktari wa afya ya kinywa na meno wameamua kutumia ‘Wiki ya Afya ya Meno’ inayohitimishwa Machi 20, Wilayani Tarime Mkoani Mara, kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kutunza afya ya kinywa.
Wakiongozwa na kauli mbiu ya ‘Sema ahh, fikiria kinywa, fikiria afya ya meno’, madaktari hao wanasema kinywa kisafi humfanya mtu kuwa huru kuzungumza na yeyote wakati wowote.
Rais wa Chama Cha Madaktari Wanafunzi wa Kinywa na Meno Tanzania (TDSA), Evarist Wilson anasema ni muhimu kuelewa kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya afya ya kinywa na afya ya mwili.
Anasema kinywa kinaweza kuonyesha hali ya lishe ya mtu, dalili za maradhi mengine ya mfumo kama wa kisukari, maradhi ya mfumo wa upumuaji, maradhi ya moyo na baadhi ya saratani.
Anasema pia huonyesha tabia ya mtu kama ni mvutaji wa sigara na mtumiaji wa vilevi (pombe) ikiakisi afya yako kwa ujumla.
“Kinywa ndicho kinachokufanya uzungumze, utabasamu, ule chakula, unywe na kufanya shughuli nyingine za kimaisha ikiwamo kuongeza ujasiri na uhusiano wako wa kila siku na watu wengine,”anasema Dk Wilson.
Anazungumziaje kinywa kisicho na afya
Dk Wilson anasema kinywa kisicho kisafi husababisha maumivu na muhusika kutojisikia vizuri na wakati mwingine mhusika uhisi harufu mbaya mdomoni, utapiamlo na humpunguzia ujasiri na kupoteza muda wake wa kazi au shule kutokana na maumivu ayapatayo.
Anasema kuna maradhi mengi yanayoweza kushambulia kinywa ikiwamo ya saratani, meno kutoboka na hata maradhi ya fizi.
Takwimu zinaonyesha maradhi ya kinywa huathiri takribani watu bilioni 3.9 duniani kote, huku saratani ya kinywa ikiua watu milioni 8.8 duniani,” anasema Dk Wilson.
Namna ya kujikinga na maradhi ya kinywa
Wahenga walisema ‘Kinga ni bora kuliko tiba’ hivyo ni bora kuwa na kinga ya maradhi kuliko kusubiri matibabu baada ya ugonjwa husika kukukuta.
Madaktari wa vinywa wanasema inawezekana kabisa kujikinga na maradhi ya kinywa kwa kuepuka vihatarishi, kuzingatia lishe na usafi wa kinywa kama inavyoshauriwa.
Dk Wilson anasema kula kwa afya ni hatua ya kwanza ya kukikinga kinywa dhidi ya maradhi hayo.
“Matumizi ya mara kwa mara ya vyakula vyenye sukari ni kihatarishi cha maradhi hayo, kwakuwa husababisha kuoza kwa meno, kisukari na maradhi ya moyo,” anasema na kuongeza;
“Wazazi na walezi wengi huwapa watoto wao pipi kama njia ya kuwabembeleza bila kujua kwa kufanya hivyo wanahatarisha vinywa vya watoto wao.”
Dk Wilson anasema unaweza kuepuka maradhi ya kinywa na meno kwa kuepuka matumizi ya bidhaa za tumbaku.
“Matumizi ya tumbaku aidha kwa kuvuta sigara, ugoro ama tumbaku kwa namna nyingine yoyote ni kihatarishi cha maradhi ya fizi na saratani za aina mbalimbali ikiwamo ya kinywa na mapafu. Pia matumizi ya tumbaku huchangia maradhi ya moyo na ya mfumo wa upumuaji,” anasema Dk Wilson.
Anasema pia matumizi ya pombe huweza kuhatarisha afya ya kinywa ili kuepuka ni muhimu kupunguza.
Anasema unywaji wa pombe kupita kiasi ni kihatarishi cha zaidi ya maradhi 200. Miongoni mwake ni ya kinywa na ni chanzo kikubwa cha ulemavu katika nchi nyingi zilizoendelea.
“Pombe pekee ama na sigara kwa pamoja huongeza hatari ya kupata saratani ya kinywa, maradhi ya fizi na meno kuoza kwa sababu ya kiwango chake cha sukari,” anasema.
Ili kuepuka hali hiyo, Dk Wilsoni anashauri kupiga mswaki walau mara mbili kwa siku hasa asubuhi na usiku kabla ya kulala.
“Hii husaidia kulinda fizi zako na mara zote, hakikisha sehemu zote za meno yako zimepigwa mswaki,” anasema.
Anasema pia ni vizuri kutumia dawa ya meno yenye madini ya floraidi kwa kuwa kupiga mswaki pekee hakuzuii meno kutoboka.
“Inatakiwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya floride, usisukutue kinywa chako kwa maji baada ya kupiga mswaki na dawa yenye fluoride ili kuruhusu kiwango cha kutosha cha dawa kinywani ili kulinda meno yako,” anasema