Fanya hivi kulinda afya ya kinywa na meno

Muktasari:
- Kwa usaidizi wa misuli ya taya na mashavuni, kinywa hupata nguvu ya kufanya kazi ya kuvunja vunja vyakula na kuwezesha kumezwa na kupita katika bomba la chakula.
Moja ya maeneo muhimu ya mwili ni kinywa. Eneo hili huanzia sehemu ya nje ya mdomo, meno, fizi, ulimi, eneo la mwanzo la koo na paa na kitako cha mdomo.
Kinywa huwa na jukumu la awali la mfumo wa chakula la kikuvunja vunja na kukilowesha na mate kwa ajili ya kuanza usagaji wa vyakula tunavyokula.
Kwa usaidizi wa misuli ya taya na mashavuni, kinywa hupata nguvu ya kufanya kazi ya kuvunja vunja vyakula na kuwezesha kumezwa na kupita katika bomba la chakula.
Kutokana na kinywa kuvunja vunja vyakula, eneo hili huwa na mabaki kadhaa ambayo huweza kubaki na kuchachishwa na bakteria wa mdomoni.
Magonjwa ya mara kwa mara yanayoshambulia kinywa ni pamoja na kuoza meno, shambulizi la fizi, vidonda mdomoni na rangi ya meno kubadili na meno na udhaifu
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa watu bilioni 3.5 wana matatizo ya kinywa na meno.
Hivyo suala la utunzaji kinywa na meno ni jambo muhimu kwa jamii toka nchi zenye uchumi wa chini mpaka wa kati ambako huduma za kinywa bado si nzuri.
Ukiacha faida ya kiafya tunayopata kwa kutunza kinywa, faida nyingine husaidia kuepuka gharama zisizo na lazima. Duniani moja ya matibabu yenye gharama ni kinywa na meno.
Hivyo ni muhimu kufahamu dodondoo muhimu, ili kutunza kinywa huku ukiwa na meno imara yenye uwezo wa kustahimili kazi ngumu za kutafuna.
Jambo la kwanza ni aina ya maji unayokunywa, yanahitajika kuwa safi na salama. Maji rafiki kwa meno imara ni yale ambayo huwa na madini ya floride. Upungufu wa madini hayo huwa na matokeo mabaya kwa Aaya ya meno.
Uzingatiaji wa kila siku wa usafi wa kinywa kwa mujibu wa wataalamu wa afya kinywa kwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku au kila baada ya kula.
Itahitajika kutumia mswaki sahihi unaotunzwa kwa kujibu wa kanuni za afya ya kinywa, angalau kila baada ya miezi mitatu kutumia mswaki mpya.
Tumia dawa za meno zinazopendekezwa na wataalamu wa afya ya kinywa ikiwamo zenye madini ya floride.
Epuka matumizi ya mara kwa mara ya kuchokonoa meno na vijiti, kwani huchangia kuongeza nafasi kati ya jino na jino.
Tazama na uwe makini na aina ya vyakula unavyokula, kwani vipo ambavyo si rafiki wa kinywa ikiwamo vyenye sukari nyingi.
Kunywa maji mengi angalau glasi 10 kwa siku ili kuepukana na tatizo la ukavu wa kinywa.
Epuka matumizi ya tumbaku na pombe kwani yanaharibu ubora wa meno na kuchangia harufu mbaya mdomoni.
Kwa wagonjwa kama wa kisukari ni vema kuhakikisha wanashikamana na matibabu na njia za kujikinga ili kudhibiti kupanda kwa sukari, kwani hali hii inachangia magonjwa ya kinywa ikiwamo shambulizi la fizi.
Hakikisha unahudhuria kliniki za wataalamu wa afya kinywa hata kama kinywa chako kina afya njema, angalau kwa miezi sita mara moja. Jiongezee maarifa ya afya ya kinywa na meno kwa kufika katika huduma za afya zilizo jirani.