Madaktari wa moyo Kuwait kutibu watoto bure Dodoma

Mwonekano wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati Benjamin Mkapa.

Muktasari:

  • Madaktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka nchini Kuwait kuweka kambi ya huduma kwa watoto Benjamin Mkapa.

Dodoma. Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka nchini Kuwait wanatarajiwa kuweka kambi ya siku tano kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kati Benjamin Mkapa.

Kufuatia hali hiyo wazazi wa watoto wenye viashiria vya magonjwa ya moyo wametakiwa kuwapeleka watoto kwa kuwa huduma ya uchunguzi na kumuona daktari ni bure.

Miongoni mwa viashiria vilivyotajwa kutolewa huduma ni mtoto kutoongezeka uzito, kuchoka, kikohozi cha mara kwa mara, kushindwa kuhimili mazoezi, kupumua kwa shida na kushindwa kunyonya au kutokwa jasho jingi wakati wa kunyonya.

Katika taarifa iliyotolewa leo Januari 26, 2023 na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na uhusiano hospitalini hapo, Jeremiah Mbwambo ilisema huduma hizo zitaanza kutolewa Februari 6 hadi 10, 2023 saa mbili asubuhi na kumalizika saa tisa alasiri.

“Wazazi wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kumuona daktari ni bure, ikiwa mtoto atagundulika na tatizo basi atapata huduma ya upasuaji kutoka kwa madaktari hao kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa hospitali yetu,” amesema Jeremiah.