Madaktari washauri kipimo cha mkojo kuokoa figo zinazofeli

Muktasari:

  • Wakati madaktari wakiomba Serikali iangalie namna ya kukifanya kipimo cha mkojo kuwa cha lazima kama ilivyo shinikizo la damu ‘presha’ ili kudhibiti changamoto ya figo kufeli, takwimu za afya za hivi karibuni zinaonyesha wagonjwa wanaopatiwa huduma za usafishaji damu (dialysis) nchini imefikia 3,250 huku waliopandikizwa figo idadi yao ikifikia 335.

Dar es Salaam. Wakati madaktari wakiomba Serikali iangalie namna ya kukifanya kipimo cha mkojo kuwa cha lazima kama ilivyo shinikizo la damu ‘presha’ ili kudhibiti changamoto ya figo kufeli, takwimu za afya za hivi karibuni zinaonyesha wagonjwa wanaopatiwa huduma za usafishaji damu (dialysis) nchini imefikia 3,250 huku waliopandikizwa figo idadi yao ikifikia 335.

Ushauri huo ulitolewa kufuatia mkutano wa madaktari bingwa wa figo ulioagiza kuangalia suluhisho la ongezeko la magonjwa hayo.

Wataalamu hao wanasema mgonjwa anapoanza kuwa na tatizo la figo katika hatua ya kwanza na pili hugundulika kupitia kipimo cha mkojo kwa kuangalia wingi wa protini.

Daktari bingwa wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige alisema,“Protini kwenye mkojo ndiyo sababu mojawapo, ingawa inaweza kupanda kutokana na kufanya mazoezi, lakini ukimuona mtu anakuwa na protini kwenye mkojo na inazidi kiwango ni vyema kwenda kufanyiwa kipimo cha figo.

“Napoona mgonjwa ana protini nyingi namshauri afanyiwe kipimo hiki na wakibainika hatua za awali wanapewa matibabu wanapona kabisa.”

Dk Mzige aliwahi kuwa mkurugenzi wa kinga Wizara ya Afya mwaka 2005 ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kliniki ya Mshangai iliyopo Korogwe mkoani Tanga, anasema kuna haja ya kuhakikisha kinga inafuatwa mapema kuliko kusubiri tiba inayogharimu fedha nyingi.

Anataja changamoto nyingine ni vituo vya afya vinapowapima wagonjwa hutoa majibu matatizo katika mfumo wa mkojo (UTI) na kuishia kuwapa dawa mengi zinazoendeleza kuumiza zaidi figo.

“Anakwambia una UTI wakati huna kumbe una tatizo la figo na wengi wanaokaa pembezoni wengi wana shida ya figo kwa kuwa hawanywi maji ya kutosha,”anasema Dk Mzige.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya, Profesa Pascal Rugajjo anasema magonjwa ya figo hasa sugu yanaongezeka nchini na inakadiriwa kati ya watu 100, saba wana tatizo hilo.

“Namna pekee ambayo ni nzuri ya kujilinda ni kujiwekea utaratibu wa kupima mara kwa mara angalau mara moja kwa mwaka kwa wale wasio na magonjwa ya presha au kisukari,” anasema Profesa Rugajjo.

Anasema wenye historia ya magonjwa hayo wanashauriwa kupima kila robo au nusu mwaka wenye umri wa zaidi ya miaka 40 ni vizuri wakapima mara mbili kwa mwaka.

“Kundi hili ni muhimu kupima shinikizo la juu la damu, kisukari lakini protini kwenye mkojo, kupima kwa namna hii kutasababisha ugunduzi wa mapema ili kuweka mipango endelevu ya kujilinda pia kwa wale wanaotoka kwenye familia ambazo zina wagonjwa wa kisukari au shinikizo la juu la damu au ugonjwa figo waweke utaratibu huu,” anasema.

Pia, anasema wenye viashiria hatari vya mwanzo wanapaswa kuwa na mpango wa ufuatiliaji wa afya huku akitoa angalizo kwa watu kuacha matumizi ya dawa za mitishamba ambazo hazijathibitishwa ikiwamo matumizi ya dawa za Kichina na Kikorea.

Chanzo figo kuharibika

Wakati hayo yakisemwa, kuna aina nne za magonjwa ya figo ikiwamo figo kutofanya kazi au kufeli, mawe kwenye figo au kuziba kwa njia ya mkojo, figo kupoteza protini na maambukizi kwenye figo.

Daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo Dodoma, Kessy Shija anasema figo zinapofeli wataalamu huangalia chanzo ili kubaini iwapo zimefeli ghafla au ni tatizo lililoiumiza figo kwa muda mrefu.
“Figo huumia kidogo kidogo na bahati mbaya maumivu ya kwenye figo hauwezi kuyatambua mpaka utakapofika hatua ya mwili kushindwa kuchuja taka mwili.

“Tatizo la kufeli kwa ghafla hutokea iwapo mtu amepata ajali na kumwaga damu nyingi, figo huchuja damu isipopata damu ya kutosha inaweza ikaumia au kupoteza maji mengi kwa kuharisha au kutapika hiyo ni mshtuko yaani ghafla,” anasema Dk Kessy ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Figo.

Anasema kufeli kwa figo ni changamoto kubwa kwa sasa dunia kote na Tanzania kuna tafiti chache zimefanywa na ukubwa wa tatizo umeonekana kwa asilimia 7 mkoani Kilimanjaro na asilimia 15 Kisarawe, lakini hiyo ni nje ya hospitali zinazotoa huduma ya magonjwa ya figo kuanzia waliolazwa au kuhudhuria kliniki.

Dk Kessy anasema kwa Afrika chanzo kikuu ni shinikizo la juu la damu au presha na ugonjwa wa kisukari pamoja na unywaji holela wa dawa.