Madiwani Simanjiro wataka watumishi wanne wahamishwe

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Jacob Kimeso akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la kupitia taarifa za Kata zao 18, kulia ni Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo Dominica Ngaleka na kushoto ni Katibu wa UWT Wilayani Simanjiro Leokadia Fissoo. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Kati ya watumishi hao wanne walioazimiwa kuhamishwa, mmoja ni Ofisa mtendaji wa mamlka ya Mji mdogo wa Mirerani na mwingine ni mwanasheria wa Halmashauri

Simanjiro. Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, limeazimia mmoja kati ya wanasheria wa Halmashauri ya wilaya hiyo na watumishi watatu wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, wahamishwe.

Baraza hilo limetoa azimio hilo kwenye kikao chao cha kujadili taarifa mbalimbali maendeo na changamoto za kata zao 18, kilichofanyika Januari 31 mji mdogo wa Orkesumet.

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Jacob Kimeso, amesema madiwani hao wameridhia watumishi hao wanne wahamishwe kwenye nafasi zao.

Kimeso amesema ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, ofisa ardhi, ofisa ushirika wa mamlaka hiyo na mmoja kati ya mwanasheria wa halmashauri wahamishwe.

Hata hivyo, ofisa maendeleo ya jamii Asia Ngaliwason amesema suala la watumishi hao kuhamishwa linapaswa kuzungumziwa faragha na halipaswi kuelezewa wazi kwenye baraza hilo.

Diwani wa Kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer amesema azimio hilo ni uamuzi wa madiwani wa halmashauri hiyo kwani kamati ya fedha, iliazimia suala la kuhamishwa kwa watumishi hao.

Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Mnyawi amesema migogoro ya uuzaji ardhi kiholela hususani eneo la shamba la Maro limesababishwa na viongozi hao hivyo wahamishwe.

Hata hivyo, ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Evence Mbogo amesema amefanya kazi yake ipasavyo hivyo hana lolote la kuzungumza juu ya hilo.