Maelfu wajitokeza kumzika Paroko aliyeuawa Karatu
Ibada ya Misa Takatifu kabla ya maziko ya Paroko Pamfili Nada, aliyeuawa Kanisani Karatu
Muktasari:
- Padri Pamfili Nada aliuawa Julai 19 na Roman Leonard (30) mtu anayedhaniwa kuwa na matatizo ya afya ya akili kwa kupigwa na chuma kichwani.
Mbulu. Maelfu wajitokeza kwenye maziko ya Padri Pamfili Nada aliyeuawa wilayani Karatu Mkoa wa Manyara, na mtu anayedaiwa kuwa na matatizo ya afya ya akili.
Katika misa hiyo iliongozwa na Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbulu, Antony Lagweni, pia ilihudhuriwa na Mhashamu Askofu wa Jimbo la Singida, Edward Mapunda, na Wakuu wa Wilaya za Mbulu na Karatu ambao ni Kheri James na Dadi Kolimba.
Taarifa za kipolisi zimethibitisha kuwa Padri Nada aliuawa Julai 19, 2023 kwa kupigwa na chuma kichwani, na Roman Leonard (30), ambaye anayedhaniwa kuwa na matatizo ya afya ya akili.
Katika mahubiri yake, Mhashamu Askofu Lagwen amewasihi wakristu kuwa watulivu katika kipindi hiki cha msiba na pia wapokee kwa imani taarifa hizo za kusikitisha.
Askofu Lagweni amesema Padri Nada alifanya utume wake bila kuogopa na hata kifo chake kimetokea akiwa anapambana kulilinda kanisa.
Kwa upande wake Askofu Mapunda, amesema jamii inapaswa kuiga matendo ya kusimamia haki kama alivyokuwa anafanya Padri Nada kipindi cha uhai wake.
Akizungumza kwenye ibada hiyo ya maziko, DC James amesema, tatizo la afya ya akili lipo na lina madhara makubwa kwa jamii kwani ndiyo chanzo cha kifo hicho.
“Familia na jamii kwa ujumla inapaswa iangalie na kudhibiti matatizo ya afya akili kwa kuwapeleka katika vituo vya afya vinavyohusika, ili matatizo kama haya yasijitokeze,” amesema James.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Kolimba amesema wao kama Serikali pia wanalitegemea kanisa hivyo kifo cha Padri Nada ni pigo kwa kanisa na Taifa kwa ujumla.
“Padri Nada alikuwa kiongozi na sisi watu wa Serikali pia tunalitegemea kanisa kutokana na kuisaidia jamii, ni pigo kwa kifo hicho ila jamii inapaswa, kuimarisha ulizi shirikishi ili kuepuka matukio kama haya,” amesema.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha, Justin Masejo amesema Padri Nada alifariki dunia baada ya kupigwa kichwani kwa chuma na mtu mwenye matatizo ya afya ya akili ambaye naye aliuawa na kundi la watu.
Padri Nada alizaliwa Mei 6 mwaka 1962 akapata upadrisho mwaka 1997 na Julai 19 mwaka 2023 akapoteza maisha kwa kuuawa parokiani kwake.