Padri alivyouawa, kutupwa mtoni
Muktasari:
Ni wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya
Mbeya. Ni mauaji ya kikatili. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mwili wa Padri Michael Samson kukutwa kando mwa mto Meta ukiwa umeviringishwa kwenye blanketi.
Padri Samson ni wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) aliyekuwa akifanya kazi na Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.
Juzi jioni, Askofu Mkuu wa jimbo hilo, Gervas Nyaisonga alitoa taarifa ya kuokotwa kwa mwili wa padri huyo aliyesema alitoweka kwenye kituo chake cha kazi cha vijana tangu Juni 10, na kupatikana juzi Jumamosi saa 12:30 jioni akiwa amefariki dunia.
Tukio hili limetokea ikiwa imepita miezi michache tangu Padri Francis Kangwa, raia wa Zambia wa shirika hilo la White Fathers aliyekuwa akifanya kazi na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Parokia ya Mtakatifu Yohanne Paul II, Mbezi Mshikamano, kukutwa amefariki dunia ndani ya tanki la maji kwenye nyumba ya mapadri wa shirika hilo.
Tanki hilo liko nyuma ya nyumba ya mapadri wa shirika hilo, Mtaa wa Sokoine katika jengo la Ottoman jijini Dar es Salaam.
Akisimulia tukio hilo jana, shuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Simon Amos alidai kuwa mtoto ambaye hajafahamika ndiye aliubaini mwili wa padri huyo anayedaiwa kuuawa na watu wasiojulikana, alipokuwa akipita eneo la mto Meta.
Amos ambaye pia ni dereva bodaboda alisema juzi, saa 3:30 asubuhi mtoto huyo alikuwa akipita kwenye njia iliyo kando mwa mto Meta na alipouona mwili huo, alikimbia na kwenda kuwaita madereva bodaboda waliokuwa wameegesha pikipiki zao jirani na eneo hilo.
“Tulipofika tuliuona mkono uliovishwa saa ukiwa ndani ya maji tukausogelea tukaona kuna mwili uliokuwa umeviringishwa blanketi, tukawatafuta viongozi wa Serikali akiwemo Mwenyekiti wa Mtaa wa Sabasaba Kata ya Mbalizi na Polisi ambao walifika na kuuopoa. Walipofungua wakakuta viungo vyake vimetenganishwa,” alisimulia Amos alipozungumza na Gazeti la Mwananchi na kuongeza;
“Mauaji haya ni ya kinyama, marehemu alichinjwa kama kuku. Ametenganishwa kichwa, kiwiliwili, miguu na shingo inasikitisha sana.”
Mwenyekiti wa Mtaa azungumza
Mwenyekiti wa Mtaa wa Sabasaba, Ally Mbika alikiri kutokea tukio hilo, huku akilaani mauaji hayo ambayo aliyaita ni ya kikatili na kinyama.
“Mwili uliviringishwa kwenye blanketi na kilichokuwa kikionekana ni mkono ambao umevishwa saa, lakini viungo vilikuwa tofauti. Kichwa, shingo, miguu na kiwiliwili vilitengenishwa,” alisema Mbika.
Watumishi waeleza
Asteria Lunguya, mmoja wa watumishi wa kituo cha vijana, alisema Padri Samson alikuwa na ratiba za kufanya mazoezi ya kutembea kila jioni maeneo ya karibu na kituo hicho.
“Hata siku hiyo aliyotoweka, aliondoka hapa na kwenda kufanya mazoezi, na hakuwahi kutuambia kama alikuwa amekwazana na mtu au anaumwa, afya yake ilikuwa imara na hakuwa na mambo mengi zaidi ya kazi,” alisema Lunguya.
Alisema taarifa za kifo cha padri huyo walianza kuzisikia juzi, saa saba mchana. “Hatukaumini, tukawa tunajipa moyo, huenda si za kweli na tukawa tunasubiri taarifa rasmi. Kwa kweli kwetu ni pigo, tumempoteza kiongozi mwema,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi, mlinzi wa kituoni hapo, Theresia Mwela alisema siku aliyotoweka Padri Samson, alikuwa yuko lindo, alipopita langoni wakasalimiana akamuaga anakwenda kwenye mazoezi.
Lakini hadi anamaliza muda wake wa kazi saa 12 jioni, alikuwa hajarejea na siku iliyofuata ndipo alipata taarifa za kifo chake.
Neno lake la mwisho
Akisimulia kuhusiana na mahubiri yake ya mwisho aliyoyatoa Jumapili ya Juni 5, mwaka huu, Mhudumu wa kituo hicho, Robert Maekena alisema Padri Samson alisisitiza watu wazidi kumuomba Mungu kwa kuwa ulimwengu wa sasa umekengeuka, vitendo vya kikatili vinazidi kushamiri.
“Nakumbuka Jumapili yake ya mwisho kanisani alisema pia viongozi wa dini wanapaswa kushukuru na kumuomba Mungu kwa anayowakinga nayo akisema vitendo vya ukatili vimekithiri,” alisema Maekane, ambaye pia ni Mwenyekiti wa utumishi wa kituo hicho cha vijana.
Viongozi wa dini walaani
Kadhi wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Mbarazi alisema ni masikitiko makubwa na wanalaani ukatili huo. “Hata vitabu tukufu vinapinga kuua nafsi yako na ya mwingine isipokuwa kwa haki, unapomuua kiongozi wa dini inamaana unazima sauti za amani, kwa ujumla ni masikitiko na huzuni kwetu,” alisema Sheikh huyo.
Naye mchungaji wa Kanisa la Efatha Mbeya, Philipo Mollel alisema vitendo hivyo ni kumchukiza Mungu, lakini hata kama hawakamatwi wanaofanya unyama huo, mkono wa Mungu utawakamata.
“Hivi vitendo vimeshamiri sana, hata huku Uyole kumeibuka mauaji ya watoto akiwamo mtoto wangu alinisurika juzi kuuawa, yote haya aidha ni kubeba vinyongo au kutaka kubeba imani za kishirikina ambapo Mungu atatukasirikia sote,” alisema.