Maeneo manne kudhibiti uchumi

Muktasari:

  • Mhariri wa takwimu wa Mwananchi Communications Ltd, Halili Letea ametoa angalizo katika maeneo manne yanayoweza kuathiri mwenendo wa ukuaji wa uchumi, ambayo ni urari wa biashara, thamani ya shilingi, mfumuko wa bei na ukuaji wa pato la Taifa.

Dar es Salaam. Mhariri wa takwimu wa Mwananchi Communications Ltd, Halili Letea ametoa angalizo katika maeneo manne yanayoweza kuathiri mwenendo wa ukuaji wa uchumi, ambayo ni urari wa biashara, thamani ya shilingi, mfumuko wa bei na ukuaji wa pato la Taifa.

Pia, amegusia umuhimu wa kuepuka athari za uhaba wa dola unaoathiri kwa kiwango shughuli za kiuchumi kutokana na mahitaji yake kwa zaidi ya asilimia 80 kwenye miamala ya kimataifa.

Halili ametoa rai hiyo leo Desemba 27, 2023 wakati wa mjadala unaohoji “Mwaka 2023 ulikuwaje kiuchumi, kisiasa na kijamii. Lengo ni kutazama makosa yaliyojitokeza na kuyarekebisha mwaka 2024.

Kuhusu mafanikio, Halili amesema Serikali imefanikiwa kulinda mwenendo wa mfumuko wa bei kwa kubakia ndani ya viwango vinavyokubalika kiuchumi, usiozidi asilimia tano huku ukuaji wa Pato la Taifa ukileta matumaini katika robo mbili za mwaka huu (Januari-Juni) ikilinganisha na miaka mitatu iliyopita.

“Kwa mfano, robo ya kwanza ya mwaka 2023 ukuaji ulikuwa asilimia 5.4 na robo ya pili ulikuwa asilimia 5.2, lakini katika kipindi hicho hicho kwa mwaka 2020 hadi 2022 ulikuwa chini ya asilimia tano, kwa hiyo ni mafanikio makubwa yaliyoonekana kwa mwaka huu, hivyo umakini uendelee,” amesema Halili.

Amesema jambo la kuvutia ni kiashiria cha kukua pato hilo kwa kasi miaka kumi ijayo ikilinganishwa na mataifa mengine yote ndani ya Afrika Mashariki kama ilivyonukuliwa na Shirika la Fedha duniani (IMF).

Hata hivyo, Halili ameonyesha wasiwasi katika tishio la urari hasi wa biashara katika mwenendo wa mahitaji ya ukuaji wa biashara za ndani katika masoko ya nje.

Amesema hatua ya uagizaji mkubwa wa bidhaa nje kuliko Tanzania inavyouza nje ni hatari katika usalama wa shilingi pamoja na akiba ya fedha za kigeni ikiwamo dola ya kimarekani.

“Hali inazidi kuwa mbaya kwa ushahidi wa miaka mitano mfululizo, mwaka 2017 hadi 2022. Takwimu za Benki ya Tanzania (BOT) zinaonyesha kiwango cha urari hasi kinaongezeka kutoka dola bilioni 2.78 mwaka 2017 hadi dola bilioni 6.98bilioni mwaka jana, hii sio dalili nzuri,” amesema Halili.

Kuhusu Dola, Halili amesema sarafu hiyo inayotumia kwa zaidi ya asilimia 80 katika miamala ya kimataifa, imetikisa uchumi wa Taifa kupitia mahitaji muhimu. Lakini amesema hali hiyo ilitengeneza wanufaika na waathirika katika jamii.

“Wastani wa shilingi ukilinganisha na nguvu ya Dola ulifikia Sh2, 507 ikilinganishwa na tofauti ya Sh2, 300 Januari mwaka huu, sawa na ongezeko la Sh210. Hii ilikuwa ni ongezeko kubwa,” amesema.