Maeneo yaliyoachwa na wapigania uhuru kupandishwa hadhi

Baadhi ya washiriki wa mbio za Kongwa African Liberation Marathon wakianza kutimua mbio zinazolenga kutangaza utalii wa Wilaya ya Kongwa.
Muktasari:
- Wilaya ya Kongwa imefanya mbio za Ukombozi wa Waafrika, lengo likiwa ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyomo wilayani humo, huku Serikali ikiweka wazi mchakato wa kutangaza maeneo yaliochwa na wapigania uhuru kuwa ni sehemu ya uridhi wa utamaduni wa Tanzania.
Kongwa. Wizara ya Maliasili na Utalii, imeanza mchakato wa kutangaza maeneo yaliyoachwa na wapigania uhuru Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma kuwa ni urithi wa utamaduni wa Tanzania.
Hatua hiyo, inatokana na maeneo hayo kuwa na historia ya kuwahifadhi wanaharakati waliokuwa wanapigania uhuru wa nchi zao hasa za Kusini mwa Bara la Afrika.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Prisca Kirway ameyasema hayo jana Jumamosi Novemba 25, 2023 wakati akizungumza kwenye mbio za ‘Kongwa African liberation Marathon’ zenye lengo la kutangaza maeneo yaliyoachwa na wapigania uhuru.
Prisca amesema historia hiyo iliyoachwa wakati wa kipindi cha kupigania uhuru na ukombozi wa bara la Afrika ni kubwa na adhimu ambayo inafaa kurithishwa kwa kila kizazi cha Watanzania na dunia kwa ujumla.
Amesema Kongwa ilikuwa ni sehemu na kitovu cha kuhifadhi wapigania uhuru wa nchi za Afrika, hivyo kuna kila sababu za kuhakikisha maeneo hayo yaliyoachwa yanahifadhiwa na kuendelezwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Kwa kuzingatia hilo Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo ina dhamana ya kutangaza maeneo ya utamaduni nchini, inakamilisha utaratibu wa kuhakikisha eneo hilo linaingia kwenye orodha ya urithi wa utamaduni wa Tanzania,” amesema.
Naye, Msimamizi na Mratibu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi barani Afrika, Boniface Kadili amesema baada ya Kongwa kutangazwa kuwa urithi wa Taifa watafanya mchakato ili iwe urithi wa dunia kwa sababu ina vigezo vyote.
Bila kutaja kiasi, amesema Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya kusaidia katika maeneo ya urithi yaliyopo hapa nchini likiwemo eneo hilo.
Amesema kutokana na kupendwa huko ndiyo maana baadhi ya wapigania uhuru walianzisha familia na wenyeji na wapo watoto walioachwa na wapigania uhuru hao kwenye eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remidius Mwema amesema watu wengi walikuwa hawajui kama Wilaya ya Kongwa ina makambi ya wapigania uhuru wa nchi za Namibia, Angola, Afrika Kusini, Msumbiji na Zimbabwe, hivyo wana wajibu wa kutangaza ili dunia ijue.