Mafuriko Turiani 45 waokolewa, nyumba 13 zabomoka

Mkazi wa  Msufini Kata ya Muhonda wilayani Mvomero, akiwa amebebwa na askari wa Jeshi la Zimamoto baada ya kuokolewa aliposombwa na mafuriko Aprili 11, 2024  Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Mafuriko hayo yalitokana na mvua kubwa zilizonyesha mkoani Arusha usiku wa kuamkia Aprili 11 ambapo maji yake hupita katika wilaya hiyo kupitia mto Mbulumi.

Morogoro. Kamanda wa jeshi la zimamoto na Uokoaji mkoa wa Morogoro Shaban Marugujo amethibitisha kuokolewa kwa 45 ambao walisombwa na maji yaliyotokana na mafuriko ambayo yalitokea Aprili 11, 2024 Turiani, Wilayani Mvomero.

Mafuriko hayo yalitokana na mvua kubwa zilizonyesha mkoani Arusha usiku wa kuamkia Aprili 11 ambapo maji yake hupita katika wilaya hiyo kupitia mto Mbulumi.

"Aprili 11,2024 majira ya saa 11 jioni tulipokwa taarifa za uwepo wa mafuriko kijiji cha Kichangani, kata ya Muhonda Turiani, tulifanya jitihada za kufika, tulikuta maji ni mengi ndipo tukaanza zoezi la uokoaji mara moja zoezi ambalo tumelifanya kwa weledi mkubwa na mafanikio"

Mbulumi amesema mpaka sasa wamefanikiwa kuokoa watu 45 ambao walikuwa tayari wamesombwa na mafuriko hayo, wote ni wazima hakuna aliyepoteza maisha, na waliookolewa tumefanikiwa kuwaleta nchi kavu ambapo wengi wao walikua ni wazee na watoto kutoka vitongoji viwili cha  Msufini.

“Kutokana na Mafuriko hayo jumla ya nyumba 13 zimebomoka kutokana na Mafuriko hayo, Sababu za mafuriko haya ni mvua zilizonyesha juzi mkoani Arusha na kusababisha mto Mbulumi unaopita Turiani kufurika na kumwaga maji hayo katika vitongoji hivyo viwili, hakuna madhara kwa binadamu zaidi ya nyumba kubomoka"

Mussa Juma mkazi wa Turiani anasema mto Mbulumi hupitisha maji wakati wote lakini maji ya jana yalizidi kwakuwa yalikuja kwa wingi pamoja na kwamba ilikua mchana.

"Tulikua tunaendelea na shughuli zetu mara tukaanza kuona maji yanaongezeka kwenye makazi ya watu, nilipompigia jirani yangu ambaye alikwenda dukani naye akasema hata huko Dukani maji ni mengi, baada ya hilo kutokea tukaanza jitihada za kujiokoa. Mimi na familia yangu tulifanikiwa kwenda kwa jirani yetu ambaye alikua kwenye mlima kidogo tukajihifadhi na hatukupata madhara ila maji yalikua mengi," amesema Juma.

Juma anasema mafuriko katika maeneo hayo huwa hayatokei mara kwa mara lakini kitendo mto Mbulumi kujaa ndicho kilichosababisha changamoto hiyo na mpaka wakati anaozungumza baadhi ya nyuma zilikuwa bado ziko kwenye maji.

Kwa upande wake Peter Damiani mkazi wa kitongoj cha msufini anasema kitongoji chao ndicho kimeathirika zaidi na mafuriko hayo huku hivyo aliiomba Serikali mitaro mikubwa itakayosaidia maji kupita pale mafuriko yanapotokea

"Kitongoji chetu cha Msufini kimeongoza kwa maeneo mengi kujaa maji, na kwa jinsi yale mafuriko yalivyotokea ni kwakua hakuna mitaro mikubwa ya kupitisha maji maana maji yalipojaa kwenye mto kama kungekua na mitaro mikubwa maji yasingefika kwenye makazi ya watu,” amesema.

Damiani anaiomba Serikali msaada wa chakula na makazi kwa familia ambazo zimeathiriwa zaidi na mafuriko hayo akisema mpaka sasa kuna watu hawana nyuma wala uhakika wa chakula baada ya mafuriko hayo.

Katika hatua nyingne kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wananchi wa mkoa wa Morogoro wameshauriwa kuchukua tahadhali dhidi ya wanyama wanaohama na maji akiwemo wakiwemo mamba pamoja na viboko.

Tahadhali hiyo haishii kwa Morogoro tu kwani mvua kubwa zinazoendelea zimesababisha hali inayofanana katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Arusha, Mbeya, Mwanza hivyo wananchi wa maeneo hayo wameaswa kuwa makini kipindi hiki cha mafuriko ili wasiliwe na wanyama hao wakali

Akizungumza na Mwananchi Leo Aprili 12,2024 Mhifadhi Gilbert Magafu amesema kipindi hiki cha mafuriko wanyama Mamba na Viboko wanahama na maji mengi hususan ya mafuriko hivyo wananchi wawe makini

"Mamba ni Mnyama jamii ya mjusi ambaye maisha yake kwa asilimia kubwa yanakua kwenye maji lakini wakati mwingine utamkuta nchi kavu, na anapokuwa nchi kavu huwa anaota jua na wakati mwingine huwa kwenye mawindo”.

Ameongeza “Mamba ana uwezo wa kuogelea umbali wa kilometa 32 kwa saa moja, hivyo huyu mnyama kipindi hiki cha Mvua nyingi watafika kwenye makazi ya binaadamu kwa kusombwa au kusafiri  na maji hivyo tahadhari zinapaswa kuongezeka ili tusipate shida ya watu kuliwa na mamba wakati huu wa mafuriko"

Anasema tabia za mnyama Mamba ni kuwinda kwa kushtukiza ndiyo maana watu wengi wanaliwa na sasa kwakua Maeneo mengi kama Ifakara, Rufiji yamekuwa na mafuriko mara kwa mara wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kuchukua tahadhari ili wasiliwe na mnyama huyu.

“Kwa uchunguzi ambao tumeufanya ni kwamba mpaka sasa wanyama hao wako kwenye makazi ya watu baada ya kusombwa na Mafuriko hivyo wananchi watoe taarifa kwa viongozi wao pale watakapoona wanyama hao hatarishi ili wakaondolewe mara moja"

"Mamba ni mnyama mwenye akili mno, anaweza kukaa kwenye maji kwa zaidi ya saa moja bila kutoka kupumua, na ana uwezo wa kuona akiwa ndani ya maji, sasa kwa kuwa maeneo mengi hapa nchini kuna maji yametuama wananchi wanapaswa kuacha kufanya shughuli zao pale hasa zile za kufua nguo, kuvua samaki, kuchota"