Magufuli atajwa tena kesi ya Sabaya

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akishuka kwenyw gari la Magereza leo wakati Rufaa yake ya kupinga hukumu ya miaka 30 iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ilipotajwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

Kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita imeendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Arusha, ambapo shahidi wa 13 amedai kuwa, kiongozi huyo alidai kupewa cheo na Hayati Rais John Magufuli cha Mkuu wa kikosi kazi maalum cha kupambana na uhujumu uchumi Kanda ya Kaskazini.

Arusha. Rais wa awamu ya tano Hayati John Magufuli ametajwa tena katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake sita.

Akizungumza leo Januari 7, Shahidi wa 13 ambaye ni Ofisa Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kupamana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Ramadhan Juma ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa, Sabaya alijitambilisha kama Mkuu wa kikosi kazi maalum cha kupambana na uhujumu uchumi Kanda ya Kaskazini.

Alisema Sabaya alitumia cheo alipofika gereji ya mfanyabiashara Francis Mrosso, akidai kuwa cho hicho alipewa na Rais Magufuli.

Akihojiwa na Wakili wa utetezi, Sylvester Kahunduka, mbele ya Hakimu Mkazi Patricia Kisinda, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa walipomkamata Sabaya na wenzake jijini Dar es Salaam, walimkamata na fedha ambazo ni mazalia ya rushwa katika tuhuma zingine zinazomkabili.

Sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Shahidi si kweli ulieleza mahakama walivyofika kwa Mrosso, Sabaya alijitambulisha mkuu wa Kikosi Maalum cha Kupamabana na Uhujumu Uchumi Kanda ya Kaskanzini?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Na akasema cheo hicho amepewa na Rais Magufuli?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Katika uchunguzi wako ulibaini aliteuliwa na Rais Magufuli kwa cheo hicho?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Lakini ulifanyia uchunguzi hilo suala?

Shahidi: Ndiyo nilifanyia uchunguzi.

 Wakili: Ulibaini kitu gani?

Shahidi: Nikabaini kwamba Sabaya ni mtu ambaye anamiliki genge la kihalifu na yeye ndiyo kiongozi wa genge hili. Niligundua hakuwahi kuteuliwa (kwa cheo hicho).

Wakili: Shahidi ulisema umebaini Sabaya anaongoza genge la uhalifu na wanafanya matukio Kilimanjaro na Arusha?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Na ukasema wanatumia silaha za moto?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Si kweli katika ushahidi wako wa msingi hakuna tukio hata moja ulitaja walilotumia silaha za moto?

Shahidi: Nilitaja tukio la uporaji duka la mapazia Arusha.

Wakili: Si kweli kwenye ushahidi wako hukusema mmekamata silaha ya moto?

Shahidi: Walikamatwa na silaha Dar es Salaam.

Wakili: Hiyo silaha imepatikana kihalali au kwa njia za kihalifu?

Shahidi: Uchunguzi unaendelea kuhusiana na hilo kwani ana tuhuma nyingi.

Wakili: Tukubaliane silaha hiyo siyo sehemu ya kesi hii?

Shahidi: Kabisa

Wakili: Tunakubaliana kwamba washitakiwa wote walikaa zaidi ya saa 48 kabla ya kupandishwa mahakamani?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Unafahamu kwamba sheria inataka ndani ya sa 24 wafikishwe mahakamni?

Shahidi: Walikuwa na tuhuma nyingine nyingi ndiyo maana hawakupelekwa mahakamani.

Wakili: Haiwezekani kuletwa mahakamani wakati uchunguzi unaendelea?

Shahidi: Inategemea na mazingira ila inawezekana.

Wakili: Si tunakubaliana kabisa wewe kama mchunguzi hakuna mtu hata mmoja ulimchukua maelezo ya onyo watihumiwa wote?

Shahidi: Ndiyo sikuwahi kuchukua hata mmoja.

Wakili: Si kweli kwamba Julai 18, 2021 ulikwenda magereza ya Arusha kwa lengo la kuchukua maelezo ya baadhi ya watuhumiwa?

Shahidi: Ndiyo nilikwenda.

Wakili: Na si kweli kati ya watu ulitaka kuwahoji ni mshitakiwa wa kwanza Sabaya?

Shahidi: Ni kweli ndiyo.


Wakili: Si kweli kwamba hukufanikiwa kuchukua maelezo ya Sabaya?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Na si kweli kwamba alikwambia kwamba wewe unashirikiana na wafanyabiashara kum fix kwa hiyo hayuko tayari kutoa maelezo mbele yako?

Shahidi: Si kweli.

Wakili: Kwanini hukufanikiwa?

Shahidi: Alisema anahitaji kuwa na wakili wake, alisema hawezi kuhojiwa pasipokuwa na wakili wake.

Wakili: Ulikuwa na kibali kwenda magereza kuwahoji watihumiwa wakati kesi inaendelea?

Shahidi: Ndiyo nilikuwa na kibali na sikwenda kumhoji Sabaya kwa kesi iliyopo mahakamani, nilienda kumhoji kuhusiana na tuhuma zingine.

Wakili: Unafahamu Hakimu anayeendesha kesi ndiye anapaswa kukupa kibali?

Shahidi: Sikwenda kumhoji Sabaya kuhusiana na kesi iliyopo mahakamani, nilienda kumhoji kuhusiana na tuhuma nyingine na niliomba kibali kwa sababu kwenda magereza kuna utaratibu.

Wakili: Uliomba kwa Hakimu gani?

Shahidi: Ni ofisi ilifanya mchakato na sikumbuki jina la Hakimu.

Wakili: Shahidi ulisema kwamba kuna mgao wa hizi fedha ulifanyika ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi?

Wakili: Na ulisema ulifanyikia Tulia hotel ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi

Wakili: Na vilevile ukasema rushwa ilikuwa inagaiwa na mmoja mmoja chumbani?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Si kweli wewe hukuwepo wakati fedha zinagawanywa?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Si kweli hata watuhumiwa hakuna mwingine akiyekuwepo wakati mwenzake anapewa pesa

Shahidi: Ni kweli

Wakili: Lakini ukipata taarifa za kuhusu mgao

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Nani alikupa taarifa za mgao?

Shahidi: Ni taarifa za siri/fiche

Wakili:Sasa hizii taarifa fiche uluvyozipata ulithibitishaje ndivyo mgao ulivyokuwa?

Shahidi:Nilithibitisha baada ya kufanya mahojiano ya awali na  kuthibitisha kuwa walipata mgao wa pesa

Wakili:Hawa watu walikupa maelezo hayo bila kuwahurutisha?

Shahidi:Ndiyo

Wakili:Ni kwanini watu hao wako tayari kutoa taarifa nyeti hizo na hukuandika maelezo yao na kusaini na siyo kwamba unawasingizia hapa mahakamani

Shahidi:Maelezo yapo

Wakili:Hebu iambue mahakama gari namba  T 222 BDY ni kwanini mmelileta mahakamani kwenye kesi hii?

Shahidi:Tumeileta kama sehemu ya kielelezo

Wakili:Ni kwamba ilishiriki kupokea rushwa?

Shahidi:Ni kielelezo ambacho ni zao la rushwa.Kimepatikana baada ya Sabaya akishirikiana na genge la vijana wake kuomba  na kupokea rushwa ya Sh 90 milioni toka kwa Francis Mrosso

Wakili:Niko sahihi nikisema mlileta kwa sababu ni zao la pesa chafu?

Shahidi:Ni zao la rushwa

Wakili:Una uthibitisho gani kwamba hizo pesa za ryshwa ndo zimeznunulia gari hilo?

Shahidi:Gari hii imenunuliwa siku 10 baada uya tukio la kuomba na kupokea rushwa ya Sh 90 milioni .Katika uchunguzi wangu jiliangalia taasisi za fedha Sabaya hakuwa na mkopo hii pekee yake ilitosha kuthibitisha gari hii ni zao la rushwa

Wakili:Unakubaliana na mimi kwamba kabla ya Januari 22,2021 Sabayaa alikuwa na uwezo wa kumiliki magari?

Shahidi:Ndiyo nakubaliana

Wakili:katika uchunguzi wako sasa kuna sehemu  ambayo umeona amekopa kwa ajili ya kununua hayo magari kabla ya Januari 22?

Shahidi:Sikufanyia magari aliyokuwa nayo kabla

Wakili:Katika uchunguzi wako uliweza kubaini sabaya aliwahi kuwa mkt wa UVCCM mkoa?

Shahidi: Ndiyo

Wakili:Hivyo vitu viwili si kazi ambazo zinaingiza kipato?

Shahidi:Ndiyo

Wakili:akqa hiyo mtu huyu alikuwa na maisha kabla ya kuteuliwa Mkuu wa Wilaya Hai?

Shahidi: Ni sahihi

Wakili: Unafahamu watuhumiwa kwa pamoja wanatuhumiwa kutakatisha fedha Sh90 milioni?

Shahidi: Ndiyo nafahamu

Wakili: Sasa lile gari unalosema ni zao lilinunuliwa kwa Shilingi ngapi na Sabaya?

Shahidi: Sh60 milioni.

Wakili: Katika 90 milioni ambazo zilichukuliwa ukitoa Sh60 milioni inabaki shilingi ngapi?

Shahidi: Sh30 milioni.

Wakili: Si ni kweli katika ushahidi wako wote hakuna sehemu umeeleza Sh30 milioni zimetumika kwa namna gani?

Shahidi: Nilieleza kuna mgao alifanya kwa vijana wake na nilitaja mgao wa pesa na nilisema waliendelea kunywa na kuburudika pale Tulia hotel na pesa iliyobaki ilinunua gari

Wakili: Waliburudika kwa shilingi ngapi?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Jana ulikiri kuna fedha ambazo mlizikamata.

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Kwa nini mmezikamata?

Shahidi: Tumezikamata kwa sababu nazo ni pesa ambazo ni mazalia ya rushwa.

Wakili: Rushwa ya Sh90 milioni?

Shahidi: Hapana kuna tuhuma nyingi ambazo zinaendelea. Tunachakata tuhuma mbalimbali ndiyo maana kuna vielelezo vimekuja kwenye kesi hii na vingine vitakuja kwenye kesi nyingine

Wakili: Sabaya siku hiyo mlimkataka kwa kosa gani?

Shahidi: Ilikuwa ni kesi nyingine.

Wakili: Pesa mlizokamata zina alama gani tofauti na zilizochukuliwa kwa Mrosso?

Shahidi: Sikuziona zilizokamatwa kwa Mrosso kwa sababu ziliingia kwenye mzunguko.

Wakili: Unasema Sabaya ana kesi nyingine na aliandika maelezo ile maelezo alionywa kwa kesi gani?

Shahidi: Alionywa kwa kosa la kuomba kupokea rushwa, kuratibu genge la kihalifu na matumizi mabaya ya mamlaka.

Baada ya ushahidi huo, Hakimu Kisinda ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 10, ambapo shahidi wa 14 wa Jamhuri ataanza kutoa ushahidi wake.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27 ya mwaka huu, bali na Sabaya, washitakiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.