Mahakama Kuu kujengwa kila mkoa

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma akifungua jengo la mahakama ya wilaya ya Busega. Picha na Samirah Yusuph.
Muktasari:
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema serikali iko mbioni kuanza kujenga majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ambayo haina majengo hayo ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma.
Busega. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema serikali iko mbioni kuanza kujenga majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ambayo haina majengo hayo ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma.
Katika taarifa yake aliyoitoa leo Ijumaa Novemba 25, 2022 wakati wa hafla ya ufunguzi wa majengo 18 ya mahakama za wilaya nchini iliyofanyika kwa niaba wilayani Busega mkoani Simiyu imesema hatua hiyo ni kutimiza haki ya kila mwananchi kupata huduma katika maeneo yake.
Majengo ya mahakama yaliyofunguliwa ni jengo la mahakama ya wilaya ya Busega, Itilima, Butiama, Rorya, Songwe, Gairo, Nkinga, Mbogwe, Nyanh'wale, kyelwa, Misenyi, kaliua, Uvinza, Buhigwe, Mvomero, Kakonko, Tanganyika na Kilombero.
Amesema 2015 Mahakama ya Tanzania ilifanya thatmini ya kina kuhusu uhaba na uchakavu wa majengo ya mahakama nchi nzima na iliandaa ripoti ya tathmini ikionyesha kwajumla ya wilaya 104 kati ya 139 za Tanzania bara zilikuwa zinahitaji majengo mapya ya mahakama.
"Tunaendelea kukubali kwamba maeneo mengi ya nchi yetu yanasubiri majengo mfano Mkoa wa Simiyu bado unasubiri jengo la Mahakama Kuu.
Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inampango wa kuhakikisha mikoa yote ambayo haina majengo ya Mahakama Kuu yataanza kujengwa kuanzia mwaka ujao," amesema Profesa Ibrahim.
Mikoa itakayonufaika na ujenzi huo imetajwa kuwa ni Pwani, Manyara, Lindi, Singida, Geita Songwe, Simiyu, Njombe na Katavi na majengo hayo yanatarajiwa kukamilika ifikapo 2024.
Ameongeza kuwa aina hii ya maboresho ya miundombinu ya mahakama inalenga na kumthamini mwananchi wa chini na kuchangamsha uchumi kwa kuwa wananchi wataepuka adha ya kutembea umbali mrefu hivyo watapata huduma Karibu ili wawahi kufanya shughuli za kujiingizia kipato.
Taarifa ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante ole Gabriel imebainisha gharama za ujenzi wa mahakama hizo kote nchini kuwa ni Sh18.3 bilioni ambazo ni wastani wa Sh1 bilioni kwa kila mahakama sambamba na samani ambazo zimagharimu Sh2.9 bilioni.