Mahakama yabatilisha mwenendo, hukumu ya aliyetuhumiwa kumuua mkewe

File Photo
Muktasari:
- Jopo la majaji watatu baada ya kupitia mwenendo na adhabu ya kifungo cha maisha jela alichohukumiwa Mateso Shantiwa, mkazi wa Mbeya, imeamuru shauri hilo lisikilizwe upya na Mahakama Kuu baada ya kubaini dosari za kisheria wakati wa usikilizwaji.
Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha mwenendo wa kesi na kufuta hukumu ya kifungo cha maisha jela, alichohukumiwa Mateso Shantiwa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe, Zaina Mlela.
Pia, Mahakama hiyo imeamuru kumbukumbu za kesi hiyo zipelekwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa upya kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, mrufani atasalia kizuizini akisubiri kesi yake kusikilizwa upya.
Uamuzi huo umetolewa jana, Julai 10, 2024, baada ya Mahakama ya Rufani kubaini dosari za kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kukubaliana na hoja za pande zote, kuwa Mahakama iliyosikiliza kesi hiyo ilikosea kisheria kwa kumkuta mrufani na hatia bila kufuata utaratibu wa kukabidhiana jalada la kesi kutoka kwa hakimu mmoja kwenda kwa aliyeandaa hukumu.
Rufaa hiyo ya jinai namba 106/2021 ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Barke Seleh, wengine ni Ignas Kitusi na Issa Maige.
Rufaa hiyo ilitokana na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, iliyosikiliza kesi hiyo baada ya hakimu kupewa mamlaka ya nyongeza ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji, Oktoba 15, 2021.
Mrufani huyo alisomewa mashtaka chini ya kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, kwa tuhuma za mauaji ya mkewe yaliyofanyika katika Kijiji cha Kitusi, mkoani Mbeya.
Mahakama hiyo ilijiridhisha kuwa mashahidi saba wa upande wa mashtaka walithibitisha kesi hiyo na mrufani kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Jaji Kitusi amesema kwa kuwa uamuzi wao hauhusiani na maelezo ya ushahidi, wataruka kipande hicho.
Mrufani huyo aliyewakilishwa na Wakili Irene Mwakyusa aliwasilisha sababu nane za kukata rufaa huku upande wa mjibu rufaa ukiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Xaveria Makombe.
Wakili Mwakyusa aliwasilisha hoja moja ya msingi wa rufaa na kuacha sababu nyingine, kwamba Mahakama ya awali ilikosea kisheria kwa kumtia hatiani mrufani bila kufuata utaratibu wa Mahakama.
Jaji Kitusi alisema kwa kuangalia kiini cha rufaa hiyo, wataanza kwa kuangalia jinsi kesi ya msingi iliendeshwa na nani aliyeiendesha.
Amesema ni jambo la kawaida mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji yako kwa Mahakama Kuu isipokuwa pale ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi na hakimu maalumu aliyeongezewa mamlaka.
Jaji Kitusi amesema hukumu iliyokatiwa rufaa iliandaliwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Laizer, lakini wasiwasi wao ni iwapo kulikuwa na kufuatwa utaratibu wa kuhamisha kesi hiyo kutoka kwa Hakimu Mkazi Mwandamizi Richard Chaungu ambaye alirekodi ushahidi wa shahidi wa kwanza hadi wa tatu.
Amesema Julai 12, 2018, kesi hiyo ilihamishiwa kwa Hakimu Mkazi Mwandamizi Mutaki, ambaye alirekodi usikilizwaji wa awali Agosti 20, 2018.
Jaji alifafanua kuwa kwa sababu ambazo hazijaingizwa kwenye rekodi, Oktoba 2, 2019, kesi ilianza kusikilizwa mbele ya Hakimu Chaungu na alirekodi mashahidi hao watatu.
Amesema bado kuna amri nyingine ya uhamisho ya Juni 12, 2020, wakati huo ambapo Hakimu Laizer alihitimisha rekodi ya ushahidi wa mashahidi waliosalia na kutoa hukumu.
Akinukuu hukumu za kesi zilizowahi kutolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani, ni wazi kuwa hakukuwa na amri ya kuhamishia kesi hiyo kwa Hakimu Chaungu, hivyo ilifanyika bila mamlaka na hata ushahidi uliorekodiwa ni wa kimakosa.
Wakili Xaveria alikubaliana na hoja ya Wakili Irene juu ya ubatili wa mashauri yaliyozaa hukumu hiyo, wakitolea mfano kesi ya rufaa ya jinai namba 545/2017 ya Nasra Hamisi iliyotupiliwa mbali, akasisitiza Mutaki ambaye kesi ilihamishiwa alikuwa na wajibu wa kuendelea nayo mpaka mwisho.
Jaji Kitusi amesema katika kulitafakari suala hili, wanakubaliana na mawakili wote wawili kwamba kifungu cha 256A (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinamtaka Hakimu Mutaki kuendelea na kesi hadi mwisho.
“Kesi kuchukuliwa na Laizer, ingawa kulifuata utaratibu wa uhamisho, hakukurekebisha makosa ya Hakimu Mutaki kutokuendelea na kesi ile na Hakimu Chaungu kuichukua. Kwa hiyo, tunapata sifa katika msingi wa rufaa na kuikubali. Tunabatilisha mwenendo mzima, tunafuta hukumu,” amesema Jaji Kitusi.
“Kwa kuzingatia mrufani amekuwa kizuizini kwa miaka saba, kwa maoni yetu tunahitaji kusawazisha kati ya haki za mrufani, kwamba hakuna ushahidi, isipokuwa wa kimazingira, wa kumhusisha mrufani, na wajibu wa upande wa mashtaka ni kuthibitisha madai ya uhalifu.
“Kwa hiyo, kwa ajili ya kujiepusha na shaka, tunabatilisha shauri, tunafuta hukumu, tunaamuru rekodi hiyo ipelekwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa upya kwa mujibu wa sheria. Wakati huo, mrufani atabaki kizuizini,” amesema Jaji Kitusi.